Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 20:1-31

Yohane 20:1-31 Biblia Habari Njema (BHN)

Alfajiri na mapema Jumapili, kukiwa bado na giza, Maria Magdalene alikwenda kaburini, akaliona lile jiwe limeondolewa mlangoni pa kaburi. Basi, akaenda mbio hadi kwa Petro na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, “Wamemwondoa Bwana kaburini, na wala hatujui walikomweka.” Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine wakaenda kaburini. Wote wawili walikimbia lakini yule mwanafunzi mwingine alikimbia mbio kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini. Alipoinama na kuchungulia ndani, aliona sanda, lakini hakuingia ndani. Simoni Petro naye akaja akimfuata, akaingia kaburini; humo akaona sanda, na kile kitambaa alichofungwa Yesu kichwani. Hicho kitambaa hakikuwekwa pamoja na hiyo sanda, bali kilikuwa kimekunjwa na kuwekwa mahali peke yake. Kisha yule mwanafunzi mwingine aliyetangulia kufika kaburini, akaingia pia ndani, akaona, akaamini. ( Walikuwa bado hawajaelewa Maandiko Matakatifu yaliyosema kwamba ilikuwa lazima afufuke kutoka kwa wafu). Basi, hao wanafunzi wakarudi nyumbani. Maria alikuwa amesimama nje ya kaburi, akilia. Huku akiwa bado analia, aliinama na kuchungulia kaburini, akawaona malaika wawili waliovaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja kichwani na wa pili miguuni. Hao malaika wakamwuliza, “Mama, kwa nini unalia?” Naye akawaambia, “Wamemwondoa Bwana wangu, na wala sijui walikomweka!” Baada ya kusema hayo, aligeuka nyuma, akamwona Yesu amesimama hapo, lakini asitambue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwuliza, “Mama, kwa nini unalia? Unamtafuta nani?” Maria, akidhani kwamba huyo ni mtunza bustani, akamwambia, “Mheshimiwa, kama ni wewe umemwondoa, niambie ulikomweka, nami nitamchukua.” Yesu akamwambia, “Maria!” Naye Maria akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, “Raboni” (yaani “Mwalimu”). Yesu akamwambia, “Usinishike; sijaenda bado juu kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu uwaambie: Naenda juu kwa Baba yangu na Baba yenu, Mungu wangu na Mungu wenu.” Hivyo Maria Magdalene akaenda akawapasha habari wale wanafunzi kuwa amemwona Bwana, na kwamba alikuwa amemwambia hivyo. Ilikuwa jioni ya siku hiyo ya Jumapili. Wanafunzi walikuwa wamekutana pamoja ndani ya nyumba, na milango ilikuwa imefungwa kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi. Basi, Yesu akaja, akasimama kati yao, akawaambia, “Amani kwenu!” Alipokwisha sema hayo, akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Basi, hao wanafunzi wakafurahi mno kumwona Bwana. Yesu akawaambia tena, “Amani kwenu! Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma nyinyi.” Alipokwisha sema hayo, akawapulizia na kuwaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. Mkiwasamehe watu dhambi zao, wamesamehewa; msipowasamehe, hawasamehewi.” Thoma, mmoja wa wale kumi na wawili (aitwaye Pacha), hakuwa pamoja nao wakati Yesu alipokuja. Basi, wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana.” Thoma akawaambia, “Nisipoona mikononi mwake alama za misumari na kutia kidole changu katika kovu hizo, na kutia mkono wangu ubavuni mwake, sitasadiki.” Basi, baada ya siku nane hao wanafunzi walikuwa tena pamoja mle ndani, na Thoma alikuwa pamoja nao. Milango ilikuwa imefungwa, lakini Yesu akaja, akasimama kati yao, akasema, “Amani kwenu!” Kisha akamwambia Thoma, “Lete kidole chako hapa uitazame mikono yangu; lete mkono wako ukautie ubavuni mwangu. Usiwe na mashaka, ila amini!” Thoma akamjibu, “Bwana wangu na Mungu wangu!” Yesu akamwambia, “Je, unaamini kwa kuwa umeniona? Heri yao wale ambao hawajaona, lakini wameamini.” Yesu alifanya mbele ya wanafunzi wake ishara nyingine nyingi ambazo hazikuandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini kwamba Yesu ni Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mpate kuwa na uhai kwa nguvu ya jina lake.

Shirikisha
Soma Yohane 20

Yohane 20:1-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Hata siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalene alikwenda kaburini alfajiri, kukiwa bado giza; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka. Basi Petro akatoka, na yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini. Wakaenda mbio wote wawili; na yule mwanafunzi mwingine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza kufika kaburini. Akainama na kuchungulia, akaona vitambaa vya sanda vimelala; lakini hakuingia. Basi akaja na Simoni Petro, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala, na ile leso iliyokuwako kichwani pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwazongwa mbali mahali peke yake. Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza kufika kaburini, akaona na kuamini. Kwa maana hawajalifahamu bado andiko, ya kwamba imempasa kufufuka. Basi wale wanafunzi wakaenda zao tena nyumbani kwao. Lakini Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia. Wakati alipokuwa akilia, aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi. Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu. Nao wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka. Naye akiisha kusema hayo, akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa. Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (Yaani, Mwalimu wangu). Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu. Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo. Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Na wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa. Lakini mmoja wa wale Kumi na Wawili, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. Basi wanafunzi wengine wakamwambia, Tumemwona Bwana. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo. Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu. Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye. Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu! Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki. Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini muwe na uzima kwa jina lake.

