Mwanzo 19:12-29
Mwanzo 19:12-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi wale watu wakamwambia Lutu, Je! Unaye mtu hapa zaidi? Mkwe, wanao, na binti zako, na wo wote ulio nao katika mji, uwatoe katika mahali hapa; maana tutapaharibu sisi mahali hapa, kwa kuwa kilio chake kimezidi mbele za BWANA; naye BWANA ametupeleka tupaharibu. Lutu akatoka akasema na wakweze, waliowaposa binti zake, akasema, Ondokeni mtoke katika mahali hapa kwa sababu BWANA atauharibu mji huu. Lakini akawa kama achezaye machoni pa wakweze. Hata alfajiri ndipo malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, usipotee katika maovu ya mji huu. Akakawia-kawia; nao wale watu wakamshika mkono, na mkono wa mkewe, na mkono wa binti zake wawili, kwa jinsi BWANA alivyomhurumia, wakamtoa wakamweka nje ya mji. Ikawa walipomtoa nje, mmoja alisema, Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea. Lutu akawaambia, Sivyo, bwana wangu! Tazama, mtumwa wako ameona kibali machoni pako, nawe umezidisha rehema zako ulizonifanyia kwa kuponya nafsi yangu, nami siwezi kukimbilia mlimani nisipatwe na yale mabaya, nikafa. Basi mji huu u karibu, niukimbilie, nao ni mdogo, nijiponye sasa huko, sio mdogo huu? Na nafsi yangu itaishi. Akamwambia, Tazama, nimekukubali hata kwa neno hili, kwamba sitauangamiza mji huo uliounena. Hima, ujiponye huko, maana siwezi kufanya neno lo lote, hata uingiapo humo. Kwa hiyo jina la mji ule likaitwa Soari. Jua lilikuwa limechomoza juu ya nchi Lutu alipoingia Soari. Ndipo BWANA akanyesha juu ya Sodoma na juu ya Gomora kiberiti na moto toka mbinguni kwa BWANA. Akaangusha miji hiyo na Bonde lote, na wote waliokaa katika miji hiyo, na yote yaliyomea katika nchi ile. Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi. Ibrahimu akatoka asubuhi kwenda mahali aliposimama mbele za BWANA, naye akatazama upande wa Sodoma na Gomora na nchi yote ya hilo Bonde, akaona, na tazama, moshi wa nchi ukapanda, kama moshi wa tanuru. Ikawa Mungu alipoiharibu miji ya Bondeni, Mungu akamkumbuka Ibrahimu, akamtoa Lutu katika maangamizi alipoiangamiza miji hiyo aliyokaa Lutu.
Mwanzo 19:12-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Wale watu wawili wakamwambia Loti, “Je, una mtu mwingine hapa, pengine wana, mabinti, wachumba wa binti zako au watu wengine wa jamaa yako wanaoishi mjini humu? Watoe mahali hapa haraka, kwa maana kilio kilichomfikia Mwenyezi-Mungu dhidi ya wakazi wa hapa ni kikubwa mno, naye ametutuma tuje kuwaangamiza.” Basi, Loti akawaendea wachumba wa binti zake, akawaambia, “Haraka! Tokeni mahali hapa, maana Mwenyezi-Mungu atauangamiza mji huu.” Lakini wao wakamwona kama mtu mcheshi tu. Kulipokucha, malaika wakamhimiza Loti wakisema, “Amka, mchukue mkeo na hawa binti zako wawili msije mkaangamia wakati mji huu unapoadhibiwa.” Loti akawa anasitasita. Lakini kwa vile Mwenyezi-Mungu alivyomhurumia Loti, wale malaika wakamshika yeye, mkewe na binti zake wawili, wakamtoa nje ya mji. Walipowatoa nje ya mji, malaika mmoja wao akawaambia, “Kimbieni kwa usalama wenu. Msiangalie nyuma wala kusimama popote bondeni. Kimbilieni milimani, msije mkaangamia.” Loti akawaambia, “La, bwana zangu! Ni kweli kwamba mimi mtumishi wenu nimepata fadhili mbele yenu, nanyi mmenionea huruma sana kwa kuyaokoa maisha yangu; lakini milimani ni mbali