Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 7:1-16

Mwanzo 7:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu akamwambia Noa, “Ingia ndani ya safina wewe pamoja na jamaa yako yote, kwa maana, kati ya watu wote wanaoishi nyakati hizi zako, nimekuona wewe peke yako kuwa mwadilifu mbele yangu. Chukua pamoja nawe wanyama wote walio safi, dume na jike, saba saba; lakini wanyama walio najisi, chukua dume na jike, wawiliwawili. Vilevile chukua ndege wa angani dume na jike, saba saba, ili kuzihifadhi hai aina zao duniani. Baada ya siku saba, nitanyesha mvua nchini siku arubaini mchana na usiku, na kila kiumbe hai nilichokiumba duniani nitakiangamiza.” Noa akafanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru. Noa alikuwa na umri wa miaka 600 wakati gharika ilipotokea nchini. Noa, mkewe, wanawe na wake zao wakaingia ndani ya safina ili kuiepa gharika. Wanyama walio safi, wanyama walio najisi, ndege na viumbe vyote vitambaavyo, wawiliwawili, dume na jike, wakaingia ndani ya safina pamoja na Noa kama Mungu alivyomwamuru. Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaanza kuifunika nchi. Noa alipokuwa na umri wa miaka 600, mnamo siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili, siku hiyo chemchemi zote za vilindi vya nchi zikabubujika maji, na madirisha ya mbinguni yakafunguka. Mvua ikanyesha nchini siku arubaini mchana na usiku. Siku hiyohiyo mvua ilipoanza kunyesha, Noa, mkewe na wanawe, Shemu, Hamu na Yafethi, pamoja na wake zao, waliingia ndani ya safina. Waliingia wao wenyewe pamoja na aina zote za wanyama wa porini, wanyama wafugwao, wanyama watambaao na ndege wa kila aina. Waliingia ndani ya safina pamoja na Noa wiliwawili wa kila aina ya viumbe hai. Kila aina yao waliingia, dume na jike, kama Mungu alivyomwamuru Noa. Kisha, Mwenyezi-Mungu akaufunga mlango wa safina nyuma yake Noa.

Shirikisha
Soma Mwanzo 7

Mwanzo 7:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki. Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, wa kiume na wa kike; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, wa kiume na wa kike. Tena katika ndege wa angani saba saba, wa kike na wa kiume; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote. Kwa maana baada ya siku saba nitainyeshea dunia mvua, siku arubaini mchana na usiku; na kila kilicho hai nilichokifanya juu ya uso wa nchi nitakifutilia mbali. Nuhu akafanya kama vile BWANA alivyomwamuru. Naye Nuhu alikuwa mtu wa miaka mia sita hapo hiyo gharika ya maji ilipokuwa juu ya nchi. Nuhu akaingia katika safina, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kwa sababu ya maji ya gharika. Na katika wanyama walio safi, na wanyama wasio safi, na ndege, navyo vyote vitambaavyo juu ya nchi, wakaingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, wa kike na wa kiume, kama vile Mungu alivyomwamuru Nuhu. Ikawa baada ya siku hizo saba, maji ya gharika yakawa juu ya nchi. Katika mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu, mwezi wa pili, siku ya kumi na saba ya mwezi, siku ile chemchemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu, madirisha ya mbinguni yakafunguka. Mvua ikanyesha juu ya nchi, siku arubaini mchana na usiku. Siku ile ile Nuhu akaingia katika safina, yeye, na Shemu na Hamu na Yafethi, wana wa Nuhu, na mkewe Nuhu, na wake watatu wa wanawe pamoja naye; wao na kila mnyama wa mwitu kwa jinsi yake, na kila mnyama wa kufugwa kwa jinsi yake, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi, kwa jinsi yake, na kirukacho kwa jinsi yake, kila ndege wa namna yoyote. Waliingia katika safina alimokuwa Nuhu, wawili wawili, wa kila chenye mwili kilicho na pumzi ya uhai ndani yake. Na walioingia, waliingia wa kike na wa kiume, wa kila kitu chenye mwili, kama vile alivyomwamuru Mungu; BWANA akamfungia.

