Isaya 22:15-25
Isaya 22:15-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliniambia niende kwa Shebna, msimamizi wa jamaa ya kifalme, nikamwambie hivi: “Una haki gani kuwa huku? Je, una ndugu yeyote hapa, hata ukajichongea kaburi mwambani juu ya mlima? Wewe ni mwenye nguvu, lakini Mwenyezi-Mungu atakutupilia mbali kwa nguvu. Atakubana kabisa na kukuzungushazungusha, kisha atakutupa kama mpira mpaka katika nchi pana. Huko utafia karibu na magari yako ya vita unayojivunia. Wewe ni aibu kwa nyumba ya bwana wako. Mwenyezi-Mungu atakungoa madarakani mwako na kukuporomosha kutoka mahali ulipo. “Siku hiyo, nitamleta mtumishi wangu Eliakimu mwana wa Hilkia. Nitamvisha vazi lako rasmi, nitamfunga mshipi wako na kumpa madaraka yako. Yeye atakuwa baba kwa watu wa Yerusalemu na kwa ukoo wa Yuda. Nitamwekea begani mwake ufunguo wa nyumba ya Daudi. Akifungua, hakuna atakayeweza kufunga na akifunga, hakuna atakayeweza kufungua. Nitamwimarisha Eliakimu kama kigingi kilichofungiwa mahali salama, naye atapata heshima tukufu katika ukoo wa wazee wake. “Watu wote na jamaa yake, wadogo kwa wakubwa watajitegemeza kwake kama chungu na vikombe vilivyotundikwa kwenye kigingi. Lakini siku moja, kama vile kile kigingi kilichofungwa mahali salama kitalegea kwa uzito, Eliakimu naye atapoteza madaraka yake na jamaa zake wote watabaki bila msaada. Mimi Mwenyezi-Mungu nimenena.”
Isaya 22:15-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Bwana, BWANA wa majeshi, asema hivi, Haya! Nenda kwa huyu mtunza hazina, yaani, Shebna, aliye juu ya nyumba, ukamwambie, Unafanyaje hapa? Nawe una nani hapa? Hata ukachimba kaburi hapa; ukamchimbia kaburi huko juu, na kumchongea makao katika jabali! Tazama, BWANA atakutupa kwa nguvu, kama mtu mwenye nguvu; naam, atakuzongazonga. Hakika atakukunja na kukutupa kama mpira, mpaka nchi iliyo mbali; huko utakufa, na magari ya utukufu wako yatakuwa kuko huko, ewe uliye aibu ya nyumba ya bwana wako. Nami nitakusukuma na kukutoa katika mahali pako, naye atakushusha utoke hapa usimamapo. Na itakuwa katika siku ile nitamwita mtumishi wangu Eliakimu, mwana wa Hilkia; nami nitamvika vazi lako, nitamtia nguvu kwa mshipi wako, nami nitamkabidhi yeye mamlaka yako; naye atakuwa baba kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa nyumba ya Yuda. Na ufunguo wa nyumba ya Daudi nitauweka begani mwake; yeye atafungua wala hapana atakayefunga; naye atafunga wala hapana atakayefungua. Nami nitamkaza kama msumari mahali palipo imara; naye atakuwa kiti cha utukufu kwa nyumba ya baba yake. Nao wataangika juu yake utukufu wote wa nyumba ya baba yake; wazao wake na watoto wao, kila chombo kidogo tangu vyombo vya vikombe hata vyombo vya makopo vyote pia. Katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, ule msumari uliokazwa katika mahali palipo imara utalegea; nao utakatwa na kuanguka chini, na ule mzigo uliokuwa juu yake utakatiliwa mbali; maana BWANA amesema haya.
Isaya 22:15-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Bwana, BWANA wa majeshi, asema hivi, Haya! Enenda kwa huyu mtunza hazina, yaani, Shebna, aliye juu ya nyumba, ukamwambie, Unafanyaje hapa? Nawe una nani hapa? Hata ukachimba kaburi hapa; ukamchimbia kaburi huko juu, na kumchongea makao katika jabali! Tazama, BWANA atakutupa kwa nguvu, kama mtu mwenye nguvu; naam, atakuzonga-zonga. Hakika atakukunja na kukutupa kama mpira, mpaka nchi iliyo mbali; huko utakufa, na magari ya utukufu wako yatakuwa kuko huko, ewe uliye aibu ya nyumba ya bwana wako. Nami nitakusukuma na kukutoa katika mahali pako, naye atakushusha utoke hapa usimamapo. Na itakuwa katika siku ile nitamwita mtumishi wangu Eliakimu, mwana wa Hilkia; nami nitamvika vazi lako, nitamtia nguvu kwa mshipi wako, nami nitamkabidhi yeye mamlaka yako; naye atakuwa baba kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa nyumba ya Yuda. Na ufunguo wa nyumba ya Daudi nitauweka begani mwake; yeye atafungua wala hapana atakayefunga; naye atafunga wala hapana atakayefungua. Nami nitamkaza kama msumari mahali palipo imara; naye atakuwa kiti cha utukufu kwa nyumba ya baba yake. Nao wataangika juu yake utukufu wote wa nyumba ya baba yake; wazao wake na watoto wao, kila chombo kidogo tangu vyombo vya vikombe hata vyombo vya makopo vyote pia. Katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, ule msumari uliokazwa katika mahali palipo imara utalegea; nao utakatwa na kuanguka chini, na ule mzigo uliokuwa juu yake utakatiliwa mbali; maana BWANA amesema haya.
Isaya 22:15-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hili ndilo Bwana, BWANA wa majeshi, asemalo: “Nenda ukamwambie huyu wakili Shebna, ambaye ni msimamizi wa jumba la kifalme: Unafanya nini hapa, na ni nani aliyekupa ruhusa kujikatia kaburi lako mwenyewe, ukichonga kaburi lako mahali palipo juu, na kutoboa kwa patasi mahali pako pa kupumzikia katika mwamba? “Jihadhari, BWANA yu karibu kukukamata thabiti, na kukutupa mbali, ewe mtu mwenye nguvu. Atakuvingirisha uwe kama mpira na kukutupa katika nchi kubwa. Huko ndiko utakakofia, na huko ndiko magari yako ya vita ya fahari yatabakia, na kuwa fedheha kwa nyumba ya bwana wako! Nitakuondoa kutoka kazi yako, nawe utaondoshwa kutoka nafasi yako. “Katika siku ile, nitamwita mtumishi wangu, Eliakimu mwana wa Hilkia. Nitamvika joho lako, nami nitamfunga mshipi wako kiunoni mwake, na kumkabidhi mamlaka yako. Yeye atakuwa baba kwa wale wanaoishi Yerusalemu na kwa nyumba ya Yuda. Nitaweka begani mwake ufunguo wa nyumba ya Daudi. Kile afunguacho hakuna awezaye kufunga, na kile afungacho hakuna awezaye kufungua. Nitampigilia kama kigingi kilicho mahali palipo imara, naye atakuwa kiti cha heshima kwa ajili ya nyumba ya baba yake. Utukufu wote wa jamaa yake utakuwa juu yake: Wazao wa jamaa hiyo na machipukizi yake, vyombo vyake vyote vidogo, tangu bakuli hadi magudulia yote.” BWANA wa majeshi asema, “Katika siku ile, kigingi kilichopigiliwa mahali imara kitaachia njia. Kitakatwa, nacho kitaanguka na mzigo ulioningʼinia juu yake utaanguka chini.” BWANA amesema.