Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hosea 12:1-14

Hosea 12:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Watu wa Efraimu wananirundikia uongo, na Waisraeli udanganyifu. Watu wa Yuda, wananiasi mimi Mungu Mtakatifu. “Watu wa Efraimu wanachunga upepo kutwa nzima wanafukuza upepo wa mashariki. Wanazidisha uongo na ukatili, wanafanya mkataba na Ashuru na kupeleka mafuta Misri.” Mwenyezi-Mungu ana mashtaka dhidi ya Yuda; atawaadhibu wazawa wa Yakobo kadiri ya makosa yao, na kuwalipa kadiri ya matendo yao. Yakobo akiwa bado tumboni mwa mama yake, alimshika kisigino kaka yake. Na alipokuwa mtu mzima alishindana na Mungu. Alipambana na malaika, akamshinda; alilia machozi na kuomba ahurumiwe. Huko Betheli, alikutana na Mungu, huko Mungu aliongea naye. Mwenyezi-Mungu, wa majeshi, Mwenyezi-Mungu, ndilo jina lake. Lakini nyinyi mrudieni Mungu wenu. Zingatieni upendo na haki, mtumainieni Mungu wenu daima. “Efraimu ni sawa na mfanyabiashara atumiaye mizani danganyifu, apendaye kudhulumu watu. Efraimu amesema, ‘Mimi ni tajiri! Mimi nimejitajirisha! Hamna ubaya kupata faida. Hata hivyo, hilo si kosa!’” Mwenyezi-Mungu asema, “Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wako; mimi ndimi niliyekutoa nchini Misri! Mimi nitakukalisha tena katika mahema, kama ufanyavyo sasa kwa siku chache tu, wakati wa sikukuu ya vibanda. Mimi niliongea na manabii; ni mimi niliyewapa maono mengi, na kwa njia yao natangaza mpango wangu. Huko Gileadi ni mahali pa dhambi; huko Gilgali walitambika fahali, kwa hiyo madhabahu zao zitakuwa marundo ya mawe kwenye mitaro shambani.” Yakobo alikimbia nchi ya Aramu akiwa huko alifanya kazi apate mke, akachunga kondoo ili apate mke. Kwa nabii Mwenyezi-Mungu aliwatoa Waisraeli nchini Misri, na kwa nabii Mungu aliwahifadhi. Waefraimu wamemchukiza Mwenyezi-Mungu sana. Lakini Mwenyezi-Mungu atawalipiza makosa yao, atawaadhibu kwa mambo maovu waliyotenda.

Shirikisha
Soma Hosea 12

Hosea 12:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Efraimu hujilisha upepo, na kuandamana na upepo wa mashariki; haachi kuongeza uongo na uharibifu; nao wafanya agano na Ashuru, na mafuta huchukuliwa kwenda Misri. BWANA naye ana shutuma juu ya Yuda, naye atamwadhibu Yakobo kwa kadiri ya njia zake; kwa kadiri ya matendo yake atamlipa. Tumboni alimshika ndugu yake kisigino; Na alipokuwa mtu mzima alishindana na Mungu; Naam, alishindana na malaika Akashinda; alilia, na kumsihi; Alimwona huko Betheli, naye akasema nasi huko; Naam, BWANA, Mungu wa majeshi; BWANA ndilo kumbukumbu lake. Basi, mrudie Mungu wako; shika fadhili na hukumu; ukamngojee Mungu wako daima. Ni mfanya biashara, aliye na mizani ya udanganyifu mkononi mwake; anapenda kudhulumu. Naye Efraimu alisema, Kweli nimekuwa tajiri, nimejipatia mali nyingi; katika kazi zangu zote hawataona kwangu uovu wowote uliokuwa dhambi. Lakini mimi ni BWANA, Mungu wako tangu ulipotoka katika nchi ya Misri; nitakukalisha tena katika hema, kama siku za sikukuu teule. Tena nimenena na hao manabii, nami nimeongeza maono, na kwa utumishi wa manabii nimetumia mifano. Katika Gileadi kuna uovu? Nao wamekuwa ubatili tu; huko Gilgali hutoa dhabihu za ng'ombe; naam, madhabahu zao zimekuwa kama chungu katika matuta ya mashamba. Na Yakobo alikimbia mpaka Padan-Aramu, Na Israeli alitumika apate mke; Ili apate mke alichunga kondoo. Na kwa nabii BWANA alimtoa Israeli katika Misri, Na kwa mkono wa nabii alihifadhiwa. Efraimu amenitia hasira kali sana; kwa sababu hiyo damu yake itaachwa juu yake, na Bwana wake atamrudishia lawama yake.

