Isaya 54:4-8
Isaya 54:4-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena. Kwa sababu Muumba wako ni mume wako; BWANA wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote. Maana BWANA amekuita kama mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni, kama mke wakati wa ujana, atupwapo, asema Mungu wako. Kwa kitambo kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya. Kwa ghadhabu ifurikayo nalikuficha uso wangu dakika moja; lakini kwa fadhili za milele nitakurehemu, asema BWANA, Mkombozi wako.
Isaya 54:4-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Usiogope maana hutaaibishwa tena; usifadhaike maana hutadharauliwa tena. Utaisahau aibu ya ujana wako, wala hutaikumbuka tena fedheha ya ujane wako. Muumba wako atakuwa mume wako; Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ndilo jina lake, Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; yeye aitwa ‘Mungu wa ulimwengu wote’. “Yerusalemu, Mwenyezi-Mungu amekuita tena wewe kama vile mke aliyeachwa na kuhuzunika, mke aliyeolewa akiwa kijana akaachwa. Mungu wako anasema: Nilikuacha kwa muda mfupi tu; kwa huruma nyingi, nitakurudisha. Kwa hasira nyingi nilikuficha uso wangu kwa kitambo, lakini kwa fadhili za milele nitakuonea huruma. Mimi Mwenyezi-Mungu Mkombozi wako, nimesema.
Isaya 54:4-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia masuto ya ujane wako hutayakumbuka tena. Kwa sababu Muumba wako ni mume wako; BWANA wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote. Maana BWANA amekuita kama mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni, kama mke wakati wa ujana, atupwapo, asema Mungu wako. Kwa kitambo kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakurudisha. Kwa ghadhabu ifurikayo nilikuficha uso wangu dakika moja; lakini kwa fadhili za milele nitakurehemu, asema BWANA, Mkombozi wako.
Isaya 54:4-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Usiogope, wewe hutaaibika. Usiogope aibu, wewe hutaaibishwa. Wewe utasahau aibu ya ujana wako, wala hutakumbuka tena mashutumu ya ujane wako. Kwa maana Muumba wako ndiye mume wako, BWANA Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ni Mkombozi wako, yeye anaitwa Mungu wa dunia yote. BWANA atakuita urudi kana kwamba ulikuwa mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni; kama mke aliyeolewa bado angali kijana na kukataliwa,” asema Mungu wako. “Kwa kitambo kidogo nilikuacha, lakini kwa huruma nyingi nitakurudisha. Katika ukali wa hasira nilikuficha uso wangu kwa kitambo, lakini kwa fadhili za milele nitakuwa na huruma juu yako,” asema BWANA Mkombozi wako.