Wagalatia 5:2-12
Wagalatia 5:2-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Sikilizeni! Ni mimi Paulo ninayesema nanyi! Kama mkikubali kutahiriwa, Kristo hatawafaidia chochote. Nasema tena wazi: Kila anayekubali kutahiriwa itambidi kuishika sheria yote. Kama mnatazamia kufanywa waadilifu kwa njia ya sheria, basi, mmejitenga mbali na Kristo; mko nje ya neema ya Mungu. Kwa upande wetu, lakini, sisi tunangojea kwa matumaini kwa nguvu ya Roho tufanywe waadilifu kwa njia ya imani. Maana ikiwa tumeungana na Kristo Yesu, kutahiriwa au kutotahiriwa hakuna maana; cha maana ni imani ifanyayo kazi kwa mapendo. Mwenendo wenu ulikuwa mzuri! Nani, basi, aliyewazuia kuuzingatia ukweli? Aliyesababisha hali hiyo si Mungu ambaye amewaiteni. “Chachu kidogo tu huchachusha donge lote la unga!” Kutokana na kuungana kwetu na Bwana, nina tumaini kubwa kwamba nyinyi hamtakuwa na msimamo tofauti nami. Tena yeyote huyo anayewavurugeni – awe nani au nani – hakika ataadhibiwa. Na kwa upande wangu, ndugu zangu, kama bado ninahubiri kwamba kutahiriwa ni lazima, kwa nini basi, bado ninadhulumiwa? Kama ingalikuwa hivyo, mahubiri yangu juu ya msalaba wa Kristo yasingalileta aibu yoyote. Laiti hao wanaowavurugeni wangejihasi wenyewe!
Wagalatia 5:2-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tazama, mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidi neno. Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kuitimiza torati yote. Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema. Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani. Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutotahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo. Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli? Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi. Chachu kidogo huchachua donge zima. Nina matumaini kwenu katika Bwana, ya kwamba hamtakuwa na nia ya namna nyingine. Lakini yeye anayewasumbua atachukua hukumu yake, awaye yote. Nami, ndugu zangu ikiwa ninahubiri habari ya kutahiriwa, kwa nini ningali ninaudhiwa? Kwa kufanya hivyo kikwazo cha msalaba kimeondolewa! Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao!
Wagalatia 5:2-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tazama, mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia neno. Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kuitimiza torati yote. Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema. Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani. Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo. Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli? Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi. Chachu kidogo huchachua donge zima. Nina matumaini kwenu katika Bwana, ya kwamba hamtakuwa na nia ya namna nyingine. Lakini yeye anayewafadhaisha atachukua hukumu yake, awaye yote. Nami, ndugu zangu ikiwa ninahubiri habari ya kutahiriwa, kwa nini ningali ninaudhiwa? Hapo kwazo la msalaba limebatilika! Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao!
Wagalatia 5:2-12 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba mkikubali kutahiriwa, basi Al-Masihi hatakuwa na thamani kwenu hata kidogo. Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika Torati yote. Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kupitia kwa Torati mmetengwa na Al-Masihi, mko mbali na neema ya Mungu. Kwa maana, kupitia Roho wa Mungu tunangojea kwa shauku tumaini la haki kwa imani. Kwa maana ndani ya Al-Masihi Isa, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kupitia kwa upendo. Mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msiitii kweli? Ushawishi kama huo haukutoka kwa yule anayewaita. “Chachu kidogo huchachua donge zima.” Nina hakika katika Bwana Isa kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu anayewachanganya anastahili adhabu, hata awe nani. Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini bado ninateswa? Katika hiyo hali basi, kwazo la msalaba limeondolewa. Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe!