Yohane 14:1-11
Yohane 14:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu aliwaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama isingekuwa hivyo, ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi. Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na kuwachukueni kwangu, ili nanyi muwe pale nilipo mimi. Mnajua njia ya kwenda huko ninakokwenda.” Thoma akamwuliza, “Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje basi, kuijua hiyo njia?” Yesu akamjibu, “Mimi ni njia, na ukweli na uhai. Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu. Ikiwa mnanijua mimi, mnamjua na Baba yangu pia. Na tangu sasa, mnamjua, tena mmekwisha mwona.” Filipo akamwambia, “Bwana, tuoneshe Baba, nasi tutatosheka.” Yesu akamwambia, “Nimekaa nanyi muda wote huu, nawe Filipo hujanijua? Aliyekwisha niona mimi amemwona Baba. Unawezaje basi, kusema: ‘Tuoneshe Baba?’ Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambieni siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba aliye ndani yangu anafanya kazi yake. Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya Baba naye Baba yuko ndani yangu. Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo ninayofanya.
Yohane 14:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi muwepo. Nami niendako mwaijua njia. Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi tunaijuaje njia? Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuoneshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuoneshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe.
Yohane 14:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. Nami niendako mwaijua njia. Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia? Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe.
Yohane 14:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Naenda kuwaandalia makao. Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo. Ninyi mnajua njia ya kufika ninakokwenda.” Tomaso akamwambia, “Bwana, sisi hatujui unakokwenda, tutaijuaje njia?” Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba pia. Tangu sasa, mnamjua Baba yangu, tena mmemwona.” Filipo akamwambia, “Bwana, tuonyeshe Baba yako yatosha.” Yesu akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu yeyote aliyeniona mimi, amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuonyeshe Baba’? Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi. Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba na Baba yuko ndani yangu, la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo.