Yohane 19:12-19
Yohane 19:12-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Tangu hapo, Pilato akawa anatafuta njia ya kumwachilia, lakini Wayahudi wakapiga kelele: “Ukimwachilia huyu mtu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu anayejifanya kuwa mfalme humpinga Kaisari!” Basi, Pilato aliposikia maneno hayo akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo “Sakafu ya Mawe” (kwa Kiebrania, Gabatha). Ilikuwa yapata saa sita mchana, siku ya maandalio ya Pasaka. Pilato akawaambia Wayahudi, “Tazameni, Mfalme wenu!” Wao wakapaza sauti: “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!” Pilato akawauliza, “Je, nimsulubishe Mfalme wenu?” Makuhani wakuu wakajibu, “Sisi hatuna mfalme isipokuwa Kaisari!” Hapo, Pilato akamtia Yesu mikononi mwao ili asulubiwe. Basi, wakamchukua Yesu. Naye akatoka akiwa amejichukulia msalaba wake kwenda mahali paitwapo “Fuvu la Kichwa” (kwa Kiebrania Golgotha). Hapo ndipo walipomsulubisha, na pamoja naye waliwasulubisha watu wengine wawili; mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto, naye Yesu katikati. Pilato aliandika ilani akaiweka juu ya msalaba. Nayo ilikuwa imeandikwa hivi: “Yesu Mnazareti, Mfalme wa Wayahudi.”
Yohane 19:12-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua; lakini Wayahudi wakapiga makelele wakisema, Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari. Basi Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha. Nayo ilikuwa Maandalio ya pasaka, yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi, Tazama, Mfalme wenu! Basi wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Je! Nimsulibishe mfalme wenu! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme ila Kaisari. Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu. Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha. Wakamsulibisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati. Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI.
Yohane 19:12-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Tangu wakati huo, Pilato akajitahidi kutafuta njia ya kumfungua Yesu, lakini Wayahudi wakazidi kupiga kelele wakisema, “Ukimwachia huyu mtu, wewe si rafiki wa Kaisari. Mtu yeyote anayedai kuwa mfalme anampinga Kaisari.” Pilato aliposikia maneno haya akamtoa Yesu nje tena akaketi katika kiti chake cha hukumu, mahali palipoitwa Sakafu ya Jiwe, kwa Kiebrania paliitwa Gabatha Basi ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, yapata kama saa sita hivi. Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!” Wao wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!” Pilato akawauliza, “Je, nimsulubishe mfalme wenu?” Wale viongozi wa makuhani wakamjibu, “Sisi hatuna mfalme mwingine ila Kaisari.” Ndipo Pilato akamkabidhi Yesu kwao ili wamsulubishe. Kwa hiyo askari wakamchukua Yesu. Yesu, akiwa ameubeba msalaba wake, akatoka kuelekea mahali palipoitwa Fuvu la Kichwa (kwa Kiebrania ni Golgotha). Hapo ndipo walipomsulubisha. Pamoja naye walisulubisha watu wengine wawili, mmoja kila upande wake, naye Yesu katikati. Pilato akaamuru tangazo liandikwe na liwekwe juu kwenye msalaba wa Yesu, likasema: “YESU WA NAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI.”
Yohane 19:12-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua; lakini Wayahudi wakapiga makelele wakisema, Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari. Basi Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha. Nayo ilikuwa Maandalio ya Pasaka, yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi, Tazama, Mfalme wenu! Basi wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulubishe! Pilato akawaambia, Je! Nimsulubishe mfalme wenu! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme ila Kaisari. Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulubiwe; nao wakampokea Yesu. Akatoka, huku akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha. Wakamsulubisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati. Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI.