Yohane 4:43-53
Yohane 4:43-53 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya siku mbili Yesu aliondoka hapo, akaenda Galilaya. Maana Yesu mwenyewe alisema waziwazi kwamba, “Nabii hapati heshima katika nchi yake.” Basi, alipofika Galilaya, Wagalilaya wengi walimkaribisha. Maana nao pia walikuwa kwenye sikukuu ya Pasaka, wakayaona mambo yote Yesu aliyotenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu hiyo. Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya, mahali alipogeuza maji kuwa divai. Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto mgonjwa huko Kafarnaumu. Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka Yudea na kufika Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake aliyekuwa mgonjwa mahututi. Yesu akamwambia, “Msipoona ishara na maajabu hamtaamini!” Huyo ofisa akamwambia, “Bwana, tafadhali twende kabla mwanangu hajafa.” Yesu akamwambia, “Nenda tu, mwanao ataishi.” Huyo mtu akaamini maneno ya Yesu, akaenda zake. Alipokuwa bado njiani, watumishi wake walikutana naye, wakamwambia kwamba mwanawe alikuwa mzima. Naye akawauliza saa mtoto alipopata nafuu; nao wakamwambia, “Jana saa saba mchana, homa ilimwacha.” Huyo baba akakumbuka kwamba ilikuwa ni saa ileile ambapo Yesu alimwambia: “Mwanao ataishi.” Hapo yeye akaamini pamoja na jamaa yake yote.
Yohane 4:43-53 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na baada ya siku mbili hizo akaondoka huko, akaenda Galilaya. Kwa maana Yesu mwenyewe alishuhudia ya kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe. Basi alipotoka Galilaya, Wagalilaya walimpokea; kwa kuwa wameyaona mambo yote aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu; maana hao nao waliiendea sikukuu. Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na ofisa mmoja ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Yudea mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa karibu kufa. Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa? Yule ofisa akamwambia, Bwana, ushuke mtoto wangu asije akafa. Yesu akamwambia, Nenda; mwanao yu hai. Mtu yule akaliamini lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia. Na alipokuwa akishuka, watumwa wake walimlaki, wakisema ya kwamba mtoto wake yu hai. Basi akawauliza habari ya saa alipoanza kuwa na nafuu; nao wakamwambia, Jana, saa saba, homa ilimwacha. Basi babaye akafahamu ya kuwa ni saa ile ile aliyoambiwa na Yesu, Mwanao yu hai. Akaamini yeye na wote wa nyumbani mwake.
Yohane 4:43-53 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na baada ya siku mbili hizo akaondoka huko, akaenda Galilaya. Kwa maana Yesu mwenyewe alishuhudia ya kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe. Basi alipotoka Galilaya, Wagalilaya walimpokea; kwa kuwa wameyaona mambo yote aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu; maana hao nao waliiendea sikukuu. Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe hawezi huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa kufani. Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa? Yule diwani akamwambia, Bwana, ushuke asijakufa mtoto wangu. Yesu akamwambia, Enenda; mwanao yu hai. Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia. Hata alipokuwa akishuka, watumwa wake walimlaki, wakisema ya kwamba mtoto wake yu hai. Basi akawauliza habari ya saa alipoanza kuwa hajambo; nao wakamwambia, Jana, saa saba, homa ilimwacha. Basi babaye akafahamu ya kuwa ni saa ile ile aliyoambiwa na Yesu, Mwanao yu hai. Akaamini yeye na wote wa nyumbani mwake.
Yohane 4:43-53 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Baada ya zile siku mbili, Isa aliondoka kwenda Galilaya. (Basi Isa mwenyewe alikuwa amesema kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe.) Alipofika Galilaya, Wagalilaya walimkaribisha, kwani walikuwa wameona yale aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa Sikukuu ya Pasaka. Kwa maana wao pia walikuwa wamehudhuria hiyo Sikukuu. Hivyo Isa akafika tena Kana ya Galilaya, kule alikuwa amebadili maji kuwa divai. Kulikuwa na afisa mmoja wa mfalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. Huyo mtu aliposikia kwamba Isa alikuwa amewasili Galilaya kutoka Yudea, alimwendea na kumsihi aende akamponye mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa. Isa akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.” Yule afisa wa mfalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.” Isa akamjibu, “Nenda zako, mwanao yu hai.” Yule afisa akaamini yale maneno Isa aliyomwambia, akaenda zake. Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake, wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima. Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, “Jana saa saba, ndipo homa iliisha.” Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati Isa alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Isa.