Mwanzo 4:8-24
Mwanzo 4:8-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Baadaye, Kaini akamwambia Abeli nduguye, “Twende nje shambani” Basi, walipokuwa shambani, Kaini akamvamia Abeli nduguye, akamuua. Mwenyezi-Mungu akamwuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?” Kaini akamjibu, “Mimi sijui! Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” Mwenyezi-Mungu akasema, “Umefanya nini? Damu ya ndugu yako yanililia kutoka udongoni. Sasa wewe umelaaniwa! Hutailima tena ardhi yenye rutuba ambayo kama kinywa imeipokea damu ya nduguyo uliyemuua. Ukiilima ardhi haitakupatia tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani.” Kaini akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Adhabu yangu ni kubwa mno; siwezi kuistahimili. Leo umenifukuza kutoka ardhi yenye rutuba na mbali nawe. Basi, nitakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani, na yeyote atakayeniona ataniua.” Lakini Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Sivyo! Atakayekuua wewe Kaini atalipizwa mara saba.” Basi, Mwenyezi-Mungu akamtia Kaini alama ya tahadhari, ili yeyote atakayemwona asimuue. Kisha Kaini akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawa anaishi katika nchi ya Nodi, upande wa mashariki wa Edeni. Kaini akalala na mkewe, naye akapata mimba, akamzaa Henoki. Kaini akajenga mji akauita kwa jina la Henoki mwanawe. Henoki akamzaa Iradi, naye Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli, naye Methushaeli akamzaa Lameki. Lameki alioa wanawake wawili, mmoja aliitwa Ada na mwingine Sila. Ada alimzaa Yabali ambaye alikuwa baba yao wafugaji waishio mahemani. Ndugu yake alikuwa Yubali; huyo alikuwa baba yao wanamuziki wote wapigao zeze na filimbi. Sila naye alimzaa Tubal-kaini, ambaye alikuwa mhunzi wa vyombo vyote vya shaba na chuma. Dada yake Tubal-kaini alikuwa Naama. Lameki akawaambia wake zake, “Ada na Sila sikieni sauti yangu! Sikilizeni nisemayo enyi wake za Lameki. Mimi niliua mtu kwa kunijeruhi, naam, nilimuua kijana kwa kuniumiza. Ikiwa Kaini atalipizwa mara saba, kweli Lameki atalipizwa mara sabini na saba.”
Mwanzo 4:8-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]. Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua. BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, kwani mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kutoka kwa mkono wako; utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na makao duniani. Kaini akamwambia BWANA, Adhabu yangu imeniwia kubwa, haichukuliki. Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na makao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua. BWANA akamwambia, Kwa sababu hiyo yeyote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. BWANA akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga. Kaini akatoka mbele za uso wa BWANA, akakaa katika nchi ya Nodi, Mashariki mwa Edeni. Kaini akamjua mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Henoko; akajenga mji akauita Henoko, kwa jina la mwanawe. Henoko akamzaa Iradi, Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli; Methushaeli akamzaa Lameki. Lameki akajitwalia wake wawili, jina la wa kwanza ni Ada, na jina la wa pili ni Sila. Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama. Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba ya wote wapigao kinubi na filimbi. Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na dada yake Tubal-kaini alikuwa Naama. Lameki akawaambia wake zake, Sikieni sauti yangu, Ada na Sila; Enyi wake za Lameki, sikilizeni ninachosema; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua; Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba, Hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba.
Mwanzo 4:8-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]. Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua. BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako; utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani. Kaini akamwambia BWANA, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki. Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua. BWANA akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. BWANA akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga. Kaini akatoka mbele za uso wa BWANA, akakaa katika nchi ya Nodi, mbele ya Edeni. Kaini akamjua mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Henoko; akajenga mji akauita Henoko, kwa jina la mwanawe. Henoko akamzaa Iradi, Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli; Methushaeli akamzaa Lameki. Lameki akajitwalia wake wawili, jina la wa kwanza ni Ada, na jina la wa pili ni Sila. Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama. Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi. Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake Tubal-kaini alikuwa Naama. Lameki akawaambia wake zake, Sikieni sauti yangu, Ada na Sila; Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua; Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba, Hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba.
Mwanzo 4:8-24 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Basi Kaini akamwambia ndugu yake Habili, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Habili ndugu yake, akamuua. Kisha Mwenyezi Mungu akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Habili yuko wapi?” Akamjibu, “Sijui. Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” Mwenyezi Mungu akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini. Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako. Utakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu.” Kaini akamwambia Mwenyezi Mungu, “Adhabu yangu ni zaidi ya ninavyoweza kustahimili. Leo unanifukuza kutoka nchi, nami nitafichwa mbali na uwepo wako. Nitakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu, na yeyote anionaye ataniua.” Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia, “La, sivyo! Ikiwa mtu yeyote atamuua Kaini, atalipizwa kisasi mara saba.” Kisha Mwenyezi Mungu akamwekea Kaini alama ili yeyote angemwona asimuue. Kwa hiyo Kaini akaondoka mbele za Mwenyezi Mungu, akaenda kuishi katika nchi ya Nodi, mashariki mwa Edeni. Kaini akakutana kimwili na mkewe, naye akapata mimba na akamzaa Idrisi. Wakati huo Kaini alikuwa anajenga mji, akauita Idrisi, jina la mtoto wake. Idrisi akamzaa Iradi; Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli; naye Methushaeli akamzaa Lameki. Lameki alioa wanawake wawili: mmoja aliitwa Ada, na mwingine Sila. Ada akamzaa Yabali; huyu akawa baba wa wale wanaoishi katika mahema na kufuga wanyama. Kaka yake aliitwa Yubali, aliyekuwa baba wa wote wapigao zeze na filimbi. Pia Sila alikuwa na mtoto wa kiume aliyeitwa Tubali-Kaini, ambaye alifua vifaa vya aina mbalimbali vya shaba na chuma. Naama alikuwa dada wa Tubali-Kaini. Lameki akawaambia wake zake, “Ada na Sila, nisikilizeni mimi; wake wa Lameki sikieni maneno yangu. Nimemuua mtu kwa kunijeruhi, kijana mdogo kwa kuniumiza. Kama Kaini atalipizwa kisasi mara saba, basi Lameki itakuwa mara sabini na saba.”