Yohane 15:18-27
Yohane 15:18-27 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kama ulimwengu ukiwachukia nyinyi, kumbukeni kwamba umenichukia mimi kabla ya kuwachukia nyinyi. Kama mngalikuwa watu wa ulimwengu, ulimwengu ungaliwapenda nyinyi kama watu wake. Lakini kwa vile nyinyi si wa ulimwengu, ila mimi nimewachagueni kutoka ulimwenguni, kwa sababu hiyo ulimwengu unawachukieni. Kumbukeni niliyowaambieni: Mtumishi si mkuu kuliko bwana wake. Ikiwa wamenitesa mimi, watawatesa na nyinyi pia; kama wameshika neno langu, watalishika na lenu pia. Lakini hayo yote watawatendeeni nyinyi kwa sababu ya jina langu, kwani hawamjui yeye aliyenituma. Kama nisingalikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia; lakini sasa hawawezi kujitetea kwamba hawana dhambi. Anayenichukia mimi, anamchukia na Baba yangu pia. Kama nisingalifanya kwao mambo ambayo hakuna mtu mwingine amekwisha yafanya wasingalikuwa na hatia; lakini sasa wameona niliyoyafanya wakanichukia mimi, wakamchukia na Baba yangu pia. Ndiyo maana yale yaliyoandikwa katika sheria yao ni kweli: ‘Wamenichukia bure!’ “Atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, huyo Roho wa ukweli, atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. Nanyi pia mtanishuhudia kwa kuwa mmekuwa nami tangu mwanzo.
Yohane 15:18-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi niliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenituma. Kama nisingalikuja na kusema nao, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa hawana kisingizio kwa dhambi yao. Yeye anichukiaye mimi humchukia na Baba yangu. Kama nisingalitenda kwao kazi asizozitenda mtu mwingine, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa wametuona mimi na Baba yangu, na kutuchukia. Lakini litimie lile neno lililoandikwa katika torati yao, Walinichukia bure. Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia. Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami.
Yohane 15:18-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka. Kama nisingalikuja na kusema nao, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa hawana udhuru kwa dhambi yao. Yeye anichukiaye mimi humchukia na Baba yangu. Kama nisingalitenda kwao kazi asizozitenda mtu mwingine, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa wametuona mimi na Baba yangu, na kutuchukia. Lakini litimie lile neno lililoandikwa katika torati yao, Walinichukia bure. Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia. Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami.
Yohane 15:18-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba ulinichukia mimi kabla yenu. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungeliwapenda kama vile unavyowapenda walio wake. Kwa sababu ninyi si wa ulimwengu, lakini mimi nimewachagua kutoka ulimwengu, hii ndiyo sababu ulimwengu unawachukia. Kumbukeni lile neno nililowaambia, ‘Hakuna mtumishi aliye mkuu kuliko bwana wake.’ Kama wamenitesa mimi, nanyi pia watawatesa. Kama wamelishika neno langu, watalishika na neno lenu pia. Watawatendea ninyi haya yote kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu hawamjui yeye aliyenituma. Kama sikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa hawana udhuru kwa ajili ya dhambi zao. Yeyote anayenichukia mimi, anamchukia pia na Baba yangu. Kama sikuwa nimefanya miujiza ambayo haijapata kufanywa na mtu mwingine yeyote, wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa wameiona miujiza hii na bado wakatuchukia mimi na Baba yangu. Lakini hii ni kutimiza lile neno lililoandikwa kwenye Sheria kwamba, ‘Walinichukia pasipo sababu.’ “Lakini atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, yaani, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. Ninyi nanyi itawapasa kushuhudia kwa sababu mmekuwa pamoja nami tangu mwanzo.