Yakobo 5:13-20
Yakobo 5:13-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Je, pana mtu yeyote miongoni mwenu aliye na shida? Anapaswa kusali. Je, yuko mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa. Je, yuko mgonjwa kati yenu? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa, nao watamwombea na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Wakiomba kwa imani mgonjwa ataponyeshwa; Bwana atampatia nafuu, na dhambi alizotenda zitaondolewa. Basi, ungamanieni dhambi zenu, na ombeaneni, ili mpate kuponywa. Sala ya mtu mwema ina nguvu ya kutenda mengi. Elia alikuwa binadamu kama sisi. Aliomba kwa moyo mvua isinyeshe, nayo haikunyesha nchini kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. Kisha akaomba tena, mvua ikanyesha kutoka angani na nchi ikatoa mazao yake. Ndugu zangu, mmoja wenu akipotoka kuhusu ukweli, na mwingine akamrudisha, fahamuni kwamba, huyo anayemrudisha mwenye dhambi kutoka njia yake ya upotovu, ataiokoa roho yake kutoka kifo, na dhambi nyingi zitaondolewa.
Yakobo 5:13-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kuna mtu miongoni mwenu anayeteseka? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. Mtu wa kwenu amekuwa mgonjwa? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. Basi ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, ili mpate kuponywa. Sala yake mwenye haki ina nguvu nyingi, na hutenda mengi. Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia sawa na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake. Ndugu zangu, mtu yeyote miongoni mwenu akipotoka mbali na kweli, na kurejeshwa na mtu mwingine; jueni ya kuwa yeye amrejeshaye mwenye dhambi hadi akatoka katika njia ya upotevu, ataokoa roho ya mwenye dhambi kutoka mauti, na kufunika wingi wa dhambi.
Yakobo 5:13-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii. Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake. Ndugu zangu, ikiwa mtu wa kwenu amepotelea mbali na kweli, na mtu mwingine akamrejeza; jueni ya kuwa yeye amrejezaye mwenye dhambi hata atoke katika njia ya upotevu, ataokoa roho na mauti, na kufunika wingi wa dhambi.
Yakobo 5:13-20 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Je, mtu yeyote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna yeyote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu. Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kundi la waumini wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana Isa. Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana Isa atamwinua, na kama ametenda dhambi, atasamehewa. Kwa hiyo, ungamianeni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu, tena yanafaa sana. Ilya alikuwa mwanadamu kama sisi. Aliomba kwa bidii kwamba mvua isinyeshe, nayo haikunyesha juu ya nchi kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. Kisha akaomba tena, nazo mbingu zikatoa mvua, nayo ardhi ikatoa mazao yake. Ndugu zangu, yeyote miongoni mwenu akipotoka na kuicha kweli, naye akarejeshwa na mtu mwingine, hamna budi kujua kwamba yeyote amrejeshaye mwenye dhambi kutoka upotovu wake, ataiokoa roho ya huyo mwenye dhambi kutoka mauti na kufunika wingi wa dhambi.