Shirikisha
Soma Hosea 12

Hosea 12:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Efraimu hujilisha upepo, na kuandamana na upepo wa mashariki; haachi kuongeza uongo na uharibifu; nao wafanya agano na Ashuru, na mafuta huchukuliwa kwenda Misri. BWANA naye ana mateto na Yuda, naye atamwadhibu Yakobo kwa kadiri ya njia zake; kwa kadiri ya matendo yake atamlipa. Tumboni alimshika ndugu yake kisigino; Na alipokuwa mtu mzima alikuwa na uwezo kwa Mungu; Naam, alikuwa na uwezo juu ya malaika Akashinda; alilia, na kumsihi; Alimwona huko Betheli, naye akasema nasi huko; Naam, BWANA, Mungu wa majeshi; BWANA ndilo kumbukumbu lake. Basi, mrudie Mungu wako; shika fadhili na hukumu; ukamngojee Mungu wako daima. Ni mchuuzi, mizani ya udanganyifu i mkononi mwake; anapenda kudhulumu. Naye Efraimu alisema, Kweli nimekuwa tajiri, nimejipatia mali nyingi; katika kazi zangu zote hawataona kwangu uovu wo wote uliokuwa dhambi. Lakini mimi ni BWANA, Mungu wako tangu ulipotoka katika nchi ya Misri; nitakukalisha tena katika hema, kama siku za karamu ya idi. Tena nimenena na hao manabii, nami nimeongeza maono, na kwa utumishi wa manabii nimetumia mifano. Je! Gileadi ni uovu? Wamekuwa ubatili tu; huko Gilgali hutoa dhabihu za ng’ombe; naam, madhabahu zao zimekuwa kama chungu katika matuta ya mashamba. Na Yakobo alikimbia mpaka Padan-Aramu, Na Israeli alitumika apate mke; Ili apate mke alichunga kondoo. Na kwa nabii BWANA alimtoa Israeli katika Misri, Na kwa mkono wa nabii alihifadhiwa. Efraimu amenitia hasira kali sana; kwa sababu hiyo damu yake itaachwa juu yake, na Bwana wake atamrudishia lawama yake.

Shirikisha
Soma Hosea 12

Hosea 12:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Efraimu anajilisha upepo; hufukuzia upepo wa mashariki kutwa nzima na kuzidisha uongo na jeuri. Anafanya mkataba na Ashuru na kutuma mafuta ya zeituni Misri. BWANA analo shtaka dhidi ya Yuda, atamwadhibu Yakobo kwa kadiri ya njia zake na kumlipa kwa kadiri ya matendo yake. Yakobo akiwa tumboni alishika kisigino cha kaka yake; kama mwanadamu, alishindana na Mungu. Alishindana na malaika na kumshinda; alilia na kuomba upendeleo wake. Alimkuta huko Betheli na kuzungumza naye huko: BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote, BWANA ndilo jina lake! Lakini ni lazima urudi kwa Mungu wako; dumisha upendo na haki, nawe umngojee Mungu wako siku zote. Mfanyabiashara hutumia vipimo vya udanganyifu; hupenda kupunja. Efraimu hujisifu akisema, “Mimi ni tajiri sana; nimetajirika. Pamoja na utajiri wangu wote hawatakuta ndani yangu uovu wowote au dhambi.” “Mimi ndimi BWANA Mungu wenu niliyewaleta kutoka Misri; nitawafanya mkae tena kwenye mahema, kama vile katika siku za sikukuu zenu zilizoamriwa. Niliongea na manabii, nikawapa maono mengi na kusema mifano kupitia wao.” Je, Gileadi si mwovu? Watu wake hawafai kitu! Je, hawatoi dhabihu za mafahali huko Gilgali? Madhabahu zao zitakuwa kama malundo ya mawe katika shamba lililolimwa. Yakobo alikimbilia katika nchi ya Aramu; Israeli alitumika ili apate mke, ili aweze kulipa kwa ajili yake alichunga kondoo. BWANA alimtumia nabii kumpandisha Israeli kutoka Misri, kwa njia ya nabii alimtunza. Lakini Efraimu amemchochea sana hasira; Bwana wake ataleta juu yake hatia yake ya kumwaga damu naye atamlipiza kwa ajili ya dharau yake.

Shirikisha
Soma Hosea 12