mno. Maangamizi haya yatanikuta kabla sijafika huko, nami nitakufa. Tazameni, kule kuna mji mdogo ambao naweza kuukimbilia kwani uko karibu. Basi, mniruhusu nikimbilie huko. Ule ni mji mdogo tu, na huko nitasalimika.” Naye akamjibu, “Sawa, nimekubali ombi lako. Sitauangamiza mji ulioutaja. Harakisha! Kimbilia huko, nami sitafanya lolote mpaka utakapowasili huko.” Hivyo mji huo ukaitwa Soari. Jua lilikuwa limekwisha chomoza wakati Loti alipowasili mjini Soari. Ndipo Mwenyezi-Mungu akateremsha moto mkali wa kiberiti kutoka mbinguni juu ya Sodoma na Gomora, akaiangamiza miji hiyo, bonde lote, wakazi wake wote na mimea yote katika nchi hiyo. Lakini mkewe Loti aliyekuwa nyuma ya Loti, akatazama nyuma, akageuka nguzo ya chumvi. Asubuhi na mapema, Abrahamu alikwenda mahali alipokuwa amesimama mbele ya Mwenyezi-Mungu. Akiwa hapo, akatazama chini pande za Sodoma na Gomora na eneo lote la bondeni, akashangaa kuona moshi ukipanda, moshi kama wa tanuri kubwa. Mungu alipoiangamiza miji ya bondeni alimokuwa anakaa Loti, alimkumbuka Abrahamu kwa kumtoa Loti katika miji hiyo, ili Loti asije akaangamia pamoja nayo.
Mwanzo 19:12-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi wale watu wakamwambia Lutu, Je! Unaye mtu hapa zaidi? Wakwe, wanao wa kiume au wa kike, na wowote ulio nao katika mji uwatoe katika mahali hapa; maana tutapaharibu mahali hapa, kwa kuwa kilio chake kimezidi mbele za BWANA; naye BWANA ametutuma tupaharibu. Lutu akatoka na kusema na wachumba wa binti zake, akawaambia, “Ondokeni mahali hapa kwa sababu BWANA atauharibu mji huu”. Lakini akaonekana kama achezaye machoni pa wakwe zake. Hata alfajiri ndipo malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, la sivyo utapotelea katika maangamizi ya mji huu. Akakawiakawia; nao wale watu wakamshika mkono, na mkono wa mkewe, na mkono wa binti zake wawili, kwa jinsi BWANA alivyomhurumia, wakamtoa wakamweka nje ya mji. Ikawa walipomtoa nje, mmoja alisema, Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala usisimame katika hilo bonde popote; ujiponye mlimani, usije ukaangamia. Lutu akawaambia, Sivyo, bwana wangu! Tazama, mtumwa wako ameona kibali machoni pako, nawe umezidisha rehema zako ulizonifanyia kwa kuponya nafsi yangu, nami siwezi kukimbilia mlimani nisipatwe na yale mabaya, nikafa. Basi mji huu u karibu, niukimbilie, nao ni mdogo, nijiponye sasa huko, sio mdogo huu? Na nafsi yangu itaishi. Akamwambia, Tazama, nimekukubali hata kwa neno hili, kwamba sitauangamiza mji huo uliounena. Hima, ujiponye huko, maana siwezi kufanya neno lolote, hadi uingiapo humo. Kwa hiyo jina la mji ule likaitwa Soari. Jua lilikuwa limechomoza juu ya nchi Lutu alipoingia Soari. Ndipo BWANA akanyesha juu ya Sodoma na juu ya Gomora kiberiti na moto kutoka mbinguni kwa BWANA. Akaangusha miji hiyo na Bonde lote, na wote waliokaa katika miji hiyo, na yote yaliyomea katika nchi ile. Lakini mkewe Lutu, akiwa nyuma ya mumewe, aliangalia nyuma akawa nguzo ya chumvi. Abrahamu akatoka asubuhi kwenda mahali aliposimama mbele za BWANA, naye akatazama upande wa Sodoma na Gomora na nchi yote ya hilo Bonde, akaona, na tazama, moshi wa nchi ukapanda, kama moshi wa tanuri. Ikawa Mungu alipoiharibu miji ya Bondeni, Mungu akamkumbuka Abrahamu, akamtoa Lutu katika maangamizi alipoiangamiza miji hiyo aliyokaa Lutu.
