Hosea 4:10-19
Hosea 4:10-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Watakula, lakini hawatashiba; watazini, lakini hawatapata watoto, kwa sababu wameniacha mimi Mwenyezi-Mungu, na kufuata miungu mingine. “Divai mpya na ya zamani huondoa maarifa. Watu wangu huomba shauri kutoka kwa mti; kijiti chao cha ramli ndicho kinachowapa kauli. Nia ya kufanya uzinzi imewapotosha; wamefanya uzinzi kwa kufuata miungu mingine, wakaniacha mimi Mungu wao. Wanatambikia kwenye vilele vya milima; naam, wanatoa tambiko vilimani, chini ya mialoni, migude na mikwaju, maana kivuli chao ni kizuri. “Kwa hiyo binti zenu hufanya uzinzi, na bibiarusi wenu hufanya uasherati. Lakini sitawaadhibu binti zenu wanapofanya uzinzi, wala bibi arusi wenu wanapofanya uasherati, maana, wanaume wenyewe ndio wanaofuatana na wazinzi, na kutambikia pamoja nao katika ibada za uzinzi. Watu hawa watovu wa akili hakika wataangamia! “Ama kweli nyinyi Waisraeli ni wazinzi! Lakini, msiwafanye watu wa Yuda wawe na hatia! Msiende mahali patakatifu huko Gilgali, wala msiende kule Beth-aveni. Wala msiape mkisema, ‘Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo!’” Waisraeli ni wakaidi kama punda. Kwa nini basi Mungu ashughulike kuwachunga, kama kondoo kwenye malisho mapana? “Watu wa Efraimu wamejifunga na sanamu. Haya! Waache waendelee tu! Kama vile genge la walevi, wanajitosa wenyewe katika uzinzi; wanapendelea aibu kuliko heshima yao. Basi, kimbunga kitawapeperusha, na watayaonea aibu matambiko yao kwa miungu ya uongo.
Hosea 4:10-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nao watakula, lakini hawatashiba; watafanya zinaa, lakini hawataongezeka; kwa sababu wameacha kumwangalia BWANA. Uzinzi na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu. Watu wangu hutaka shauri kwa kipande cha mti, na fimbo yao huwatolea uaguzi; maana roho ya uzinzi imewapotosha, wakawacha Mungu wao. Hutoa dhabihu juu ya vilele vya milima, na kufukiza uvumba juu ya vilima, chini ya mialoni na milibua na miela, kwa kuwa uvuli wake ni mwema; kwa sababu hiyo binti zenu huzini, na bibi arusi zenu hufanya uasherati. Sitawaadhibu binti zenu wazinipo, wala bibi arusi zenu wafanyapo uasherati; maana wenyewe huenda kando pamoja na wanawake wazinzi, hutoa dhabihu pamoja na makahaba; na watu hawa wasiofahamu wataangamia. Ingawa wewe, Israeli, unafanya uzinzi, lakini asiasi Yuda; nanyi msiende Gilgali wala msipande mpaka Beth-aveni, wala msiape mkisema, Aishivyo BWANA. Kwa maana Israeli ametenda kwa ukaidi, kama ndama mkaidi; sasa je! BWANA atawalisha kama mwana-kondoo katika mahali penye malisho mazuri. Efraimu amejiungamanisha na sanamu; mwache. Kileo chao kimegeuka kuwa uchungu; huzini daima; wakuu wake hupenda aibu. Upepo umemfunika kwa mbawa zake; nao watatahayarika kwa sababu ya dhabihu zao.
Hosea 4:10-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nao watakula, lakini hawatashiba; watafanya zinaa, lakini hawataongezeka; kwa sababu wameacha kumwangalia BWANA. Uzinzi na divai na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu. Watu wangu hutaka shauri kwa gongo lao, na fimbo yao huwahubiri mambo; maana roho ya uzinzi imewakosesha, nao wamekwenda kuzini mbali na Mungu wao. Hutoa dhabihu juu ya vilele vya milima, na kufukiza uvumba juu ya vilima, chini ya mialoni na milibua na miela, kwa kuwa uvuli wake ni mwema; kwa sababu hiyo binti zenu huzini, na bibi arusi zenu hufanya uasherati. Sitawaadhibu binti zenu wazinipo, wala bibi arusi zenu wafanyapo uasherati; maana wao wenyewe huenda kando pamoja na wanawake wazinzi, hutoa dhabihu pamoja na makahaba; na watu hawa wasiofahamu wataangamia. Ingawa wewe, Israeli, unafanya uzinzi, lakini asiasi Yuda; nanyi msiende Gilgali wala msipande mpaka Beth-Aveni, wala msiape mkisema, Aishivyo BWANA. Kwa maana Israeli ametenda kwa ukaidi, kama ndama mkaidi; sasa je! BWANA atawalisha kama mwana-kondoo katika mahali penye nafasi! Efraimu amejiungamanisha na sanamu; mwache. Kileo chao kimegeuka kuwa uchungu; huzini daima; wakuu wake hupenda aibu. Upepo umemfunikiza kwa mbawa zake; nao watatahayarika kwa sababu ya dhabihu zao.
Hosea 4:10-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Watakula lakini hawatashiba; watajiingiza katika ukahaba lakini hawataongezeka, kwa sababu wamemwacha BWANA na kujiingiza wenyewe katika ukahaba, divai ya zamani na divai mpya, ambavyo huondoa ufahamu wa watu wangu. Hutaka shauri kutoka kwa sanamu ya mti nao hujibiwa na fimbo ya mti. Roho ya ukahaba imewapotosha, hawana uaminifu kwa Mungu wao. Wanatoa dhabihu juu ya vilele vya milima na sadaka za kuteketezwa juu ya vilima, chini ya mialoni, milibua na miela, ambako kuna vivuli vizuri. Kwa hiyo binti zenu wamegeukia ukahaba na wake za wana wenu uzinzi. “Sitawaadhibu binti zenu wakati wanapogeukia ukahaba, wala wake za wana wenu wanapofanya uzinzi, kwa sababu wanaume wenyewe huandamana na malaya na kutambikia pamoja na makahaba wa mahali pa kuabudia miungu: watu wasiokuwa na ufahamu wataangamia! “Ingawa umefanya uzinzi, ee Israeli, Yuda naye asije akawa na hatia. “Usiende Gilgali, usipande kwenda Beth-Aveni Wala usiape, ‘Hakika kama BWANA aishivyo!’ Waisraeli ni wakaidi, kama mtamba wa ngʼombe ambaye ni mkaidi. Ni jinsi gani basi BWANA anaweza kuwachunga kama wana-kondoo katika shamba la majani? Efraimu amejiunga na sanamu, ondokana naye! Hata wakati wamemaliza vileo vyao wanaendelea na ukahaba wao, watawala wao hupenda sana njia za aibu. Kisulisuli kitawafagilia mbali na dhabihu zao zitawaletea aibu.