Yohane 17:1-26
Yohane 17:1-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maneno hayo aliyasema Yesu; akainua macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe; kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma. Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye. Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako. Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika. Sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka kwako. Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao; nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao. Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie. Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli. Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi. Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu. Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma. Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.
Yohane 17:1-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alipokwisha sema hayo, alitazama juu mbinguni, akasema, “Baba, ile saa imefika! Mtukuze Mwanao ili naye Mwana apate kukutukuza. Maana ulimpa Mwanao mamlaka juu ya watu wote ili awape uhai wa milele wote hao uliompa. Na uhai wa milele ndio huu: Kukujua wewe uliye peke yako Mungu wa kweli, na kumjua Yesu Kristo uliyemtuma. Mimi nimekutukuza hapa duniani; nimeikamilisha ile kazi uliyonipa niifanye. Sasa, Baba, nitukuze mbele yako kwa ule utukufu niliokuwa nao kabla ya kuumbwa ulimwengu. “Nimekufanya ujulikane kwa watu wale ulionipa kutoka duniani. Walikuwa watu wako, nawe ukanipa wawe wangu; nao wamelishika neno lako. Sasa wanajua kwamba kila ulichonipa kimetoka kwako. Mimi nimewapa ule ujumbe ulionipa, nao wameupokea; wanajua kwamba kweli nimetoka kwako, na wanaamini kwamba wewe ulinituma. “Nawaombea hao; siuombei ulimwengu, ila nawaombea wale ulionipa, maana ni wako. Yote niliyo nayo ni yako, na yako ni yangu; na utukufu wangu umeonekana katika hao ulionipa. Na sasa naja kwako; simo tena ulimwenguni, lakini wao wamo ulimwenguni. Baba Mtakatifu! Kwa nguvu ya jina lako ulilonipa, tafadhali uwaweke salama ili wawe kitu kimoja kama sisi tulivyo mmoja. Nilipokuwa nao, mimi niliwaweka salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa. Mimi nimewalinda, wala hakuna hata mmoja wao aliyepotea, isipokuwa yule mwana mpotevu, ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia. Basi, sasa naja kwako, na nimesema mambo haya ulimwenguni, ili waweze kushiriki kikamilifu furaha yangu. Mimi nimewapa ujumbe wako, nao ulimwengu ukawachukia, kwa sababu wao si wa ulimwengu, kama vile nami nisivyo wa ulimwengu. Siombi uwatoe ulimwenguni, bali naomba uwakinge na yule Mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama vile nami nisivyo wa ulimwengu. Waweke wakfu katika ukweli; neno lako ni ukweli. Kama vile ulivyonituma ulimwenguni, nami pia nimewatuma wao ulimwenguni; na kwa ajili yao mimi mwenyewe najiweka wakfu ili nao pia wafanywe wakfu katika ukweli. “Siwaombei hao tu, bali nawaombea pia wote watakaoamini kutokana na ujumbe wao. Naomba ili wote wawe kitu kimoja. Baba! Naomba wawe ndani yetu kama vile wewe ulivyo ndani yangu nami ndani yako. Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma. Mimi nimewapa utukufu uleule ulionipa mimi, ili wawe kitu kimoja kama nasi tulivyo mmoja; mimi niwe ndani yao, nawe uwe ndani yangu; naomba wakamilishwe na kuwa kitu kimoja, ili ulimwengu upate kujua kwamba wewe ulinituma, na kwamba unawapenda wao kama unavyonipenda mimi. “Baba! Nataka hao ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili wauone utukufu wangu ulionipa; kwa kuwa ulinipenda kabla ya kuumbwa ulimwengu. Baba Mwema! Ulimwengu haukujui, lakini mimi nakujua. Hawa nao wanajua kwamba wewe ulinituma. Nimekufanya ujulikane kwao na nitaendelea kufanya hivyo, ili upendo ulio nao kwangu uwe ndani yao, nami niwe ndani yao.”
Yohane 17:1-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maneno hayo aliyasema Yesu; akainua macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe; kama vile ulivyompa mamlaka juu ya watu wote, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma. Mimi nimekutukuza duniani, nikiwa nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye. Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako. Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika. Sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka kwako. Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao; nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nilitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao. Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi niliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie. Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo niliwatuma hao ulimwenguni. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli. Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi. Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu. Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nilikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma. Nami niliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.
Yohane 17:1-26 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya Yesu kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema: “Baba, saa imewadia. Umtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe. Kwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa. Nao uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe uliye Mungu wa pekee, wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma. Nimekutukuza wewe duniani kwa kuitimiza ile kazi uliyonipa niifanye. Hivyo sasa, Baba, unitukuze mbele zako kwa ule utukufu niliokuwa nao pamoja na wewe kabla ulimwengu haujakuwepo. “Nimelidhihirisha jina lako kwa wale ulionipa kutoka ulimwengu. Walikuwa wako, nawe ukanipa mimi, nao wamelitii neno lako. Sasa wamejua ya kuwa vyote ulivyonipa vimetoka kwako, kwa kuwa maneno yale ulionipa nimewapa wao, nao wameyapokea na kujua kwamba kweli nimetoka kwako, nao wameamini kuwa wewe ulinituma. Ninawaombea wao. Mimi siuombei ulimwengu, bali nawaombea wale ulionipa kwa sababu wao ni wako. Wote walio wangu ni wako na walio wako ni wangu, nami nimetukuzwa ndani yao. Mimi sasa simo tena ulimwenguni, lakini wao bado wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba Mtakatifu, uwalinde kwa uweza wa jina lako ulilonipa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. Nilipokuwa pamoja nao, niliwalinda, wakawa salama kwa lile jina ulilonipa. Hakuna hata mmoja aliyepotea, isipokuwa yule aliyekusudiwa upotevu, ili Maandiko yapate kutimia. “Lakini sasa naja kwako, nami ninasema mambo haya wakati bado nikiwa ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu kamili ndani yao. Nimewapa neno lako, nao ulimwengu umewachukia kwa kuwa wao si wa ulimwengu kama mimi nisivyo wa ulimwengu huu. Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde dhidi ya yule mwovu. Wao si wa ulimwengu huu, kama vile mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndilo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nawatuma vivyo hivyo. Kwa ajili yao najiweka wakfu ili wao nao wapate kutakaswa katika ile kweli. “Siwaombei hawa peke yao, bali nawaombea na wale wote watakaoniamini kupitia neno lao ili wawe na umoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi nilivyo ndani yako, wao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiye uliyenituma mimi. Utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. Mimi ndani yako na wewe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma, nami nimewapenda wao kama unavyonipenda mimi. “Baba, shauku yangu ni kwamba, wale ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili waweze kuuona utukufu wangu, yaani, utukufu ule ulionipa kwa kuwa ulinipenda hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu. “Baba Mwenye Haki, ingawa ulimwengu haukujui, mimi ninakujua, nao wanajua ya kuwa umenituma. Nimefanya jina lako lijulikane kwao nami nitaendelea kufanya lijulikane, ili kwamba upendo ule unaonipenda mimi uwe ndani yao na mimi mwenyewe nipate kuwa ndani yao.”