Yohane 13:1-17
Yohane 13:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Ilikuwa siku kabla ya sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua kwamba saa yake ya kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ilikuwa imefika. Alikuwa amewapenda daima watu wake walioko duniani; naam, aliwapenda mpaka mwisho! Basi, Yesu na wanafunzi wake walikuwa wamekaa kula chakula cha jioni. Ibilisi alikwisha mtia Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti, nia ya kumsaliti Yesu. Yesu alijua kwamba Baba alikuwa amemkabidhi kila kitu, na kwamba alikuwa ametoka kwa Mungu na anarudi kwa Mungu. Basi, aliondoka mezani, akaweka kando vazi lake, akachukua kitambaa na kujifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuipangusa kwa kile kitambaa alichojifungia. Basi, akamfikia Simoni Petro; naye Petro akasema, “Bwana, wewe utaniosha miguu mimi?” Yesu akamjibu, “Huelewi sasa ninachofanya lakini utaelewa baadaye.” Petro akamwambia, “Wewe hutaniosha miguu kamwe!” Yesu akamjibu, “Nisipokuosha hutakuwa na uhusiano nami tena.” Simoni Petro akamjibu, “Bwana, nioshe, si miguu tu, bali na mikono yangu na kichwa pia.” Yesu akamwambia, “Aliyekwisha oga hana lazima ya kunawa isipokuwa miguu, maana amekwisha takata mwili wote. Nyinyi mmetakata, lakini si nyote.” ( Yesu alimjua yule ambaye atamsaliti, ndiyo maana alisema: “Nyinyi mmetakata, lakini si nyote.”) Alipokwisha waosha miguu na kuvaa tena vazi lake, aliketi mezani, akawaambia, “Je, mmeelewa hayo niliyowatendeeni? Nyinyi mwaniita Mwalimu na Bwana, nanyi mwasema vyema, kwa kuwa ndimi. Basi, ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu nimewaosha nyinyi miguu, nanyi pia mnapaswa kuoshana miguu. Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama nilivyowafanyieni. Kweli nawaambieni, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala mtume si mkuu kuliko yule aliyemtuma. Basi, ikiwa mwayajua hayo, mtakuwa na heri mkiyatekeleza.
Yohane 13:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, huku akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye akiwa amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo. Hata wakati wa chakula cha jioni; naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti, moyo wa kumsaliti; Yesu, huku akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. Akamfikia Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe waniosha miguu mimi? Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. Petro akamwambia, Wewe hutaniosha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Nisipokuosha, huna shirika nami. Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia. Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga mwili hana haja ila ya kuosha miguu, maana yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote. Kwa maana alimjua yeye atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, Si nyote mlio safi. Basi alipokwisha kuwaosha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa hayo niliyowatendea? Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewaosha miguu, imewapasa ninyi pia kuoshana miguu ninyi kwa ninyi. Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo. Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyemtuma. Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda.
Yohane 13:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo. Hata wakati wa chakula cha jioni; naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskariote, moyo wa kumsaliti; Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi? Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika nami. Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia. Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya kutawadha miguu, bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote. Kwa maana alimjua yeye atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, Si nyote mlio safi. Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea? Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi. Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo. Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka. Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda.
Yohane 13:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ilikuwa mara tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua ya kuwa wakati wake wa kuondoka ulimwenguni ili kurudi kwa Baba umewadia. Alikuwa amewapenda watu wake waliokuwa ulimwenguni, naam, aliwapenda hadi kipimo cha mwisho. Wakati alipokuwa akila chakula cha jioni na wanafunzi wake, ibilisi alikuwa amekwisha kutia ndani ya moyo wa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni, wazo la kumsaliti Yesu. Yesu akijua ya kwamba Baba ameweka vitu vyote chini ya mamlaka yake na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu, hivyo aliondoka chakulani, akavua vazi lake la nje, akajifunga kitambaa kiunoni. Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni. Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, je, wewe utaninawisha mimi miguu?” Yesu akamjibu, “Hivi sasa hutambui lile ninalofanya, lakini baadaye utaelewa.” Petro akamwambia, “La, wewe hutaninawisha miguu kamwe.” Yesu akamjibu, “Kama nisipokunawisha, wewe huna sehemu nami.” Ndipo Simoni Petro akajibu, “Usininawishe miguu peke yake, Bwana, bali pamoja na mikono na kichwa pia!” Yesu akamjibu, “Mtu aliyekwisha kuoga anahitaji kunawa miguu tu, kwani mwili wake wote ni safi. Ninyi ni safi, ingawa si kila mmoja wenu.” Kwa kuwa yeye alijua ni nani ambaye angemsaliti, ndiyo sababu akasema si kila mmoja aliyekuwa safi. Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi, akawauliza, “Je, mmeelewa nililowafanyia? Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana,’ hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo. Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi. Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi. Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala aliyetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma. Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri yenu ninyi kama mkiyatenda.