Ezekieli 45:18-25
Ezekieli 45:18-25 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, mtatambika fahali mdogo asiye na dosari ili kutakasa maskani yangu. Kuhani atatwaa baadhi ya damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuipaka miimo ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, kona za madhabahu, na miimo ya nafasi ya kuingilia kwenye ua wa ndani. Atafanya vivyo hivyo siku ya saba ya mwezi huo, kwa ajili ya kila mtu aliyetenda dhambi bila kukusudia au kwa kutojua. Kwa njia hiyo mtaitakasa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. “Siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, mtaadhimisha sikukuu ya Pasaka. Kwa muda wa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu. Siku hiyo, mtawala atatoa fahali mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu wote wa Israeli. Kila siku, katika muda huo wa siku saba, atamtolea sadaka Mwenyezi-Mungu fahali saba na kondoo madume saba wasio na dosari kwa kuwateketeza wazima. Tena ni lazima atoe sadaka kila siku ikiwa ni sadaka ya kuondoa dhambi. Kisha atatengeneza sadaka ya unga kilo 10 kwa kila fahali na kilo 10 kwa kila kondoo dume, halafu lita 3 za mafuta kwa kila kilo 10 za unga. “Katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, na kwa muda wa siku saba za sikukuu, mtawala atatoa mahitaji kwa ajili ya sadaka za kuondoa dhambi, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta.
Ezekieli 45:18-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Bwana MUNGU asema hivi; Mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, utatwaa ng'ombe dume mchanga na mkamilifu; nawe utapatakasa mahali patakatifu. Na kuhani atatwaa baadhi ya damu ya sadaka ya dhambi, na kuitia juu ya miimo ya milango ya nyumba, na juu ya pembe nne za daraja ya madhabahu, na juu ya miimo ya lango la ua wa ndani. Nawe utafanya vivyo hivyo katika mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi kwa ajili ya kila mtu akosaye, na kwa ajili ya mtu aliye mjinga, ndivyo mtakavyoifanyia nyumba upatanisho. Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, mtakuwa na Pasaka, sikukuu ya siku saba; mkate usiotiwa chachu utaliwa. Na siku hiyo mkuu atatengeneza ng'ombe kuwa sadaka ya dhambi, kwa ajili ya nafsi yake, na kwa ajili ya watu wote wa nchi. Tena, katika zile siku saba za sikukuu atamtengenezea BWANA sadaka ya kuteketezwa, ng'ombe saba na kondoo dume saba wakamilifu, kila siku kwa muda wa siku saba, na beberu mmoja kila siku kuwa sadaka ya dhambi. Naye atatengeneza sadaka ya unga, efa moja kwa ng'ombe, na efa moja kwa kondoo dume, na hini moja ya mafuta kwa efa moja; katika mwezi wa saba, siku ya kumi na tano ya mwezi, katika sikukuu atafanya vivyo hivyo kwa muda wa siku saba; sadaka ya dhambi vivyo hivyo, na sadaka ya kuteketezwa vivyo hivyo, na sadaka ya unga vivyo hivyo, na mafuta vivyo hivyo.
Ezekieli 45:18-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Bwana MUNGU asema hivi; Mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, utatwaa ng’ombe mchanga mume mkamilifu; nawe utapatakasa mahali patakatifu. Na kuhani atatwaa baadhi ya damu ya sadaka ya dhambi, na kuitia juu ya miimo ya milango ya nyumba, na juu ya pembe nne za daraja ya madhabahu, na juu ya miimo ya lango la ua wa ndani. Nawe utafanya vivyo hivyo katika mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi kwa ajili ya kila mtu akosaye, na kwa ajili ya mtu aliye mjinga, ndivyo mtakavyoifanyia nyumba upatanisho. Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, mtakuwa na Pasaka, sikukuu ya siku saba; mkate usiotiwa chachu utaliwa. Na siku hiyo mkuu atatengeneza ng’ombe kuwa sadaka ya dhambi, kwa ajili ya nafsi yake, na kwa ajili ya watu wote wa nchi. Tena, katika zile siku saba za sikukuu atamtengenezea BWANA sadaka ya kuteketezwa, ng’ombe saba na kondoo waume saba wakamilifu, kila siku kwa muda wa siku saba, na beberu mmoja kila siku kuwa sadaka ya dhambi. Naye atatengeneza sadaka ya unga, efa moja kwa ng’ombe, na efa moja kwa kondoo mume, na hini moja ya mafuta kwa efa moja; katika mwezi wa saba, siku ya kumi na tano ya mwezi, katika sikukuu atafanya vivyo hivyo kwa muda wa siku saba; sadaka ya dhambi vivyo hivyo, na sadaka ya kuteketezwa vivyo hivyo, na sadaka ya unga vivyo hivyo, na mafuta vivyo hivyo.
Ezekieli 45:18-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“ ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Katika mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya huo mwezi utamchukua fahali mchanga asiye na dosari na kutakasa mahali patakatifu. Kuhani itampasa achukue sehemu ya hiyo damu ya sadaka ya dhambi na kuipaka kwenye miimo ya Hekalu, kwenye pembe nne za juu za ukingo wa hayo madhabahu na juu ya miimo ya lango la ukumbi wa ndani. Itakupasa kufanya vivyo hivyo katika siku ya saba ya mwezi huo kwa ajili ya mtu yeyote ambaye hutenda dhambi bila kukusudia au bila kujua, hivyo utafanya upatanisho kwa ajili ya Hekalu. “ ‘Katika mwezi wa kwanza siku ya kumi na nne utaadhimisha Pasaka. Sikukuu itaendelea kwa siku saba, wakati huo wa hizo siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku hiyo mkuu anayetawala atatoa fahali kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu wote wa nchi. Kila siku wakati wa hizo siku saba za sikukuu atatoa mafahali saba na kondoo dume saba wasio na dosari kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA na beberu kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Pia atatoa sadaka ya nafaka efa moja kwa kila fahali na efa moja kwa kila kondoo dume, pamoja na hini moja ya mafuta kwa kila efa. “ ‘Wakati wa hizo siku saba za sikukuu, ambayo huanza katika mwezi wa saba kwenye siku ya kumi na tano, mkuu anayetawala atatoa mahitaji yale yale kwa ajili ya sadaka za dhambi, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta.