Mwanzo 1:1-31
Mwanzo 1:1-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza. Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja. Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji. Mungu akalifanya anga, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo. Mungu akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili. Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo. Mungu akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo. Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu. Mungu akasema, Na iwe mianga katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili na majira na siku na miaka; tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi; ikawa hivyo. Mungu akafanya mianga miwili mikubwa, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi na kuutawala mchana na usiku na kutenga nuru na giza; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya nne. Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na kitu kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu. Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao, na kila ndege arukaye, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akavibarikia, akisema, Zaeni, mkaongezeke, mkayajaze maji ya baharini, ndege na wazidi katika nchi. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tano. Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo. Mungu akafanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake, na mnyama wa kufugwa kwa jinsi zake, na kila kitu kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo. Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.
Mwanzo 1:1-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo mwanzo, Mungu aliumba mbingu na dunia. Dunia ilikuwa bila umbo na tupu. Giza lilikuwa limefunika vilindi vya maji na roho ya Mungu ilikuwa ikitanda juu ya maji. Mungu akasema, “Mwanga uwe.” Mwanga ukawa. Mungu akauona mwanga kuwa ni mwema. Kisha Mungu akautenganisha mwanga na giza, mwanga akauita “Mchana” na giza akaliita “Usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya kwanza. Mungu akasema, “Anga liwe katikati ya maji, liyatenge maji sehemu mbili.” Mungu akalifanya anga, akayatenga maji yaliyo juu ya anga na yale yaliyo chini ya anga hilo. Ikawa hivyo. Mungu akaliita anga “Mbingu.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya pili. Mungu akasema, “Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, nchi kavu itokee.” Ikawa hivyo. Mungu akapaita mahali pakavu “Nchi” na kusanyiko la maji akaliita “Bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema. Kisha Mungu akasema, “Nchi na ioteshe mimea. Mimea izaayo mbegu, na miti izaayo matunda yenye mbegu.” Ikawa hivyo. Basi, nchi ikaotesha mimea izaayo mbegu kwa jinsi yake, na miti izaayo matunda yenye mbegu kwa jinsi yake. Mungu akaona kuwa ni vyema. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tatu. Mungu akasema, “Mianga na iweko angani, itenge mchana na usiku, ioneshe nyakati, majira, siku na miaka, na ingae angani na kuiangazia dunia.” Ikawa hivyo. Basi, Mungu akafanya mianga miwili mikubwa; ule mkubwa utawale mchana na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. Mungu akaiweka mianga hiyo angani iiangazie dunia, ipate kutawala mchana na usiku, na kuutenga mwanga na giza. Mungu akaona kuwa ni vyema. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya nne. Mungu akasema, “Maji na yatoe makundi ya viumbe hai na ndege waruke angani.” Basi, Mungu akaumba wanyama wakubwa sana wa baharini na aina zote za viumbe vyote hai viendavyo na kujaa majini; akaumba na aina zote za ndege wote. Mungu akaona kuwa ni vyema. Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni, muongezeke, muyajaze maji ya bahari; nao ndege waongezeke katika nchi.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tano. Mungu akasema, “Nchi na itoe aina zote za viumbe hai, wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo na wanyama wa porini wa kila aina.” Ikawa hivyo. Basi, Mungu akafanya aina zote za wanyama wa porini, wanyama wa kufugwa, na viumbe vitambaavyo. Mungu akaona kuwa ni vyema. Kisha Mungu akasema, “Tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; atawale samaki wa baharini, ndege wa angani, wanyama wa kufugwa, dunia yote na viumbe vyote vitambaavyo.” Basi, Mungu akaumba mtu kwa mfano wake; naam, kwa mfano wake Mungu alimuumba. Aliwaumba mwanamume na mwanamke. Mungu akawabariki na kuwaambia, “Zaeni muongezeke, mkaijaze nchi na kuimiliki; muwatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kitembeacho duniani.” Kisha Mungu akasema, “Tazama, nawapeni kila mmea duniani uzaao mbegu, na kila mti uzaao matunda yenye mbegu; mbegu zao au matunda yao yatakuwa chakula chenu. Nao wanyama wote duniani, ndege wote wa angani, viumbe vyote vitambaavyo, naam, kila kiumbe chenye uhai, chakula chao kitakuwa majani yote ya mimea.” Ikawa hivyo. Mungu akaona kila kitu alichokifanya kuwa ni chema kabisa. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya sita.
Mwanzo 1:1-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa tupu, tena bila umbo, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza. Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya kwanza. Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji. Mungu akaliumba anga, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo. Mungu akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili. Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo. Mungu akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mimea itoayo mbegu, na miti ya matunda izaayo matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo. Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu. Mungu akasema, Na iwe mianga katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili ya kuonesha majira, siku na miaka; tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi; ikawa hivyo. Mungu akaumba mianga miwili mikubwa, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi na kuutawala mchana na usiku na kutenga nuru na giza; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya nne. Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na viumbe vyenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu. Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao, na kila ndege arukaye, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akavibarikia, akisema, Zaeni, mkaongezeke, mkayajaze maji ya baharini, ndege na wazidi katika nchi. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tano. Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo. Mungu akaumba aina zote za wanyama wa porini na wa kufugwa na viumbe vyote vitambaavyo nchini; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila kiumbe kitambaacho nchini. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuimiliki; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mmea utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa chakula chenu; na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo. Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.
Mwanzo 1:1-31 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji. Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo. Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza. Mungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza. Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji igawe maji na maji.” Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi, akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo. Mungu akaiita hiyo nafasi “anga.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili. Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja, pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo. Mungu akaiita nchi kavu “ardhi,” nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema. Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo. Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake, na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tatu. Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe usiku na mchana, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka, nayo iwe mianga kwenye nafasi ya anga ya kutia nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo. Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota. Mungu akaiweka katika nafasi ya anga iangaze dunia, itawale usiku na mchana, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne. Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, nao ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.” Kwa hiyo Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni mwongezeke, mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano. Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo ardhini na wanyama pori, kila mnyama kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo. Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, wanyama wa kufugwa kulingana na aina zake, na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.” Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe, kwa mfano wa Mungu alimuumba; mwanaume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.” Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu. Nao wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo. Mungu akaona vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.