Ezekieli 9:1-11
Ezekieli 9:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha nikamsikia Mwenyezi-Mungu akisema kwa sauti kubwa: “Njoni karibu nyinyi mtakaouadhibu mji huu. Njoni na silaha zenu za kuangamiza.” Watu sita wakaja kutoka upande wa lango la juu linaloelekea kaskazini, kila mmoja na silaha yake ya kuangamiza mkononi mwake. Pamoja nao, alikuwapo mtu mmoja ambaye alikuwa amevaa mavazi ya kitani, naye ana kidau cha wino. Wakaingia ndani ya hekalu, wakasimama pembeni mwa madhabahu ya shaba. Kisha utukufu wa Mungu wa Israeli uliondoka pale juu ya kiumbe chenye mabawa na kupanda juu mpaka kizingiti cha nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa mavazi ya kitani, mwenye kidau cha wino, akamwambia, “Pita katikati ya mji wa Yerusalemu, ukatie alama kwenye vipaji vya nyuso za watu wanaohuzunika na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayotendeka katika mji huu.” Kisha akawaambia wale wengine mimi nikiwa nasikia, “Piteni mjini mkimfuata, mkaue watu; msimwachie yeyote wala msiwe na huruma. Waueni wazee papo hapo, wavulana kwa wasichana, watoto na wanawake; lakini kila mmoja mwenye alama, msimguse. Anzeni katika maskani yangu.” Basi, wakaanza na wazee waliokuwa mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Akawaambia, “Tieni unajisi nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa kuzijaza nyua zake maiti. Songeni mbele.” Basi, wakaenda, wakawaua watu mjini. Wakati walipokuwa wakiwaua, mimi niliachwa peke yangu, nikaanguka kifudifudi, nikalia, “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, je, utaangamiza watu wote wa Israeli waliobaki, ukitimiza ghadhabu yako juu ya Yerusalemu?” Naye akaniambia, “Uovu wa watu wa Israeli na watu wa Yuda ni mkubwa sana. Nchi imejaa umwagaji damu na mjini hakuna haki, kwani wanasema: ‘Mwenyezi-Mungu ameiacha nchi; Mwenyezi-Mungu haoni.’ Kwa upande wangu, sitawaachia wala kuwahurumia; nitawatenda kadiri ya matendo yao.” Kisha mtu yule aliyevaa mavazi ya kitani, mwenye kidau cha wino, akarudi na kutoa taarifa: “Nimefanya kama ulivyoniamuru.”
Ezekieli 9:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha akalia kwa sauti kuu masikioni mwangu, akisema, Waamuru wale wanaousimamia mji wakaribie, kila mmoja na awe na silaha ya kuangamiza mkononi mwake. Na tazama, watu sita wakaja, wakitokea kwa njia ya lango la juu, lielekealo upande wa kaskazini, kila mmoja akiwa na silaha yake ya kuua mkononi; na mtu mmoja kati yao akiwa amevaa bafta, naye ana kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Wakaingia, wakasimama karibu na madhabahu ya shaba. Na huo utukufu wa Bwana wa Israeli ulikuwa umepanda juu kutoka kwa kerubi, ambaye ulikuwa juu yake, mpaka kizingiti cha nyumba; akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa bafta, mwenye kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. BWANA akamwambia, Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, ukatie alama katika vipaji vya nyuso vya watu wanaopiga kite na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika kati yake. Na hao wengine aliwaambia, nami nilisikia, Piteni kati ya mji nyuma yake, mkapige; jicho lenu lisiachilie, wala msione huruma; Waueni kabisa, wazee, na viijana, na wasichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu yeyote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu. Basi, wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba. Akawaambia, itieni nyumba unajisi, mkazijaze nyua mizoga ya hao waliouawa; haya, nendeni. Wakaenenda, wakaua watu katika mji. Tena ikawa, walipokuwa wakiwaua, nami nikaachwa, nilianguka kifudifudi, nikalia, nikasema, Ee Bwana MUNGU! Utaangamiza mabaki yote ya Israeli, wakati wa kumwaga ghadhabu yako juu ya Yerusalemu? Ndipo akaniambia, Uovu wa nyumba ya Israeli na Yuda ni mwingi sana, nayo nchi imejaa damu, nao mji umejaa kupotosha hukumu; maana husema, BWANA ameiacha nchi hii, naye BWANA haoni. Nami, jicho langu halitaachilia, wala sitakuwa na huruma; lakini nitaleta njia yao juu ya vichwa vyao. Na tazama, mtu yule aliyevaa bafta, mwenye kidau cha wino kiunoni, akaleta habari, akisema, Nimefanya kama ulivyoniamuru.
