Yohane 12:1-11
Yohane 12:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alifika Bethania alikoishi Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua kutoka wafu. Huko walimwandalia chakula cha jioni, naye Martha akawa anawatumikia. Lazaro alikuwa mmoja wa wale waliokuwa mezani pamoja na Yesu. Basi, Maria alichukua nusu lita ya marashi ya nardo safi ya thamani kubwa, akampaka Yesu miguu na kuipangusa kwa nywele zake. Nyumba yote ikajaa harufu ya marashi. Basi, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema, “Kwa nini marashi hayo hayakuuzwa kwa fedha dinari 300, wakapewa maskini?” Alisema hivyo, si kwa kuwa alijali chochote juu ya maskini, bali kwa sababu alikuwa mweka hazina, na kwa kuwa alikuwa mwizi, mara kwa mara aliiba kutoka katika hiyo hazina. Lakini Yesu akasema, “Msimsumbue huyu mama! Mwacheni ayaweke kwa ajili ya siku ya mazishi yangu. Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini hamtakuwa nami siku zote.” Wayahudi wengi walisikia kwamba Yesu alikuwa Bethania. Basi, wakafika huko si tu kwa ajili ya kumwona Yesu, ila pia wapate kumwona Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka kwa wafu. Makuhani wakuu waliamua pia kumwua Lazaro, maana kwa sababu ya Lazaro Wayahudi wengi waliwaasi viongozi wao, wakamwamini Yesu.
Yohane 12:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alifika Bethania, alipokuwapo Lazaro, yeye ambaye Yesu alimfufua katika wafu. Basi wakamwandalia karamu huko; naye Martha akatumikia; na Lazaro alikuwa mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye. Basi Mariamu akatwaa ratili ya marhamu ya nardo safi yenye thamani nyingi, akampaka Yesu miguu, akamfuta miguu kwa nywele zake. Nayo nyumba pia ikajaa harufu ya marhamu. Basi Yuda Iskarioti, mmojawapo wa wanafunzi wake, ambaye ndiye atakaye kumsaliti, akasema, Mbona marhamu hii haikuuzwa kwa dinari mia tatu, wakapewa maskini? Naye aliyasema hayo, si kwa kuwahurumia maskini; bali kwa kuwa ni mwizi, naye ndiye aliyeshika mfuko, akavichukua vilivyotiwa humo. Basi Yesu alisema, Mwache aiweke kwa siku ya maziko yangu. Kwa maana maskini mnao sikuzote pamoja nanyi; bali mimi hamko nami sikuzote. Basi watu wengi katika Wayahudi walipata kujua ya kuwa yeye yuko huko, nao wakaja, si kwa ajili yake Yesu tu, ila wamwone na Lazaro, ambaye Yesu alimfufua katika wafu. Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri la kumwua Lazaro naye; maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walijitenga, wakamwamini Yesu.
Yohane 12:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alifika Bethania, alipokuwapo Lazaro, yeye ambaye Yesu alimfufua katika wafu. Basi wakamwandalia karamu huko; naye Martha akatumikia; na Lazaro alikuwa mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye. Basi Mariamu akatwaa ratli ya marhamu ya nardo safi yenye thamani nyingi, akampaka Yesu miguu, akamfuta miguu kwa nywele zake. Nayo nyumba pia ikajaa harufu ya marhamu. Basi Yuda Iskariote, mmojawapo wa wanafunzi wake, ambaye ndiye atakaye kumsaliti, akasema, Mbona marhamu hii haikuuzwa kwa dinari mia tatu, wakapewa maskini? Naye aliyasema hayo, si kwa kuwahurumia maskini; bali kwa kuwa ni mwivi, naye ndiye aliyeshika mfuko, akavichukua vilivyotiwa humo. Basi Yesu alisema, Mwache aiweke kwa siku ya maziko yangu. Kwa maana maskini mnao sikuzote pamoja nanyi; bali mimi hamnami sikuzote. Basi watu wengi katika Wayahudi walipata kujua ya kuwa yeye yuko huko, nao wakaja, si kwa ajili yake Yesu tu, ila wamwone na Lazaro, ambaye Yesu alimfufua katika wafu. Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri la kumwua Lazaro naye; maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walijitenga, wakamwamini Yesu.
Yohane 12:1-11 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Siku sita kabla ya Pasaka, Isa alienda Bethania, makao ya Lazaro, aliyekuwa amemfufua kutoka kwa wafu. Wakaandaa karamu kwa heshima ya Isa. Martha akawahudumia, wakati Lazaro alikuwa miongoni mwa waliokaa mezani pamoja na Isa. Kisha Mariamu akachukua chupa ya painti moja yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa, akayamimina miguuni mwa Isa na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato. Ndipo Yuda Iskariote mwana wa Simoni, mmoja wa wanafunzi wa Isa, ambaye baadaye angemsaliti Isa, akasema, “Kwa nini manukato haya hayakuuzwa kwa dinari mia tatu, na fedha hizo wakapewa maskini?” Yuda hakusema hivi kwa kuwa aliwajali maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwizi; ndiye alikuwa akitunza mfuko wa fedha, na akawa akiiba zile fedha. Isa akasema, “Mwacheni. Aliyanunua manukato hayo ili ayaweke kwa ajili ya siku ya maziko yangu. Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.” Umati mkubwa wa Wayahudi walipojua kwamba Isa alikuwa huko Bethania, walikuja si tu kwa ajili ya Isa, lakini pia kumwona Lazaro ambaye Isa alikuwa amemfufua. Kwa hiyo viongozi wa makuhani wakapanga njama ya kumuua Lazaro pia, kwa kuwa kutokana na habari za kufufuliwa kwake, Wayahudi wengi walikuwa wanamfuata Isa na kumwamini.