Isaya 20:1-6
Isaya 20:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Sargoni mfalme wa Ashuru, alimtuma jemadari wake mkuu kuuvamia mji wa Ashdodi. Naye akaushambulia na kuuteka. Miaka mitatu kabla ya hapo, Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwambia Isaya, mwana wa Amozi hivi: “Nenda ukavue vazi la gunia unalovaa kiunoni, na viatu miguuni mwako.” Isaya akafanya hivyo; akawa anatembea uchi na bila viatu. Basi, mnamo mwaka huo mji wa Ashdodi ulipotekwa, Mwenyezi-Mungu alisema: “Mtumishi wangu Isaya amekuwa akitembea uchi na bila viatu kwa muda wa miaka mitatu sasa, kama ishara na alama dhidi ya nchi ya Misri na Kushi. Basi, mfalme wa Ashuru atawachukua mateka Wamisri na Wakushi, wakubwa kwa wadogo. Watachukuliwa, nao watatembea uchi na bila viatu; matako wazi, kwa aibu ya Misri. Kisha wote waliotegemea Kushi na kujivunia Misri watajuta na kufadhaika. Wakati huo, wakazi wa pwani ya Filistia watasema, ‘Tazameni yaliyowapata watu tuliowategemea na kuwakimbilia kuomba msaada watuokoe na mfalme wa Ashuru! Na sasa, sisi tutawezaje kusalimika?’”
Isaya 20:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika mwaka ule jemadari yule alipofika Ashdodi, alipotumwa na Sargoni mfalme wa Ashuru; naye alipigana na Ashdodi akautwaa; wakati huo BWANA alinena kwa kinywa cha Isaya, mwana wa Amozi, akisema, Haya, uvue nguo ya magunia viunoni mwako, na viatu vyako miguuni mwako. Naye akafanya hivyo akaenda uchi, miguu yake ikiwa haina viatu. BWANA akasema, Kama vile mtumishi wangu Isaya anavyokwenda uchi, bila viatu, awe ishara na ajabu kwa muda wa miaka mitatu juu ya Misri na juu ya Kushi; vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawachukua uchi, wafungwa wa Misri, na watu wa Kushi waliohamishwa, watoto kwa wazee, bila viatu, matako yao wazi, Misri iaibishwe. Nao watafadhaika, na kuona haya kwa ajili ya Kushi, matumaini yao, na Misri, utukufu wao. Na mwenyeji wa nchi ya pwani atasema katika siku hiyo, Angalia, haya ndiyo yaliyowapata watu wale tuliowatumainia, ambao tuliwakimbilia watuokoe kutoka kwa mfalme wa Ashuru; na sisi je! Twawezaje kupona?
Isaya 20:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika mwaka ule jemadari yule alipofika Ashdodi, alipotumwa na Sargoni mfalme wa Ashuru; naye alipigana na Ashdodi akautwaa; wakati huo BWANA alinena kwa kinywa cha Isaya, mwana wa Amozi, akisema, Haya, uvue nguo ya magunia viunoni mwako, na viatu vyako miguuni mwako. Naye akafanya hivyo akaenda uchi, miguu yake haina viatu. BWANA akasema, Kama vile mtumishi wangu Isaya anavyokwenda uchi, hana viatu, awe ishara na ajabu kwa muda wa miaka mitatu juu ya Misri na juu ya Kushi; vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawachukua uchi, wafungwa wa Misri, na watu wa Kushi waliohamishwa, watoto kwa wazee, hawana viatu, matako yao wazi, Misri iaibishwe. Nao watafadhaika, na kuona haya kwa ajili ya Kushi, matumaini yao, na Misri, utukufu wao. Na mwenyeji wa nchi ya pwani atasema katika siku hiyo, Angalia, haya ndiyo yaliyowapata watu wale tuliowatumaini, ambao tuliwakimbilia watuokoe na mfalme wa Ashuru; na sisi je! Twawezaje kupona?
Isaya 20:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mwaka ule jemadari mkuu alitumwa na Mfalme Sargoni wa Ashuru, naye akaja Ashdodi, akaushambulia na kuuteka, wakati huo BWANA alisema kwa kinywa cha Isaya mwana wa Amozi. Akamwambia, “Vua gunia kutoka mwilini mwako na viatu kutoka miguuni mwako.” Naye akafanya hivyo, akitembea uchi, bila viatu. Kisha BWANA akasema, “Kama mtumishi wangu Isaya alivyotembea uchi na bila viatu kwa miaka mitatu, kama ishara na dalili mbaya dhidi ya nchi ya Misri na Kushi, vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawaongoza mateka wa Wamisri, na watu wa uhamisho wa Kushi, uchi na bila viatu, vijana hata wazee, wakiwa matako wazi, kwa aibu ya Wamisri. Wale waliotegemea Kushi na kujivunia Misri wataogopa na kuaibika. Katika siku ile watu wanaoishi katika pwani hii watasema, ‘Tazama lililowapata wale tuliowategemea, wale tuliowakimbilia kwa msaada na wokovu kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru! Tutawezaje basi kupona?’ ”