Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 8:1-22

Mwanzo 8:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na Mungu akamkumbuka Nuhu, na kila kilicho hai, na wanyama wote waliokuwamo pamoja naye katika safina; Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakapungua; chemchemi za vilindi zikafungwa, pia na madirisha ya mbinguni, mvua kutoka mbinguni ikazuiliwa; maji yakadumu kuondoka katika nchi; na mwisho wa siku mia na hamsini maji yakapunguka. Mwezi wa saba, siku ya kumi na saba ya mwezi, safina ikatua juu ya milima ya Ararati. Maji yakapunguka-punguka hata mwezi wa kumi; mwezi huo wa kumi, siku ya kwanza ya mwezi, vilele vya milima vikaonekana. Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya; akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi. Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi; bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani. Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili, njiwa akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelitunda, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi. Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe. Ikawa mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikauka juu ya nchi. Nuhu akaondoa kifuniko cha safina, naye akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka. Na mwezi wa pili, siku ya ishirini na saba ya mwezi, nchi ilikuwa kavu. Mungu akamwambia Nuhu, akisema, Toka katika safina, wewe, na mkeo, na wanao, na wake za wanao pamoja nawe. Utoe pamoja nawe kila kilicho hai kilichomo pamoja nawe, chenye mwili, ndege, na mnyama, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi; wajae katika nchi, wawe na uzazi, wakaongezeke katika nchi. Basi Nuhu akatoka, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kila mnyama, na kila kitambaacho, na kila ndege, kila kinachokwenda juu ya nchi kwa kabila zao, wakatoka katika safina. Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. BWANA akasikia harufu ya kumridhisha; BWANA akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya. Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma.

Shirikisha
Soma Mwanzo 8

Mwanzo 8:1-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mungu akamkumbuka Noa na wanyama wote wa porini na wa kufugwa waliokuwa naye ndani ya safina, akatuma upepo ukavuma katika dunia, nayo maji yakaondoka. Zile chemchemi zilizo chini sana ya ardhi pamoja na malango ya mafuriko ya mbinguni yakawa yamefungwa nayo mvua ikawa imekoma kunyesha kutoka angani. Maji yakaendelea kupungua taratibu katika nchi. Kunako mwisho wa siku ya 150, maji yalikuwa yamepungua, katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua katika milima ya Ararati. Maji yakaendelea kupungua hadi mwezi wa kumi, na siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, vilele vya milima vikaonekana. Baada ya siku arobaini Noa akafungua dirisha alilokuwa amelifanya katika safina na akamtoa kunguru, akawa akiruka kwenda na kurudi mpaka maji yalipokwisha kukauka juu ya nchi. Kisha akamtoa hua ili aone kama maji yameondoka juu ya uso wa ardhi. Lakini hua hakupata mahali pa kutua kwa kuwa maji yalienea juu ya uso wa dunia yote, kwa hiyo akarudi kwa Noa ndani ya safina. Noa akanyoosha mkono akamchukua yule hua akamrudisha ndani ya safina. Noa akangojea siku saba zaidi kisha akamtoa tena hua kutoka safina. Wakati hua aliporejea kwa Noa jioni, alikuwa amechukua katika mdomo wake jani bichi la mzeituni, lililochumwa wakati ule ule! Ndipo Noa akajua ya kuwa maji yameondoka juu ya uso wa dunia. Akangojea siku saba zaidi na akamtuma tena hua, lakini wakati huu hua hakurudi tena kwa Noa. Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza ya mwaka 601, wa kuishi kwake Noa, maji yalikuwa yamekauka duniani. Kisha Noa akafungua mlango wa safina akaona ya kuwa uso wa ardhi ulikuwa umekauka. Katika siku ya ishirini na saba ya mwezi wa pili dunia ilikuwa imekauka kabisa. Ndipo Mungu akamwambia Noa, “Toka ndani ya safina, wewe na mkeo na wanao na wake zao. Utoe nje kila aina ya kiumbe hai aliye pamoja nawe: Ndege, wanyama na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi, ili wakazae, na kuongezeka na kuijaza tena dunia.” Kwa hiyo Noa akatoka nje pamoja na mkewe, wanawe na wake zao. Wanyama wote na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi na ndege wote, kila kitu kiendacho juu ya nchi, aina moja baada ya nyingine vikatoka katika safina, kila aina ya kiumbe, kimoja baada ya kingine. Kisha Noa akamjengea BWANA madhabahu, akachukua baadhi ya wale wanyama na ndege wote walio safi, akatoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. BWANA akasikia harufu nzuri ya kupendeza, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena ardhi kwa sababu ya mwanadamu, hata ingawa kila mwelekeo wa moyo wake ni mbaya tangu ujana. Kamwe sitaangamiza tena viumbe hai vyote kama nilivyofanya. “Kwa muda dunia idumupo, wakati wa kupanda na wa kuvuna, wakati wa baridi na wa joto, wakati wa kiangazi na wa masika, usiku na mchana kamwe havitakoma.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 8

Mwanzo 8:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha Mungu akamkumbuka Noa na wanyama wote wa porini na wa kufugwa waliokuwa pamoja naye ndani ya safina. Basi, Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakaanza kupungua. Chemchemi za maji ya vilindi na madirisha ya mbinguni yakafungwa. Mvua ikazuiwa, maji yakaendelea kupungua polepole katika nchi. Baada ya siku 150, maji yakawa yamepungua sana. Mnamo siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua juu ya milima ya Ararati. Maji yakaendelea kupungua polepole, na siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, vilele vya milima vikaonekana. Baada ya siku arubaini, Noa alifungua dirisha alilokuwa ametengeneza katika hiyo safina, akamtoa kunguru nje, naye hakurudi bali aliruka huko na huko mpaka maji yalipokauka nchini. Kisha Noa akamtoa njiwa apate kuona kama maji yalikuwa yamepungua juu ya nchi. Lakini, kwa vile maji yalikuwa bado yameifunika nchi yote, huyo njiwa hakupata mahali pa kutua, akamrudia Noa katika safina. Noa akanyosha mkono, akamtwaa na kumrudisha ndani ya safina. Noa akangoja siku nyingine saba, kisha akamtoa tena huyo njiwa. Njiwa huyo akamrudia Noa saa za jioni akiwa na tawi bichi la mzeituni mdomoni mwake. Kwa hiyo Noa akajua kwamba maji yalikuwa yamepungua katika nchi. Kisha akangoja siku nyingine saba, akamtoa tena yule njiwa; safari hii njiwa hakurudi kabisa. Noa alipokuwa na umri wa miaka 601, siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, maji yalikuwa yamekauka katika nchi. Noa akafunua kifuniko cha safina na alipotazama, akaona kwamba nchi ilikuwa imekauka. Siku ya 27 ya mwezi wa pili, nchi ilikuwa imekauka kabisa. Hapo, Mungu akamwambia Noa, “Toka katika safina, wewe pamoja na mkeo, wanao na wake zao. Toa pia viumbe wote hai wa kila aina waliokuwa pamoja nawe, ndege na wanyama na kila kiumbe kitambaacho, wapate kuzaa kwa wingi duniani, waongezeke na kuenea kila mahali duniani.” Basi, Noa akatoka katika safina pamoja na wanawe na mkewe pamoja na wake za wanawe. Wakatoka kufuatana na jamii zao, wanyama wote wa porini, viumbe wote watambaao, ndege wote na wanyama wote hai duniani. Noa akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu, akatwaa mmoja katika kila aina ya wanyama walio safi na ndege walio safi, akamtolea Mungu sadaka za kuteketezwa. Harufu nzuri ya tambiko hiyo ikampendeza Mwenyezi-Mungu, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena nchi kwa sababu ya binadamu; najua kwamba mawazo yake ni maovu tangu utoto wake. Wala sitaangamiza tena viumbe wote kama nilivyofanya. Kadiri itakavyodumu nchi majira ya kupanda na kuvuna, ya baridi na joto, ya masika na kiangazi, usiku na mchana, hayatakoma.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 8

Mwanzo 8:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na Mungu akamkumbuka Nuhu, na kila kilicho hai, na wanyama wote waliokuwamo pamoja naye katika safina; Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakapungua; chemchemi za vilindi zikafungwa, pia na madirisha ya mbinguni, mvua kutoka mbinguni ikazuiliwa; maji yakadumu kuondoka katika nchi; na mwisho wa siku mia moja na hamsini maji yakapunguka. Mwezi wa saba, siku ya kumi na saba ya mwezi, safina ikatua juu ya milima ya Ararati. Maji yakapungukapunguka hata mwezi wa kumi; mwezi huo wa kumi, siku ya kwanza ya mwezi, vilele vya milima vikaonekana. Ikawa baada ya siku arubaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya; akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huku na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi. Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi; bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani. Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili, njiwa akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelichuma, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi. Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe. Ikawa mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikauka juu ya nchi. Nuhu akaondoa kifuniko cha safina, naye akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka. Na mwezi wa pili, siku ya ishirini na saba ya mwezi, nchi ilikuwa kavu. Mungu akamwambia Nuhu, akisema, Toka katika safina, wewe, na mkeo, na wanao, na wake za wanao pamoja nawe. Utoe pamoja nawe kila kilicho hai kilichomo pamoja nawe, chenye mwili, ndege, na mnyama, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi; wajae katika nchi, wawe na uzazi, wakaongezeke katika nchi. Basi Nuhu akatoka, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kila mnyama, na kila kitambaacho, na kila ndege, kila kinachokwenda juu ya nchi kwa makabila yao, wakatoka katika safina. Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. BWANA akasikia harufu ya kumridhisha; BWANA akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya. 1 Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa joto, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma.

Shirikisha
Soma Mwanzo 8