Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 19:16-30

Yohane 19:16-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Hapo, Pilato akamtia Yesu mikononi mwao ili asulubiwe. Basi, wakamchukua Yesu. Naye akatoka akiwa amejichukulia msalaba wake kwenda mahali paitwapo “Fuvu la Kichwa” (kwa Kiebrania Golgotha). Hapo ndipo walipomsulubisha, na pamoja naye waliwasulubisha watu wengine wawili; mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto, naye Yesu katikati. Pilato aliandika ilani akaiweka juu ya msalaba. Nayo ilikuwa imeandikwa hivi: “Yesu Mnazareti, Mfalme wa Wayahudi.” Wayahudi wengi waliisoma ilani hiyo, maana mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa karibu na mji. Tena ilani hiyo ilikuwa imeandikwa kwa Kiebrania, Kilatini, na Kigiriki. Basi, makuhani wakuu wakamwambia Pilato, “Usiandike: ‘Mfalme wa Wayahudi,’ ila ‘Yeye alisema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.’” Pilato akajibu, “Niliyoandika, nimeandika!” Askari walipokwisha msulubisha Yesu, walizichukua nguo zake, wakazigawa mafungu manne, fungu moja kwa kila askari. Walichukua pia na kanzu yake; kanzu hiyo ilikuwa imefumwa kwa kipande kimoja tu, bila mshono. Basi, hao askari wakashauriana: “Tusiipasue, ila tuipigie kura itakuwa ya nani.” Jambo hilo lilifanyika ili yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: “Waligawana mavazi yangu, na nguo yangu wakaipigia kura.” Basi, ndivyo walivyofanya hao askari. Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalene. Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake, “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao.” Halafu akamwambia yule mwanafunzi, “Tazama, huyo ndiye mama yako.” Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake. Kisha, Yesu aliona kwamba yote yalikuwa yametimia; na, ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia, akasema, “Naona kiu.” Hapo palikuwa na bakuli limejaa siki. Basi, wakachovya sifongo katika hiyo siki, wakaitia juu ya ufito wa husopo, wakamwekea mdomoni. Yesu alipokwisha pokea hiyo siki, akasema, “Yametimia!” Kisha akainamisha kichwa, akatoa roho.

Shirikisha
Soma Yohane 19

Yohane 19:16-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulubiwe; nao wakampokea Yesu. Akatoka, huku akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha. Wakamsulubisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati. Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI. Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale aliposulubiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa Kiebrania, na Kirumi, na Kigiriki. Basi wakuu wa makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato, Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi. Pilato akajibu, Niliyoandika nimeyaandika. Nao askari walipomsulubisha Yesu, waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu. Basi wakaambiana, Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani. Ili litimie andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, Na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari. Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake. Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu. Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani. Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.

Shirikisha
Soma Yohane 19

Yohane 19:16-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu. Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha. Wakamsulibisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati. Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI. Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale aliposulibiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa Kiebrania, na Kirumi, na Kiyunani. Basi wakuu wa makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato, Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi. Pilato akajibu, Niliyoandika nimeyaandika. Nao askari walipomsulibisha Yesu, waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu. Basi wakaambiana, Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani. Ili litimie andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, Na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari. Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake. Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu. Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani. Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.

Shirikisha
Soma Yohane 19

Yohane 19:16-30 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndipo Pilato akamkabidhi Yesu kwao ili wamsulubishe. Kwa hiyo askari wakamchukua Yesu. Yesu, akiwa ameubeba msalaba wake, akatoka kuelekea mahali palipoitwa Fuvu la Kichwa (kwa Kiebrania ni Golgotha). Hapo ndipo walipomsulubisha. Pamoja naye walisulubisha watu wengine wawili, mmoja kila upande wake, naye Yesu katikati. Pilato akaamuru tangazo liandikwe na liwekwe juu kwenye msalaba wa Yesu, likasema: “YESU WA NAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI.” Kwa kuwa mahali hapo Yesu aliposulubiwa palikuwa karibu na mjini, Wayahudi wengi walisoma maandishi haya yaliyokuwa yameandikwa kwa lugha za Kiebrania, Kiyunani na Kilatini. Viongozi wa makuhani wa Wayahudi wakapinga, wakamwambia Pilato, “Usiandike ‘Mfalme wa Wayahudi,’ bali andika kwamba mtu huyu alisema yeye ni mfalme wa Wayahudi.” Pilato akawajibu, “Nilichokwisha kuandika, nimeandika!” Askari walipokwisha kumsulubisha Yesu, walichukua nguo zake wakazigawa mafungu manne, kila askari fungu lake. Ila walikubaliana wasilichane lile vazi lake kwa maana lilikuwa halina mshono bali limefumwa tangu juu hadi chini. Wakaambiana, “Tusilichane ila tulipigie kura ili kuamua ni nani atalichukua.” Hili lilitukia ili Maandiko yapate kutimizwa yale yaliyosema, “Wanagawana nguo zangu, na vazi langu wanalipigia kura.” Hayo ndiyo waliyoyafanya wale askari. Wakati huo huo karibu na msalaba wa Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada wa mamaye, na Maria mke wa Klopa, na Maria Magdalene. Yesu alipomwona mama yake mahali pale pamoja na yule mwanafunzi aliyempenda wamesimama karibu, akamwambia mama yake, “Mwanamke, huyo hapo ndiye mwanao,” kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyo hapo ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Yesu nyumbani kwake. Baada ya haya, Yesu hali akijua kuwa mambo yote yamemalizika, alisema ili kutimiza Maandiko, “Naona kiu.” Hapo palikuwa na bakuli lililojaa siki. Kwa hiyo wakachovya sifongo kwenye hiyo siki, wakaiweka kwenye ufito wa mti wa hisopo, wakampelekea mdomoni. Baada ya kuionja hiyo siki, Yesu akasema, “Imekwisha.” Akainamisha kichwa chake, akaitoa roho yake.

Shirikisha
Soma Yohane 19