Yohane 18:15-27
Yohane 18:15-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakamfuata Yesu, Petro na mwanafunzi mwingine. Na mwanafunzi huyo alikuwa amejulikana na Kuhani Mkuu, akaingia pamoja na Yesu katika behewa ya Kuhani Mkuu. Lakini Petro akasimama nje mlangoni. Basi yule mwanafunzi mwingine aliyejulikana na Kuhani Mkuu akatoka, akasema na mngoja mlango, akamleta Petro ndani. Basi yule kijakazi, aliyekuwa mngoja mlango, akamwambia Petro, Wewe nawe, je! Hu mwanafunzi mmojawapo wa mtu huyu? Naye akasema, Si mimi. Na wale watumwa na watumishi walikuwa wakisimama, wamefanya moto wa makaa; maana ilikuwa baridi; wakawa wakikota moto. Petro naye alikuwapo pamoja nao, anakota moto. Basi Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu habari za wanafunzi wake, na habari za mafundisho yake. Yesu akamjibu, Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; sikuzote nalifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lo lote. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena. Basi aliposema hayo, mtumishi mmojawapo aliyesimama karibu alimpiga Yesu kofi akisema, Wamjibu hivi Kuhani Mkuu? Yesu akamjibu, Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini? Basi Anasi akampeleka hali amefungwa kwa Kayafa, Kuhani Mkuu. Na Simoni Petro alikuwa akisimama huko, anakota moto. Basi wakamwambia, Wewe nawe, je! Hu mwanafunzi wake mmojawapo? Naye akakana, akasema, Si mimi. Mtumwa mmojawapo wa Kuhani Mkuu, naye ni jamaa yake yule aliyekatwa sikio na Petro, akasema, Je! Mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye? Basi Petro akakana tena, na mara akawika jimbi.
Yohane 18:15-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walimfuata Yesu. Huyo mwanafunzi mwingine alikuwa anajulikana kwa kuhani mkuu, hivyo aliingia pamoja na Yesu ndani ya ukumbi wa kuhani mkuu. Lakini Petro alikuwa amesimama nje, karibu na mlango. Basi, huyo mwanafunzi mwingine aliyekuwa anajulikana kwa kuhani mkuu alitoka nje akasema na mjakazi, mngojamlango, akamwingiza Petro ndani. Huyo mjakazi mngojamlango akamwuliza Petro, “Je, nawe pia ni mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?” Petro akamwambia, “Si mimi!” Watumishi na walinzi walikuwa wamewasha moto kwa sababu kulikuwa na baridi, wakawa wanaota moto. Naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto. Basi, kuhani mkuu akamwuliza Yesu juu ya wanafunzi wake na mafundisho yake. Yesu akamjibu, “Nimesema na kila mtu daima hadharani. Kila mara nimefundisha katika masunagogi na hekaluni, mahali wanapokutana Wayahudi wote; na wala sijasema chochote kwa siri. Kwa nini waniuliza mimi? Waulize wale waliosikia nini niliwaambia. Wao wanajua niliyowaambia.” Alipokwisha sema hayo mlinzi mmoja aliyekuwa amesimama hapo akampiga kofi akisema, “Je, ndivyo unavyomjibu kuhani mkuu?” Yesu akamjibu, “Kama nimesema vibaya, onesha huo ubaya; lakini ikiwa nimesema vema, mbona wanipiga?” Basi, Anasi akampeleka Yesu akiwa amefungwa, kwa kuhani mkuu Kayafa. Petro alikuwa hapo akiota moto. Basi, wakamwuliza, “Je, nawe pia si mmoja wa wanafunzi wake?” Yeye akakana na kusema, “Si mimi!” Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu, jamaa wa yule aliyekatwa sikio na Petro, akamwuliza, “Je, mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?” Petro akakana tena; mara jogoo akawika.
