Yohane 12:37-50
Yohane 12:37-50 Biblia Habari Njema (BHN)
Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini. Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia: “Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu? Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?” Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya alisema tena: “Mungu ameyapofusha macho yao, amezipumbaza akili zao; wasione kwa macho yao, wasielewe kwa akili zao; wala wasinigeukie, asema Bwana, ili nipate kuwaponya.” Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa Yesu, akasema habari zake. Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini Yesu. Lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba watatengwa na sunagogi. Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu. Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, “Mtu anayeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma. Anayeniona mimi anamwona pia yule aliyenituma. Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani. Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki, mimi sitamhukumu; maana sikuja kuuhukumu ulimwengu bali kuuokoa. Asiyeyashika maneno yangu anaye wa kumhukumu: Neno lile nililosema ni hakimu wake siku ya mwisho. Mimi sikunena kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila Baba aliyenituma ndiye aliyeniamuru niseme nini na niongee nini. Nami najua kuwa amri yake huleta uhai wa milele. Basi, mimi nasema tu yale Baba aliyoniagiza niyaseme.”
Yohane 12:37-50 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini ingawa amefanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, hawakumwamini; ili litimie lile neno la nabii Isaya alilolisema, Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu; Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Ndiyo sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena, Amewapofusha macho, Ameifanya mizito mioyo yao; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakafahamu kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Maneno hayo aliyasema Isaya, kwa kuwa aliuona utukufu wake, akataja habari zake. Lakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi. Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu. Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenituma. Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenituma. Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani. Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho. Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenituma, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.
Yohane 12:37-50 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Walakini ajapokuwa amefanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, hawakumwamini; ili litimie lile neno la nabii Isaya alilolisema, Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu; Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Ndiyo sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena, Amewapofusha macho, Ameifanya mizito mioyo yao; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakafahamu kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Maneno hayo aliyasema Isaya, kwa kuwa aliuona utukufu wake, akataja habari zake. Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi. Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu. Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka. Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka. Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani. Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho. Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.
Yohane 12:37-50 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Hata baada ya Isa kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini. Hili lilikuwa ili kutimiza lile neno la nabii Isaya lililosema: “Mwenyezi Mungu, ni nani aliyeamini ujumbe wetu, na mkono wa Mwenyezi Mungu umefunuliwa kwa nani?” Kwa hivyo hawakuamini, kwa sababu Isaya anasema mahali pengine: “Amewafanya vipofu, na kuifanya mioyo yao kuwa migumu, ili wasiweze kuona kwa macho yao, wala kuelewa kwa mioyo yao, wasije wakageuka nami nikawaponya.” Isaya alisema haya alipoona utukufu wa Isa na kunena habari zake. Lakini wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi walimwamini, lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakukiri waziwazi kwa maana waliogopa kufukuzwa katika masinagogi. Wao walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zinazotoka kwa Mungu. Isa akapaza sauti akasema, “Yeyote aniaminiye, haniamini mimi peke yangu, bali pia yeye aliyenituma. Yeyote anionaye mimi amemwona yeye aliyenituma. Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni, ili kila mtu aniaminiye asibaki gizani. “Mimi simhukumu mtu yeyote anayesikia maneno yangu na asiyatii, kwa maana sikuja kuuhukumu ulimwengu, bali kuuokoa. Yuko anayehukumu yule anayenikataa mimi na kuyakataa maneno yangu; yale maneno niliyoyasema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho. Kwa maana sisemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba aliyenituma aliniamuru ni nini cha kusema na jinsi ya kukisema. Nami ninajua amri zake huongoza hadi kwenye uzima wa milele. Hivyo lolote nisemalo, ndilo lile Baba aliloniambia niseme.”