Shirikisha
Soma Yohane 20

Yohane 20:1-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalene alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka. Basi Petro akatoka, na yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini. Wakaenda mbio wote wawili; na yule mwanafunzi mwingine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza kufika kaburini. Akainama na kuchungulia, akaona vitambaa vya sanda vimelala; lakini hakuingia. Basi akaja na Simoni Petro, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala, na ile leso iliyokuwako kichwani pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwa-zongwa mbali mahali pa peke yake. Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na kuamini. Kwa maana hawajalifahamu bado andiko, ya kwamba imempasa kufufuka. Basi wale wanafunzi wakaenda zao tena nyumbani kwao. Lakini Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia. Basi akilia hivi, aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi. Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu. Nao wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka. Naye akiisha kusema hayo, akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa. Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (Yaani, Mwalimu wangu). Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu. Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo. Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa. Walakini mmoja wa wale Thenashara, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. Basi wanafunzi wengine wakamwambia, Tumemwona Bwana. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo. Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu. Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye. Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu! Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki. Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.

Shirikisha
Soma Yohane 20

Yohane 20:1-31 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma, kulipokuwa bado giza, Mariamu Magdalene alienda kaburini na kukuta lile jiwe limeondolewa penye ingilio. Hivyo akakimbia kwa Simoni Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, na kusema, “Wamemwondoa Bwana kaburini, na hatujui walikomweka!” Petro na yule mwanafunzi mwingine wakaondoka mara moja kuelekea kaburini. Wote wawili walikuwa wanakimbia, lakini yule mwanafunzi mwingine akakimbia mbio kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini. Akainama na kuchungulia mle kaburini, akaona vile vitambaa vya kitani, lakini hakuingia. Ndipo Simoni Petro akaja akimfuata nyuma, akaingia ndani ya kaburi. Naye akaona vile vitambaa vya ile sanda vikiwa pale chini, na kile kitambaa kilichokuwa kichwani mwa Yesu. Kitambaa hicho kilikuwa kimekunjwa peke yake, mbali na vile vitambaa vya kitani vya ile sanda. Kisha yule mwanafunzi aliyetangulia kufika kaburini akaingia ndani, akaona, na akaamini. (Kwa kuwa hadi wakati huo walikuwa bado hawajaelewa kutoka Maandiko kwamba ilikuwa lazima Yesu afufuke kutoka kwa wafu.) Kisha hao wanafunzi wakaondoka, wakarudi nyumbani mwao. Lakini Mariamu Magdalene akasimama nje ya kaburi akilia. Alipokuwa akilia, akainama kuchungulia mle kaburini, naye akaona malaika wawili wamevaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni. Wakamuuliza Mariamu, “Mwanamke, mbona unalia?” Akawaambia, “Nalia kwa kuwa wamemchukua Bwana wangu, na sijui walikomweka.” Baada ya kusema hayo, akageuka, akamwona Yesu amesimama, lakini hakumtambua. Yesu akamwambia, “Mwanamke, mbona unalia? Unamtafuta nani?” Mariamu, akidhani alikuwa anaongea na mtunza bustani, akamwambia, “Bwana, kama ni wewe umemchukua, tafadhali nioneshe ulikomweka, nami nitamchukua.” Yesu akamwita, “Mariamu!” Ndipo Mariamu akamgeukia Yesu na kusema naye kwa Kiebrania, “Raboni!” (maana yake “Mwalimu”). Yesu akamwambia, “Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ ” Kwa hiyo Mariamu Magdalene akaenda kuwatangazia wanafunzi wa Yesu, akisema, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaambia kwamba Yesu alikuwa amemweleza mambo hayo yote. Ilipokuwa jioni ya siku hiyo hiyo ya kwanza ya juma, wanafunzi wake walikuwa pamoja, milango ikiwa imefungwa kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi. Naye Yesu akawatokea, akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!” Baada ya kusema haya, akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Wanafunzi wake wakafurahi sana walipomwona Bwana. Yesu akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi.” Alipokwisha kusema haya, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. Mkimwondolea mtu yeyote dhambi zake, zitaondolewa; na yeyote msiyemwondolea dhambi zake, hazitaondolewa.” Lakini Tomaso (aliyeitwa Didimasi), mmoja wa wale kumi na wawili, hakuwa pamoja nao Yesu alipokuja. Hivyo wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana.” Lakini yeye akawaambia, “Nisipoona zile alama za misumari mikononi mwake, na kuweka kidole changu kwenye hizo alama za misumari, na mkono wangu ubavuni mwake, sitaamini.” Baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwa tena pamoja ndani ya nyumba, naye Tomaso alikuwa pamoja nao. Ndipo Yesu akaja, milango ikiwa imefungwa, na kusimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi.” Kisha akamwambia Tomaso, “Weka kidole chako hapa na uone mikono yangu, nyoosha mkono wako uguse ubavuni mwangu. Usiwe na shaka, bali uamini tu.” Tomaso akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu!” Yesu akamwambia, “Umeamini kwa kuwa umeniona? Wamebarikiwa wale ambao hawajaona lakini wameamini.” Yesu alifanya miujiza mingine mingi mbele za wanafunzi wake, ambayo haikuandikwa katika kitabu hiki. Lakini hii imeandikwa ili mweze kuamini ya kuwa Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu, na kwa kumwamini mpate uzima katika jina lake.

Shirikisha
Soma Yohane 20