Waebrania 3:3-13
Waebrania 3:3-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana huyo amehesabiwa kuwa amestahili utukufu zaidi kuliko Musa, kama vile yeye aitengenezaye nyumba alivyo na heshima zaidi ya hiyo nyumba. Maana kila nyumba imetengenezwa na mtu; ila yeye aliyevitengeneza vitu vyote ni Mungu. Na Musa kweli alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu kama mtumishi, awe ushuhuda wa mambo yatakayonenwa baadaye; bali Kristo, kama mwana, juu ya nyumba ya Mungu; ambaye nyumba yake ni sisi, kama tukishikamana sana na ujasiri wetu na fahari ya tumaini letu mpaka mwisho. Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mkisikia sauti yake, Msifanye mioyo yenu kuwa migumu, Kama wakati wa kuasi, Siku ya kujaribiwa katika jangwa, Hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima, Wakaona matendo yangu miaka arubaini. Kwa hiyo nilichukizwa na kizazi hiki, Nikasema, Sikuzote ni watu waliopotoka mioyo hawa; Hawakuzijua njia zangu; Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu. Hadharini, ndugu zangu, usiwepo katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutoamini, ujitengao na Mungu aliye hai. Lakini mwonyane kila siku, maadamu inaitwa leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.
Waebrania 3:3-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana huyo amehesabiwa kuwa amestahili utukufu zaidi kuliko Musa, kama vile yeye aitengenezaye nyumba alivyo na heshima zaidi ya hiyo nyumba. Maana kila nyumba imetengenezwa na mtu; ila yeye aliyevitengeneza vitu vyote ni Mungu. Na Musa kweli alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu kama mtumishi, awe ushuhuda wa mambo yatakayonenwa baadaye; bali Kristo, kama mwana, juu ya nyumba ya Mungu; ambaye nyumba yake ni sisi, kama tukishikamana sana na ujasiri wetu na fahari ya taraja letu mpaka mwisho. Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha, Siku ya kujaribiwa katika jangwa, Hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima, Wakaona matendo yangu miaka arobaini. Kwa hiyo nalichukizwa na kizazi hiki, Nikasema, Sikuzote ni watu waliopotoka mioyo hawa; Hawakuzijua njia zangu; Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu. Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai. Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.
Waebrania 3:3-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini Yesu anastahili heshima kubwa kuliko Mose maana mjenzi wa nyumba hupata heshima zaidi kuliko hiyo nyumba yenyewe. Kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini Mungu ndiye mjenzi wa vitu vyote. Mose alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Bwana kama mtumishi, na alinena juu ya mambo ambayo Mungu atayasema hapo baadaye. Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana mwenye mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. Sisi wenyewe ni nyumba yake kama tukiendelea kuwa hodari na thabiti katika kile tunachotumainia. Kwa hiyo, basi, kama asemavyo Roho Mtakatifu: “Kama mkisikia sauti yake leo, msiwe wakaidi kama wakati ule waliponiasi kama wakati ule wa majaribio kule jangwani. Huko wazee wenu walinijaribu na kunichunguza, ingawa walishuhudia matendo yangu kwa miaka arubaini! Kwa sababu hiyo niliwakasirikia watu hao nikasema, ‘Fikira za watu hawa zimepotoka, hawajapata kamwe kuzijua njia zangu’. Basi, nilikasirika, nikaapa: ‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko.’ Basi ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo na asiyeamini hata kujitenga na Mungu aliye hai. Maadamu hiyo “Leo” inayosemwa katika Maandiko bado inatuhusu sisi, mnapaswa kusaidiana daima, ili mtu yeyote miongoni mwenu asidanganywe na dhambi na kuwa mkaidi.
Waebrania 3:3-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu ameonekana anastahili heshima kubwa kuliko Mose, kama vile mjenzi wa nyumba alivyo wa heshima kubwa kuliko nyumba yenyewe. Kwa kuwa kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini Mungu ni mjenzi wa kila kitu. Basi Mose kama mtumishi alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu, akishuhudia kwa yale ambayo yangetamkwa baadaye. Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana katika nyumba ya Mungu. Sisi ndio nyumba yake, kama tutashikilia sana ujasiri wetu na tumaini tunalojivunia. Kwa hiyo, kama Roho Mtakatifu asemavyo: “Leo, kama mkiisikia sauti yake, msiifanye mioyo yenu migumu, kama mlivyofanya katika uasi, wakati ule wa kujaribiwa jangwani, ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima ingawa kwa miaka arobaini walikuwa wameyaona matendo yangu. Hiyo ndiyo sababu nilikasirikia kizazi kile, nami nikasema, ‘Siku zote mioyo yao imepotoka, nao hawajazijua njia zangu.’ Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu, ‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ” Ndugu zangu, angalieni, asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai. Lakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu iitwapo Leo, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.