Waebrania 9:8-14
Waebrania 9:8-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Kutokana na taratibu hizo Roho Mtakatifu anafundisha wazi kwamba wakati ile hema ya nje ingali ipo imesimama, njia ya kuingia Mahali Patakatifu sana haijafunguliwa. Jambo hili ni mfano wa nyakati za sasa, ambapo zawadi na tambiko zinatolewa lakini haziwezi kuifanya dhamiri za wanaoabudu kuwa kamilifu, kwani haya yote yanahusika na vyakula, vinywaji na taratibu mbalimbali za kutawadha. Yote hayo ni maagizo ya njenje tu; na nguvu yake hukoma wakati Mungu atakaporekebisha vitu vyote. Lakini Kristo amekwisha fika, akiwa kuhani mkuu wa mambo yaliyo mema, ambayo sasa yamekwisha fika. Yeye anatoa huduma zake katika hema iliyo bora na kamilifu zaidi, isiyofanywa kwa mikono ya watu, yaani isiyo ya ulimwengu huu ulioumbwa. Yeye aliingia Mahali Patakatifu mara moja tu, akiwa amechukua, sio damu ya mbuzi na ng'ombe, bali amechukua damu yake yeye mwenyewe, akatupatia ukombozi wa milele. Watu waliokuwa najisi kidini waliweza kutakasika na kuwa safi waliponyunyiziwa damu ya mbuzi na ya ng'ombe pamoja na majivu ya ndama. Lakini, kwa damu ya Kristo, mambo makuu zaidi hufanyika! Kwa nguvu ya Roho wa milele, Kristo alijitolea mwenyewe tambiko kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo kifo, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai.
Waebrania 9:8-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Roho Mtakatifu akionesha neno hili, ya kwamba njia ya kupaingia patakatifu ilikuwa haijadhihirishwa bado, hapo hema ya kwanza ilipokuwa ingali ikisimama; ambayo ndiyo mfano wa wakati huu ulioko sasa; wakati huo sadaka na dhabihu zinatolewa, zisizoweza kwa jinsi ya dhambi kumkamilisha mtu aabuduye, kwa kuwa ni sheria za jinsi ya mwili tu, vyakula na vinywaji na kunawa kwingine kwingine, zilizoamriwa hata wakati wa matengenezo mapya. Lakini Kristo akiisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu, wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na dosari, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?
Waebrania 9:8-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Roho Mtakatifu akionyesha neno hili, ya kwamba njia ya kupaingia patakatifu ilikuwa haijadhihirishwa bado, hapo hema ya kwanza ilipokuwa ingali ikisimama; ambayo ndiyo mfano wa wakati huu uliopo sasa; wakati huo sadaka na dhabihu zinatolewa, zisizoweza kwa jinsi ya dhambi kumkamilisha mtu aabuduye, kwa kuwa ni sheria za jinsi ya mwili tu, vyakula na vinywaji na kutawadha kwingine kwingine, zilizoamriwa hata wakati wa matengenezo mapya. Lakini Kristo akiisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu, wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng’ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?
Waebrania 9:8-14 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Kwa njia hii, Roho wa Mungu alikuwa anaonesha kwamba, maadamu lile hema la kwanza lilikuwa bado limesimama, njia ya kuingia Patakatifu pa Patakatifu ilikuwa bado haijafunguliwa. Huu ulikuwa mfano kwa ajili ya wakati wa sasa, kuonesha kwamba sadaka na dhabihu zilizokuwa zikitolewa hazikuweza kusafisha dhamiri ya mtu anayeabudu. Lakini hizi zilishughulika tu na vyakula na vinywaji, pamoja na taratibu mbalimbali za kunawa kwa nje, kanuni kwa ajili ya mwili zilizowekwa hadi wakati utimie wa matengenezo mapya. Al-Masihi alipokuja akiwa Kuhani Mkuu wa mambo mema ambayo tayari yameshawasili, alipitia kwenye hema iliyo kuu zaidi na bora zaidi, ambayo haikutengenezwa kwa mikono ya binadamu, hii ni kusema, ambayo si sehemu ya uumbaji huu. Hakuingia kupitia kwa damu ya mbuzi na ya ndama; lakini aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kwa damu yake mwenyewe, akiisha kupata ukombozi wa milele. Damu ya mbuzi na ya mafahali, na majivu ya mitamba walivyonyunyiziwa wale waliokuwa najisi viliwatakasa, hata kuwaondolea uchafu wa nje. Basi damu ya Al-Masihi, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na waa, si itazisafisha dhamiri zetu zaidi kutokana na matendo yaletayo mauti, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai!