Yohane 2:1-11
Yohane 2:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ya tatu kulikuwa na harusi mjini Kana, mkoani Galilaya. Mama yake Yesu alikuwapo, naye Yesu alikuwa amealikwa harusini pamoja na wanafunzi wake. Divai ilipokwisha, mama yake akamwambia, “Hawana divai!” Yesu akamjibu, “Mama, usiniambie la kufanya. Saa yangu bado.” Hapo mama yake akawaambia watumishi, “Lolote atakalowaambieni, fanyeni.” Hapo palikuwa na mitungi sita ya mawe, ambayo kila mmoja uliweza kuchukua kiasi cha madebe mawili au matatu. Ilikuwa imewekwa hapo kufuatana na desturi ya Kiyahudi ya kutawadha. Yesu akawaambia, “Ijazeni mitungi hiyo maji.” Nao wakaijaza mpaka juu. Kisha akawaambia, “Sasa choteni mkampelekee mkuu wa karamu.” Mkuu wa karamu alipoonja hayo maji, kumbe yalikuwa yamegeuka kuwa divai. Yeye hakujua ilikotoka, (lakini wale watumishi waliochota maji walijua). Mkuu wa karamu akamwita bwana arusi, akamwambia, “Kila mtu huandaa divai nzuri kwanza hata wakisha tosheka huandaa ile hafifu. Lakini wewe umeiweka divai nzuri mpaka sasa!” Yesu alifanya ishara hii ya kwanza huko Kana, Galilaya, akaonesha utukufu wake; nao wanafunzi wake wakamwamini.
Yohane 2:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai ilipowaishia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai. Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia. Mamaye akawaambia watumishi, Lolote atakalowaambia, fanyeni. Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kunawa, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu. Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza mpaka juu. Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa sherehe. Wakapeleka. Naye mkuu wa sherehe alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa sherehe alimwita bwana arusi, akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; na watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa. Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.
Yohane 2:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai. Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia. Mamaye akawaambia watumishi, Lo lote atakalowaambia, fanyeni. Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu. Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu. Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza. Wakapeleka. Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi, akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa. Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.
Yohane 2:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku ya tatu kulikuwa na arusi katika mji wa Kana ya Galilaya, naye mama yake Yesu alikuwepo pale. Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wamealikwa arusini pia. Divai ilipokwisha, mama yake Yesu akamwambia, “Wameishiwa na divai.” Yesu akamwambia, “Mwanamke, nina nini nawe? Saa yangu haijawadia.” Mama yake akawaambia wale watumishi, “Lolote atakalowaambia, fanyeni.” Basi ilikuwepo mitungi sita ya kuhifadhia maji iliyotengenezwa kwa mawe kwa ajili ya kujitakasa kwa desturi ya Kiyahudi; kila mtungi ungeweza kuchukua vipipa viwili au vitatu. Yesu akawaambia wale watumishi, “Ijazeni hiyo mitungi maji.” Nao wakaijaza ile mitungi mpaka juu. Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kidogo, mpelekeeni mkuu wa meza.” Hivyo wakachota, wakampelekea. Yule mkuu wa meza akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilika kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji wao walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando akamwambia, “Watu wote hutoa kwanza divai nzuri, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa vya kutosha, lakini wewe umeiweka ile nzuri kupita zote mpaka sasa.” Huu, ndio uliokuwa muujiza wa kwanza Yesu aliofanya Kana ya Galilaya. Hivyo Yesu alidhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.