Ezekieli 9:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha akalia kwa sauti kuu masikioni mwangu, akisema, Waamuru wale wanaousimamia mji wakaribie, kila mmoja na awe na kitu chake cha kuangamiza mkononi mwake. Na tazama, watu sita wakaja, wakitokea kwa njia ya lango la juu, lielekealo upande wa kaskazini, kila mmoja ana kitu chake cha kufisha mkononi mwake; na mtu mmoja kati yao amevaa bafta, naye ana kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Wakaingia, wakasimama karibu na madhabahu ya shaba. Na huo utukufu wa Bwana wa Israeli ulikuwa umepanda juu kutoka kwa kerubi, ambaye ulikuwa juu yake, mpaka kizingiti cha nyumba; akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa bafta, mwenye kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. BWANA akamwambia, Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, ukatie alama katika vipaji vya nyuso vya watu wanaougua na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika kati yake. Na hao wengine aliwaambia, nami nalisikia, Piteni kati ya mji nyuma yake, mkapige; jicho lenu lisiachilie, wala msione huruma; Waueni kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu ye yote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu. Basi, wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba. Akawaambia, itieni nyumba unajisi, mkazijaze nyua mizoga ya hao waliouawa; haya, enendeni. Wakaenenda, wakapiga-piga katika mji. Tena ikawa, walipokuwa wakipiga, nami nikiachwa, nalianguka kifudifudi, nikalia, nikasema, Ee Bwana MUNGU! Utaangamiza mabaki yote ya Israeli, wakati wa kumwaga ghadhabu yako juu ya Yerusalemu? Ndipo akaniambia, Uovu wa nyumba ya Israeli na Yuda ni mwingi sana, nayo nchi imejaa damu, nao mji umejaa kupotosha hukumu; maana husema, BWANA ameiacha nchi hii, naye BWANA haoni. Nami, jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; lakini nitaleta njia yao juu ya vichwa vyao. Na tazama, mtu yule aliyevaa bafta, mwenye kidau cha wino kiunoni, akaleta habari, akisema, Nimefanya kama ulivyoniamuru.
Ezekieli 9:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha nikamsikia akiita kwa sauti kubwa akisema, “Walete wasimamizi wa mji hapa, kila mmoja akiwa na silaha mkononi mwake.” Nami nikaona watu sita wakija toka upande wa lango la juu, linalotazama kaskazini kila mmoja na silaha za kuangamiza mkononi mwake. Pamoja nao alikuwepo mtu aliyekuwa amevaa mavazi ya kitani safi, naye alikuwa na vifaa vya mwandishi akiwa amevishikilia upande mmoja. Wakaingia ndani ya Hekalu wakasimama pembeni mwa madhabahu ya shaba. Basi utukufu wa Mungu wa Israeli ukaondoka hapo juu ya makerubi, ulikokuwa umekaa, ukaenda kwenye kizingiti cha Hekalu. Ndipo BWANA akamwita yule mtu aliyevaa kitani safi aliyekuwa na vifaa vya mwandishi akiwa amevishikilia upande wake mmoja, akamwambia, “Pita katika mji wote wa Yerusalemu ukaweke alama juu ya vipaji vya nyuso za wale watu wanaohuzunika na kuomboleza kwa sababu ya machukizo yote yanayotendeka katika mji huu.” Nikiwa ninasikia, akawaambia wale wengine, “Mfuateni anapopita katika mji wote mkiua, pasipo huruma wala masikitiko. Waueni wazee, vijana wa kiume na wa kike, wanawake na watoto, lakini msimguse mtu yeyote mwenye alama. Anzieni katika mahali pangu patakatifu.” Kwa hiyo wakaanza na wale wazee waliokuwa mbele ya Hekalu. Ndipo akawaambia, “Linajisini Hekalu na mkazijaze kumbi zake maiti za wale waliouawa. Nendeni!” Kwa hiyo wakaenda wakaanza kuua watu mjini kote. Wakati walikuwa wakiwaua watu, nami nilikuwa nimeachwa peke yangu, nikaanguka kifudifudi, nikapiga kelele nikisema, “Ee BWANA Mwenyezi! Je, utaangamiza mabaki yote ya Israeli, katika kumwagwa huku kwa ghadhabu yako juu ya Yerusalemu?” BWANA akanijibu, “Dhambi ya nyumba ya Israeli na Yuda imekuwa kubwa mno kupita kiasi, nchi imejaa umwagaji damu na mjini kumejaa udhalimu. Kwani wamesema, ‘BWANA ameiacha nchi, BWANA hauoni.’ Kwa hiyo sitawahurumia wala kuwaachilia lakini nitaleta juu ya vichwa vyao, yale waliyoyatenda.” Ndipo mtu yule aliyekuwa amevaa nguo ya kitani safi na vifaa vya mwandishi akiwa amevishikilia upande wake mmoja, akarudi na kutoa taarifa akisema, “Nimefanya kama ulivyoniagiza.”