Isaya 21:1-17
Isaya 21:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Kauli ya Mungu dhidi ya jangwa kando ya bahari. Kama vimbunga vinavyovuma kutoka kusini, wavamizi wanakuja kutoka jangwani, kutoka katika nchi ya kutisha. Nimeoneshwa maono ya kutisha, maono ya watu wa hila watendao hila, maono ya watu waangamizi wafanyao maangamizi. Pandeni juu vitani enyi Waelamu; shambulieni enyi Wamedi! Mungu atakomesha mateso yote yaliyoletwa na Babuloni. Kwa maono hayo nimeingiwa na hofu kubwa, uchungu mwingi umenikumba; kama uchungu wa mama anayejifungua. Maumivu yamenizidi hata siwezi kusikia; nimefadhaika hata siwezi kuona. Moyo unanidunda na woga umenikumba. Nilitamani jioni ifike lakini ilipofika ikawa ya kutetemesha. Chakula kimetayarishwa, shuka zimetandikwa, sasa watu wanakula na kunywa. Ghafla, sauti inasikika: “Inukeni enyi watawala! Wekeni silaha tayari!” Maana Bwana aliniambia, “Nenda ukaweke mlinzi; mwambie atangaze atakachoona. Akiona kikosi, wapandafarasi wawiliwawili, wapandangamia na wapandapunda, na awe macho; naam, akae macho!” Kisha huyo mlinzi akapaza sauti: “Bwana, nimesimama juu ya mnara wa ulinzi mchana kutwa, nimeshika zamu usiku kucha!” Tazama, kikosi kinakuja, wapandafarasi wawiliwawili. Wanasema: “Babuloni umeanguka! Umeanguka! Sanamu zote za miungu yake zimetupwa chini na kuvunjwavunjwa!” Ewe Israeli, watu wangu, enyi mliotwangwa na kupurwa kama nafaka. Sasa nimewaambieni mambo niliyoyasikia kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli. Kauli ya Mungu dhidi ya Duma. Ninasikia mtu ananiita kutoka Seiri: “Mlinzi, nini kipya leo usiku? Kuna kipya chochote leo usiku?” Nami mlinzi nikajibu: “Asubuhi inakuja, kadhalika na usiku; ukitaka kuuliza, uliza tu; nenda urudi tena.” Kauli ya Mungu dhidi ya Arabia. Enyi misafara ya Dedani, pigeni kambi leo usiku kwenye nyika za Arabia. Enyi wakazi wa nchi ya Tema, wapeni maji hao wenye kiu; wapelekeeni chakula hao wakimbizi. Maana wamekimbia mapanga, mapanga yaliyochomolewa, pinde zilizovutwa na ukali wa mapigano. Maana Bwana aliniambia hivi: “Katika muda wa mwaka mmoja, bila kuzidi wala kupungua, fahari yote ya Kedari itakwisha. Wapiga upinde wachache kati ya mashujaa wa watu wa Kedari ndio watakaosalia. Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nimenena.”
Isaya 21:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ufunuo juu ya nyika kando ya bahari. Kama tufani za Negebu zikaribiavyo kwa kasi, inakuja kutoka kwa nyika, toka nchi itishayo. Nimeoneshwa maono magumu; atendaye hila anatenda hila, mharibu anaharibu. Panda juu, Ee Elamu; husuru, Ee Umedi; mimi ninakomesha maombolezo yake yote. Kwa sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, uchungu umenishika, kama uchungu wa mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa wa hofu, nisiweze kuona. Moyo wangu unapigapiga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka likanitetemesha. Wanaandaa meza, wanaweka ulinzi, wanakula, wanakunywa. Simameni, enyi wakuu, itieni ngao mafuta. Maana Bwana ameniambia hivi, Nenda, weka mlinzi; aonayo na ayatangaze. Naye akiona kundi la wapanda farasi, wakienda wawili wawili, na kundi la punda, na kundi la ngamia; na asikilize kwa makini, kwa makini sana. Ndipo akalia kama simba, Ee Bwana, mimi nasimama daima juu ya mnara wakati wa mchana, na kila usiku ninakaa katika zamu ya ulinzi wangu. Na, tazama, linakuja kundi la watu, wapanda farasi, wakienda wawili wawili. Akajibu na kusema, Babeli umeanguka, umeanguka; na sanamu zote za miungu yake zimevunjwa chini. Ewe wangu niliyekufikicha na kukupura; Hayo niliyoyasikia kwa BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, nayatangaza kwenu. Ufunuo juu ya Duma. Mtu ananililia toka Seiri, Ee mlinzi, habari gani za usiku? Ee mlinzi, habari gani za usiku? Mlinzi akasema, Mchana unakuja na usiku pia; mkitaka kuuliza, ulizeni; njoni tena. Ufunuo juu ya Arabuni. Ndani ya msitu wa Arabuni mtalala, Enyi misafara ya Wadedani. Waleteeni wenye kiu maji, Enyi wenyeji wa nchi ya Tema; Nendeni kuwalaki wakimbiao na chakula chao. Kwa maana wanakimbia mbele ya panga, Upanga uliofutwa, na upinde uliopindwa, Na mbele ya ukali wa vita. Kwa sababu Bwana ameniambia hivi, Katika muda wa mwaka, kama miaka ya mtu mwenye kuajiriwa, utaangamia utukufu wote wa Kedari. Na mabaki ya hesabu ya wavuta pinde, hao mashujaa wa Kedari watakuwa wachache; maana BWANA, Mungu wa Israeli, amenena neno hili.