Yohane 18:15-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakamfuata Yesu, Petro na mwanafunzi mwingine. Na mwanafunzi huyo alikuwa amejulikana na Kuhani Mkuu, akaingia pamoja na Yesu katika ukumbi wa Kuhani Mkuu. Lakini Petro akasimama nje mlangoni. Basi yule mwanafunzi mwingine aliyejulikana na Kuhani Mkuu akatoka, akasema na mlinda mlango, akamleta Petro ndani. Basi yule kijakazi, aliyekuwa mlinda mlango, akamwambia Petro, Wewe nawe, je! Hu mwanafunzi mmojawapo wa mtu huyu? Naye akasema, Si mimi. Na wale watumwa na watumishi walikuwa wakisimama, wamewasha moto wa makaa; maana kulikuwa na baridi; wakawa wakiota moto. Petro naye alikuwapo pamoja nao, anaota moto. Basi Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu kuhusu wanafunzi wake, na kuhusu mafundisho yake. Yesu akamjibu, Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; sikuzote nilifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala mimi sikusema neno lolote kwa siri. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena. Basi aliposema hayo, mtumishi mmojawapo aliyesimama karibu alimpiga Yesu kofi akisema, Wamjibu hivi Kuhani Mkuu? Yesu akamjibu, Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini? Basi Anasi akampeleka akiwa amefungwa kwa Kayafa, Kuhani Mkuu. Na Simoni Petro alikuwa akisimama huko, anakota moto. Basi wakamwambia, Wewe nawe, je! Hu mwanafunzi wake mmojawapo? Naye akakana, akasema, Si mimi. Mtumwa mmojawapo wa Kuhani Mkuu, naye ni jamaa yake yule aliyekatwa sikio na Petro, akasema, Je! Mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye? Basi Petro akakana tena, na mara jogoo akawika.
Yohane 18:15-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walikuwa wakimfuata Yesu. Huyu mwanafunzi mwingine alikuwa anafahamika kwa kuhani mkuu, hivyo aliingia ndani ya ukumbi pamoja na Yesu. Lakini Petro alisimama nje karibu na lango, ndipo yule mwanafunzi mwingine, aliyejulikana na kuhani mkuu, akazungumza na msichana aliyekuwa analinda lango, akamruhusu Petro aingie ndani. Yule msichana akamuuliza Petro, “Je, wewe pia si mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?” Petro akajibu, “Sio mimi.” Wale watumishi na askari walikuwa wamesimama wakiota moto wa makaa kwa sababu palikuwa na baridi, Petro naye alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto. Wakati huo kuhani mkuu akawa anamuuliza Yesu kuhusu wanafunzi wake na mafundisho yake. Yesu akamjibu, “Nimekuwa nikizungumza waziwazi mbele ya watu wote. Siku zote nimefundisha katika masinagogi na Hekaluni, mahali ambapo Wayahudi wote hukusanyika. Sikusema jambo lolote kwa siri. Mbona unaniuliza mimi maswali? Waulize wale walionisikia yale niliyowaambia. Wao wanajua niliyosema.” Alipomaliza kusema hayo, mmoja wa askari aliyekuwa amesimama karibu naye, akampiga Yesu kofi usoni, kisha akasema, “Je, hivyo ndivyo unavyomjibu kuhani mkuu?” Yesu akamjibu akasema, “Kama nimesema jambo baya, shuhudia huo ubaya niliousema. Lakini kama nimesema yaliyo kweli, mbona umenipiga?” Ndipo Anasi akampeleka Yesu kwa kuhani mkuu Kayafa, akiwa bado amefungwa. Wakati huo Simoni Petro alikuwa amesimama akiota moto. Baadhi ya wale waliokuwepo wakamuuliza, “Je, wewe si mmoja wa wanafunzi wake?” Petro akakana, akasema, “Sio mimi.” Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu, ndugu yake yule mtu ambaye Petro alikuwa amemkata sikio, akamuuliza, “Je, mimi sikukuona kule bustanini ukiwa na Yesu?” Kwa mara nyingine tena Petro akakana, naye jogoo akawika wakati huo huo.