Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 13:18-30

Yohane 13:18-30 Biblia Habari Njema (BHN)

“Haya nisemayo hayawahusu nyinyi nyote. Mimi nawajua wale niliowachagua. Lakini lazima yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: ‘Yule aliyeshiriki chakula changu amegeuka kunishambulia.’ Mimi nimewaambieni mambo haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini kuwa ‘Mimi Ndimi.’ Kweli nawaambieni: Anayempokea yule ninayemtuma ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma.” Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni, akasema wazi, “Kweli nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!” Wanafunzi wakatazamana wasiweze kabisa kujua anamsema nani. Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana, alikuwa ameketi karibu na Yesu. Basi, Simoni Petro akamwashiria na kusema: “Mwulize anasema juu ya nani.” Mwanafunzi huyo akasogea karibu zaidi na Yesu, akamwuliza, “Bwana, ni nani?” Yesu akajibu, “Yule nitakayempa kipande cha mkate nilichochovya katika sahani, ndiye.” Basi, akatwaa kipande cha mkate, akakichovya katika sahani, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti. Yuda alipokwisha pokea kipande hicho, Shetani akamwingia. Basi Yesu akamwambia, “Unachotaka kufanya, kifanye haraka!” Lakini hakuna hata mmoja wa wale waliokaa pale mezani aliyefahamu kwa nini alikuwa amemwambia hivyo. Kwa kuwa Yuda alikuwa mweka hazina, baadhi yao walidhani kwamba Yesu alikuwa amemwambia anunue vilivyohitajiwa kwa sikukuu, au kwamba alikuwa amemwambia akatoe chochote kwa maskini. Basi, Yuda alipokwisha twaa kile kipande cha mkate, akatoka nje mara. Na ilikuwa usiku.

Shirikisha
Soma Yohane 13

Yohane 13:18-30 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

“Sisemi hivi kuhusu ninyi nyote. Ninawajua wale niliowachagua. Lakini ni kutimiza andiko lisemalo, ‘Yeye aliyekula chakula changu ameinua kisigino chake dhidi yangu.’ “Ninawaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa Mimi ndiye. Amin, amin nawaambia, yeyote anayempokea yule niliyemtuma anipokea mimi, naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenituma mimi.” Baada ya kusema haya, Isa alifadhaika sana moyoni, akasema, “Amin, amin nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.” Wanafunzi wake wakatazamana bila kujua kuwa alikuwa anamsema nani. Mmoja wa wanafunzi wake, ambaye Isa alimpenda sana, alikuwa ameegama kifuani mwa Isa. Simoni Petro akampungia mkono yule mwanafunzi, akamwambia, “Muulize anamaanisha nani.” Yule mwanafunzi akamwegemea Isa, akamuuliza, “Bwana, tuambie, ni nani?” Isa akajibu, “Ni yule nitakayempa hiki kipande cha mkate baada ya kukichovya kwenye bakuli.” Hivyo baada ya kukichovya kile kipande cha mkate, akampa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni. Mara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, Shetani akamwingia. Isa akamwambia Yuda, “Lile unalotaka kulitenda, litende haraka.” Hakuna hata mmoja wa wale waliokuwa wameketi naye mezani aliyeelewa kwa nini Isa alimwambia hivyo. Kwa kuwa Yuda alikuwa mtunza fedha, wengine walifikiri Isa alikuwa anamwambia akanunue vitu vilivyohitajika kwa ajili ya Sikukuu, au kuwapa maskini kitu. Mara tu baada ya kupokea ule mkate, Yuda akatoka nje. Wakati huo ulikuwa ni usiku.

Shirikisha
Soma Yohane 13