Yohane 13:21-30
Yohane 13:21-30 Biblia Habari Njema (BHN)
Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni, akasema wazi, “Kweli nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!” Wanafunzi wakatazamana wasiweze kabisa kujua anamsema nani. Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana, alikuwa ameketi karibu na Yesu. Basi, Simoni Petro akamwashiria na kusema: “Mwulize anasema juu ya nani.” Mwanafunzi huyo akasogea karibu zaidi na Yesu, akamwuliza, “Bwana, ni nani?” Yesu akajibu, “Yule nitakayempa kipande cha mkate nilichochovya katika sahani, ndiye.” Basi, akatwaa kipande cha mkate, akakichovya katika sahani, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti. Yuda alipokwisha pokea kipande hicho, Shetani akamwingia. Basi Yesu akamwambia, “Unachotaka kufanya, kifanye haraka!” Lakini hakuna hata mmoja wa wale waliokaa pale mezani aliyefahamu kwa nini alikuwa amemwambia hivyo. Kwa kuwa Yuda alikuwa mweka hazina, baadhi yao walidhani kwamba Yesu alikuwa amemwambia anunue vilivyohitajiwa kwa sikukuu, au kwamba alikuwa amemwambia akatoe chochote kwa maskini. Basi, Yuda alipokwisha twaa kile kipande cha mkate, akatoka nje mara. Na ilikuwa usiku.
Yohane 13:21-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye alipokwisha kusema hayo, Yesu alifadhaika rohoni, akashuhudia akisema, Amin, amin, nawaambieni, Mmoja wenu atanisaliti. Wanafunzi wakatazamana, huku wakiwa na mashaka ni nani amnenaye. Na palikuwapo mmoja wa wanafunzi wake, ameegama kifuani pa Yesu, ambaye Yesu alimpenda. Basi Simoni Petro akampungia mkono, akamwambia, Uliza, ni nani amtajaye? Basi yeye, huku akimwelekea Yesu kifua chake, akamwambia, Bwana, ni nani? Basi Yesu akajibu, Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa. Akatowelea tonge, akalitwaa akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti. Na baada ya hilo tonge Shetani alimwingia. Basi Yesu akamwambia, Uyatendayo yatende upesi. Wala hakuna mtu katika wale walioketi chakulani aliyeijua sababu ya kumwambia hivyo. Kwa maana wengine walidhania, kwa kuwa Yuda huchukua mfuko, ya kwamba Yesu alimwambia kama, Nunua mnavyovihitaji kwa sikukuu; au kwamba awape maskini kitu. Basi huyo, akiisha kulipokea lile tonge, akatoka mara hiyo. Nako kulikuwa ni usiku.
Yohane 13:21-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye alipokwisha kusema hayo, Yesu alifadhaika rohoni, akashuhudia akisema, Amin, amin, nawaambieni, Mmoja wenu atanisaliti. Wanafunzi wakatazamana, huku wakiona shaka ni nani amtajaye. Na palikuwapo mmoja wa wanafunzi wake, ameegama kifuani pa Yesu, ambaye Yesu alimpenda. Basi Simoni Petro akampungia mkono, akamwambia, Uliza, ni nani amtajaye? Basi yeye, hali akimwelekea Yesu kifua chake, akamwambia, Bwana, ni nani? Basi Yesu akajibu, Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa. Akatowelea tonge, akalitwaa akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Na baada ya hilo tonge Shetani alimwingia. Basi Yesu akamwambia, Uyatendayo yatende upesi. Wala hakuna mtu katika wale walioketi chakulani aliyeijua sababu ya kumwambia hivyo. Kwa maana wengine walidhania, kwa kuwa Yuda huchukua mfuko, ya kwamba Yesu alimwambia kama, Nunua mnavyovihitaji kwa sikukuu; au kwamba awape maskini kitu. Basi huyo, akiisha kulipokea lile tonge, akatoka mara hiyo. Nako kulikuwa ni usiku.
Yohane 13:21-30 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Baada ya kusema haya, Isa alifadhaika sana moyoni, akasema, “Amin, amin nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.” Wanafunzi wake wakatazamana bila kujua kuwa alikuwa anamsema nani. Mmoja wa wanafunzi wake, ambaye Isa alimpenda sana, alikuwa ameegama kifuani mwa Isa. Simoni Petro akampungia mkono yule mwanafunzi, akamwambia, “Muulize anamaanisha nani.” Yule mwanafunzi akamwegemea Isa, akamuuliza, “Bwana, tuambie, ni nani?” Isa akajibu, “Ni yule nitakayempa hiki kipande cha mkate baada ya kukichovya kwenye bakuli.” Hivyo baada ya kukichovya kile kipande cha mkate, akampa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni. Mara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, Shetani akamwingia. Isa akamwambia Yuda, “Lile unalotaka kulitenda, litende haraka.” Hakuna hata mmoja wa wale waliokuwa wameketi naye mezani aliyeelewa kwa nini Isa alimwambia hivyo. Kwa kuwa Yuda alikuwa mtunza fedha, wengine walifikiri Isa alikuwa anamwambia akanunue vitu vilivyohitajika kwa ajili ya Sikukuu, au kuwapa maskini kitu. Mara tu baada ya kupokea ule mkate, Yuda akatoka nje. Wakati huo ulikuwa ni usiku.