Yeremia 29:11-14
Yeremia 29:11-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Maana, mimi Mwenyezi-Mungu ninajua mambo niliyowapangia. Nimewapangieni mema na si mabaya, ili mpate kuwa na tumaini la baadaye. Hapo ndipo mtakaponiita na kuniomba, nami nitawasikiliza. Mtanitafuta na kunipata. Mtakaponitafuta kwa moyo wote mtanipata. Nami nitawarudishieni fanaka zenu na kuwakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipowafukuzia. Nitawarudisheni mahali ambapo niliwatoa, nikawapeleka uhamishoni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
Yeremia 29:11-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za baadaye. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. Nami nitaonekana kwenu, asema BWANA, nami nitawarudisha watu wenu waliofungwa, nami nitawakusanya ninyi, nikiwatoa katika mataifa yote, na katika mahali pote, nilikowafukuza, asema BWANA; nami nitawaleta tena, hadi mahali ambapo kutoka hapo niliwafanya mchukuliwe mateka.
Yeremia 29:11-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. Nami nitaonekana kwenu, asema BWANA, nami nitawarudisha watu wenu waliofungwa, nami nitawakusanya ninyi, nikiwatoa katika mataifa yote, na katika mahali pote, nilikowafukuza, asema BWANA; nami nitawaleta tena, hata mahali ambapo kutoka hapo naliwafanya mchukuliwe mateka.
Yeremia 29:11-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema BWANA, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. Nitaonekana kwenu,” asema BWANA, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali ambapo nilikuwa nimewatoa walipochukuliwa uhamishoni,” asema BWANA.