Mwanzo 19:12-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wale watu wawili wakamwambia Loti, “Una mtu mwingine yeyote hapa, wakwe zako, wana au binti, ama yeyote mwingine aliye wako katika mji huu? Waondoe hapa, kwa sababu tunapaangamiza mahali hapa. Kilio kwa BWANA dhidi ya watu wa hapa ni kikubwa kiasi kwamba ametutuma kupaangamiza.” Kwa hiyo Loti alitoka ili kuzungumza na wakwe zake, waliokuwa wamewaposa binti zake. Akawaambia, “Fanyeni haraka kuondoka mahali hapa, kwa kuwa BWANA yu karibu kuangamiza mji huu!” Lakini wakwe zake walifikiri kwamba alikuwa akitania. Kunako mapambazuko, malaika wakamhimiza Loti, wakamwambia, “Fanya haraka! Mchukue mke wako na binti zako wawili walioko hapa, la sivyo utaangamizwa wakati mji utakapoadhibiwa.” Alipositasita, wale watu wakamshika mkono wake na mikono ya mke wake na binti zake wawili na kuwaongoza salama nje ya mji, kwa kuwa BWANA alikuwa na huruma kwao. Mara walipokwisha kuwatoa nje, mmoja wao akawaambia, “Mkimbie kwa usalama wenu! Msitazame nyuma, wala msisimame popote katika nchi tambarare! Kimbilieni milimani, ama sivyo mtaangamizwa!” Lakini Loti akawajibu, “La hasha, bwana zangu, tafadhalini! Mtumishi wenu amepata kibali mbele ya macho yenu, nanyi mmeonyesha wema mkubwa kwangu kwa kuokoa maisha yangu. Lakini siwezi kukimbilia milimani, janga hili litanikumba, nami nitakufa. Tazama, hapa kuna mji karibu wa kukimbilia, nao ni mdogo. Niruhusuni nikimbilie humo, ni mdogo sana, ama sivyo? Ndipo maisha yangu yatasalimika.” Akamwambia, “Vema sana, nitalikubali hili ombi pia, sitauangamiza mji ulioutaja. Lakini ukimbilie huko haraka, kwa sababu sitaweza kufanya lolote mpaka ufike huko.” (Ndiyo maana mji huo ukaitwa Soari.) Wakati Loti alipofika Soari, jua lilikuwa limechomoza katika nchi. Ndipo BWANA akanyesha moto wa kiberiti uliotoka mbinguni kwa BWANA juu ya Sodoma na Gomora. Hivyo akaiteketeza miji ile na eneo lote la tambarare, pamoja na wote waliokuwa wanaishi katika miji, hata pia mimea yote katika nchi. Lakini mke wa Loti akatazama nyuma, hivyo akawa nguzo ya chumvi. Asubuhi na mapema siku iliyofuata, Abrahamu akaamka na kurudi mahali pale aliposimama mbele za BWANA. Akatazama upande wa Sodoma na Gomora, kuelekea nchi yote ya tambarare, akaona moshi mzito ukipanda kutoka kwenye nchi, kama moshi utokao kwenye tanuru. Kwa hiyo Mungu alipoiangamiza miji ya tambarare alimkumbuka Abrahamu, akamtoa Loti kutoka kwenye lile janga lililoharibu miji ile ambamo Loti alikuwa ameishi.