Yohane 19:19-24
Yohane 19:19-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Pilato aliandika ilani akaiweka juu ya msalaba. Nayo ilikuwa imeandikwa hivi: “Yesu Mnazareti, Mfalme wa Wayahudi.” Wayahudi wengi waliisoma ilani hiyo, maana mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa karibu na mji. Tena ilani hiyo ilikuwa imeandikwa kwa Kiebrania, Kilatini, na Kigiriki. Basi, makuhani wakuu wakamwambia Pilato, “Usiandike: ‘Mfalme wa Wayahudi,’ ila ‘Yeye alisema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.’” Pilato akajibu, “Niliyoandika, nimeandika!” Askari walipokwisha msulubisha Yesu, walizichukua nguo zake, wakazigawa mafungu manne, fungu moja kwa kila askari. Walichukua pia na kanzu yake; kanzu hiyo ilikuwa imefumwa kwa kipande kimoja tu, bila mshono. Basi, hao askari wakashauriana: “Tusiipasue, ila tuipigie kura itakuwa ya nani.” Jambo hilo lilifanyika ili yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: “Waligawana mavazi yangu, na nguo yangu wakaipigia kura.” Basi, ndivyo walivyofanya hao askari.
Yohane 19:19-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI. Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale aliposulubiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa Kiebrania, na Kirumi, na Kigiriki. Basi wakuu wa makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato, Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi. Pilato akajibu, Niliyoandika nimeyaandika. Nao askari walipomsulubisha Yesu, waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu. Basi wakaambiana, Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani. Ili litimie andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, Na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari.
Yohane 19:19-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI. Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale aliposulibiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa Kiebrania, na Kirumi, na Kiyunani. Basi wakuu wa makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato, Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi. Pilato akajibu, Niliyoandika nimeyaandika. Nao askari walipomsulibisha Yesu, waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu. Basi wakaambiana, Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani. Ili litimie andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, Na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari.
Yohane 19:19-24 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Pilato akaamuru tangazo liandikwe na liwekwe juu kwenye msalaba wa Isa; likasema: ISA AL-NASIRI MFALME WA WAYAHUDI. Kwa kuwa mahali hapo Isa aliposulubiwa palikuwa karibu na mjini, Wayahudi wengi walisoma maandishi haya yaliyokuwa yameandikwa kwa lugha za Kiebrania, Kiyunani na Kilatini. Viongozi wa makuhani wa Wayahudi wakapinga, wakamwambia Pilato, “Usiandike ‘Mfalme wa Wayahudi,’ bali andika kwamba mtu huyu alisema yeye ni mfalme wa Wayahudi.” Pilato akawajibu, “Nilichokwisha kuandika, nimeandika!” Askari walipokwisha kumsulubisha Isa, walichukua nguo zake wakazigawa mafungu manne, kila askari fungu lake. Ila walikubaliana wasilichane lile vazi lake kwa maana lilikuwa halina mshono, bali limefumwa tangu juu hadi chini. Wakaambiana, “Tusilichane ila tulipigie kura ili kuamua ni nani atalichukua.” Hili lilitukia ili Maandiko yapate kutimizwa yale yaliyosema, “Wanagawana nguo zangu, na vazi langu wanalipigia kura.” Hayo ndiyo waliyoyafanya wale askari.