Shirikisha
Soma Mwanzo 7

Mwanzo 7:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki. Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke. Tena katika ndege wa angani saba saba, mume na mke; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote. Kwa maana baada ya siku saba nitainyeshea dunia mvua, siku arobaini mchana na usiku; na kila kilicho hai nilichokifanya juu ya uso wa nchi nitakifutilia mbali. Nuhu akafanya kama vile BWANA alivyomwamuru. Naye Nuhu alikuwa mtu wa miaka mia sita hapo hiyo gharika ya maji ilipokuwa juu ya nchi. Nuhu akaingia katika safina, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kwa sababu ya maji ya gharika. Na katika wanyama walio safi, na wanyama wasio safi, na ndege, navyo vyote vitambaavyo juu ya nchi, wakaingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, mume na mke, kama vile Mungu alivyomwamuru Nuhu. Ikawa baada ya siku hizo saba, maji ya gharika yakawa juu ya nchi. Katika mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu, mwezi wa pili, siku ya kumi na saba ya mwezi, siku ile chemchemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu, madirisha ya mbinguni yakafunguka. Mvua ikanyesha juu ya nchi, siku arobaini mchana na usiku. Siku ile ile Nuhu akaingia katika safina, yeye, na Shemu na Hamu na Yafethi, wana wa Nuhu, na mkewe Nuhu, na wake watatu wa wanawe pamoja naye; wao na kila mnyama wa mwitu kwa jinsi yake, na kila mnyama wa kufugwa kwa jinsi yake, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi, kwa jinsi yake, na kirukacho kwa jinsi yake, kila ndege wa namna yo yote. Waliingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, wa kila chenye mwili kilicho na pumzi ya uhai ndani yake. Na walioingia, waliingia mume na mke, wa kila kitu chenye mwili, kama vile alivyomwamuru Mungu; BWANA akamfungia.

Shirikisha
Soma Mwanzo 7

Mwanzo 7:1-16 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Nuhu, “Ingia katika safina, wewe na jamaa yako yote, kwa sababu katika kizazi hiki nimeona ya kuwa wewe ni mwenye haki. Chukua wanyama saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike; na wanyama wawili wawili wa kila aina walio najisi, wa kiume na wa kike. Pia uchukue ndege saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike, ili kuhifadhi aina zao mbalimbali katika dunia yote. Siku saba kuanzia sasa nitaleta mvua juu ya dunia kwa siku arobaini, usiku na mchana; nami nitafutilia mbali kutoka uso wa dunia kila kiumbe hai nilichokiumba.” Nuhu akafanya yote Mwenyezi Mungu aliyomwamuru. Nuhu alikuwa na umri wa miaka mia sita gharika ilipokuja juu ya dunia. Nuhu na mkewe, na wanawe na wake zao, wakaingia katika safina ili waepuke ile gharika. Jozi ya wanyama walio safi na walio najisi, ndege na viumbe vinavyotambaa ardhini, wa kiume na wa kike, walikuja kwa Nuhu, wakaingia katika safina kama Mungu alivyomwamuru Nuhu. Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaja juu ya dunia. Katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili, mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu, siku hiyo chemchemi zote za vilindi zilibubujika kwa nguvu, na malango ya mafuriko ya mbinguni yakafunguliwa. Mvua ikanyesha juu ya dunia siku arobaini usiku na mchana. Siku hiyo Nuhu na mkewe, na wanawe Shemu, Hamu na Yafethi pamoja na wake zao, wakaingia katika ile safina. Nao walikuwa pamoja na kila mnyama pori kufuatana na aina yake, wanyama wote wafugwao kufuatana na aina zao, kila kiumbe kinachotambaa juu ya ardhi kwa aina yake, na kila ndege kufuatana na aina yake, naam kila kiumbe chenye mabawa. Viumbe vyote vyenye pumzi ya uhai vikaja kwa Nuhu viwili viwili, vikaingia katika safina. Wanyama walioingia katika safina walikuwa wa kiume na wa kike, wa kila kiumbe chenye uhai kama Mungu alivyomwamuru Nuhu; ndipo Mwenyezi Mungu akamfungia ndani.

Shirikisha
Soma Mwanzo 7