Isaya 21:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ufunuo juu ya bara ya bahari. Kama tufani za Negebu zikaribiavyo kwa kasi, inakuja kutoka bara, toka nchi itishayo. Nimeonyeshwa maono magumu; atendaye hila anatenda hila, mharibu anaharibu. Panda juu, Ee Elamu; husuru, Ee Umedi; mimi ninakomesha maombolezo yake yote. Kwa sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, utungu umenishika, kama utungu wa mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa wa hofu, nisiweze kuona. Moyo wangu unapiga-piga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka likanitetemesha. Wanaandika meza, wanaweka ulinzi, wanakula, wanakunywa. Simameni, enyi wakuu, itieni ngao mafuta. Maana Bwana ameniambia hivi, Enenda, weka mlinzi; aonayo na ayatangaze. Naye akiona kundi la wapanda farasi, wakienda wawili wawili, na kundi la punda, na kundi la ngamia; asikilize sana, akijitahidi kusikiliza. Ndipo akalia kama simba, Ee Bwana, mimi nasimama daima juu ya mnara wakati wa mchana, na kila usiku ninakaa katika zamu ya ulinzi wangu. Na, tazama, linakuja kundi la watu, wapanda farasi, wakienda wawili wawili. Akajibu na kusema, Babeli umeanguka, umeanguka; na sanamu zote za miungu yake zimevunjwa chini. Ewe niliyekufikicha, na nafaka ya sakafu yangu; Hayo niliyoyasikia kwa BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, nimewapasha habari zake. Ufunuo juu ya Duma. Mtu ananililia toka Seiri, Ee mlinzi, habari gani za usiku? Ee mlinzi, habari gani za usiku? Mlinzi akasema, Mchana unakuja na usiku pia; mkitaka kuuliza, ulizeni; njoni tena. Ufunuo juu ya Arabuni. Ndani ya msitu wa Arabuni mtalala, Enyi misafara ya Wadedani. Waleteeni wenye kiu maji, Enyi wenyeji wa nchi ya Tema; Nendeni kuwalaki wakimbiao na chakula chao. Kwa maana wanakimbia mbele ya panga, Upanga uliofutwa, na upinde uliopindwa, Na mbele ya ukali wa vita. Kwa sababu Bwana ameniambia hivi, Katika muda wa mwaka, kama miaka ya mtu mwenye kuajiriwa, utaangamia utukufu wote wa Kedari. Na mabaki ya hesabu ya wavuta pinde, hao mashujaa wa Kedari watakuwa wachache; maana BWANA, Mungu wa Israeli, amenena neno hili.
Isaya 21:1-17 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Neno la unabii kuhusu Jangwa kando ya Bahari: Kama upepo wa kisulisuli unaopita katika nchi hadi kusini, mshambuliaji anakuja kutoka jangwani, kutoka nchi inayotisha. Nimeoneshwa maono ya kutisha: Msaliti anasaliti, mteka nyara anateka nyara. Elamu, shambulia! Umedi, zingira kwa jeshi! Nitakomesha huzuni zote alizosababisha. Kwa sababu hii, mwili wangu umeteswa na maumivu, maumivu makali ya ghafula yamenishika, kama yale ya mwanamke mwenye uchungu wa kuzaa. Nimeduwazwa na lile ninalolisikia, nimeshangazwa na lile ninaloliona. Moyo wangu unababaika, woga unanifanya nitetemeke, gizagiza la jioni nililolitamani sana, limekuwa hofu kuu kwangu. Wanaandaa meza, wanatandaza mazulia, wanakula, wanakunywa! Amkeni, enyi maafisa, zitieni ngao mafuta! Hili ndilo Bwana analoniambia: “Nenda, weka mlinzi, na atoe taarifa ya kile anachokiona. Anapoona magari ya vita pamoja na kundi la farasi, wapanda punda au wapanda ngamia, na awe macho, awe macho kikamilifu.” Naye mlinzi alipaza sauti, “Mchana baada ya mchana, bwana wangu, ninasimama katika mnara wa ulinzi, kila usiku ninakaa mahali pangu nilipoamriwa. Tazama, yuaja mtu anayepanda gari la vita pamoja na kundi la farasi. Naye anajibu: ‘Babeli umeanguka, umeanguka! Vinyago vyote vya miungu yake vimelala chini vikiwa vimevunjwa!’ ” Ee watu wangu, mliopondwa kwenye sakafu ya kupuria, ninawaambia kile nilichokisikia kutoka kwa BWANA wa majeshi, kutoka kwa Mungu wa Israeli. Neno la unabii kuhusu Duma: Mtu fulani ananiita kutoka Seiri, “Mlinzi, usiku utaisha lini? Mlinzi, usiku utaisha lini?” Mlinzi anajibu, “Asubuhi inakuja, lakini pia usiku. Ukitaka kuuliza, basi uliza; na urudi mara tena.” Neno la unabii kuhusu Arabia: Enyi misafara ya Wadedani, mnaopiga kambi katika vichaka vya Arabia, leteni maji kwa wenye kiu, ninyi mnaoishi Tema, leteni chakula kwa ajili ya wakimbizi. Wanaukimbia upanga, upanga uliochomolewa alani, kutoka upinde uliopindwa, na kutoka kwa joto la vita. Hili ndilo Bwana analoniambia: “Katika muda wa mwaka mmoja, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, majivuno yote ya Kedari yatafikia mwisho. Wanaume wavutao pinde walionusurika, mashujaa wa Kedari, watakuwa wachache.” BWANA, Mungu wa Israeli, amesema.