Yohane 5:30-47
Yohane 5:30-47 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi ninahukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma. Nikijishuhudia mimi mwenyewe, ushahidi wangu hauwezi kukubaliwa kuwa wa kweli. Lakini yuko mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba yote anayosema juu yangu ni ya kweli. Nyinyi mlituma ujumbe kwa Yohane naye aliushuhudia ukweli. Si kwamba mimi nautegemea ushahidi wa wanadamu, lakini nasema mambo haya ili mpate kuokolewa. Yohane alikuwa kama taa iliyokuwa ikiwaka na kuangaza, nanyi mlikuwa tayari kufurahia mwanga huo kwa kitambo. Lakini mimi nina ushahidi juu yangu ambao ni mkuu zaidi kuliko ule wa Yohane. Kwa maana kazi ninazofanya, kazi alizonipa Baba nizifanye, ndizo zinazonishuhudia kwamba Baba ndiye aliyenituma. Naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Nyinyi hamjapata kamwe kusikia sauti yake, wala kuuona uso wake, na ujumbe wake haukai ndani yenu maana hamkumwamini yule aliyemtuma. Nyinyi huyachunguza Maandiko Matakatifu mkidhani kwamba ndani yake mtapata uhai wa milele; na kumbe maandiko hayohayo yananishuhudia! Hata hivyo, nyinyi hamtaki kuja kwangu ili mpate uhai. “Shabaha yangu si kupata sifa kutoka kwa watu. Lakini nawajua nyinyi, najua kwamba upendo kwa Mungu haumo mioyoni mwenu. Mimi nimekuja kwa mamlaka ya Baba yangu, lakini hamnipokei; bali mtu mwingine akija kwa mamlaka yake mwenyewe, mtampokea. Mwawezaje kuamini, hali nyinyi mnapenda kupokea sifa kutoka kwenu nyinyi wenyewe, wala hamtafuti sifa kutoka kwake yeye aliye peke yake Mungu? Msifikiri kwamba mimi nitawashtaki kwa Baba. Mose ambaye nyinyi mmemtumainia ndiye atakayewashtaki. Kama kweli mngemwamini Mose, mngeniamini na mimi pia, maana Mose aliandika juu yangu. Lakini hamyaamini yale aliyoandika; mtawezaje basi, kuamini maneno yangu?”
Yohane 5:30-47 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenituma. Mimi nikijishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. Yuko mwingine anayenishuhudia; nami najua ya kuwa ushuhuda wake anaonishuhudia ni kweli. Ninyi mlituma watu kwa Yohana, naye akaishuhudia kweli. Si kwamba ninaupokea ushuhuda wa wanadamu; lakini ninasema haya ili ninyi mpate kuokoka. Yeye alikuwa taa iwakayo na kung'aa, nanyi mlipenda kuishangilia nuru yake kwa muda. Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkuu kuliko ule wa Yohana; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma. Naye Baba aliyenituma amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wowote, wala sura yake hamkuiona. Wala neno lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi hammwamini yule aliyetumwa na yeye. Mnayachunguza maandiko kwa sababu mnadhani kuwa ndani yake ninyi mna uzima wa milele; na maandiko yayo hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima. Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu. Lakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu. Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo. Mnawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti? Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa, mnayemtumaini ninyi. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika habari zangu. Lakini msipoyaamini maandiko yake, mtayaamini maneno yangu vipi?
Yohane 5:30-47 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Mimi nikijishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. Yuko mwingine anayenishuhudia; nami najua ya kuwa ushuhuda wake anaonishuhudia ni kweli. Ninyi mlituma watu kwa Yohana, naye akaishuhudia kweli. Lakini mimi siupokei ushuhuda kwa wanadamu; walakini ninasema haya ili ninyi mpate kuokoka. Yeye alikuwa taa iwakayo na kung’aa, nanyi mlipenda kuishangilia nuru yake kwa muda. Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohana; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma. Naye Baba aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wo wote, wala sura yake hamkuiona. Wala neno lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi hammwamini yule aliyetumwa na yeye. Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima. Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu. Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu. Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo. Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti? Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa, mnayemtumaini ninyi. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika habari zangu. Lakini msipoyaamini maandiko yake, mtayaamini wapi maneno yangu?
Yohane 5:30-47 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Mimi siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninavyosikia ndivyo ninavyohukumu, nayo hukumu yangu ni ya haki kwa kuwa sitafuti kufanya mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake yeye aliyenituma. “Kama ningejishuhudia mimi mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. Lakini yuko mwingine anishuhudiaye na ninajua kwamba ushuhuda wake ni wa kweli. “Mlituma wajumbe kwa Yohana, naye akashuhudia juu ya kweli. Si kwamba naukubali ushuhuda wa mwanadamu, la, bali ninalitaja hili kusudi ninyi mpate kuokolewa. Yohana alikuwa taa iliyowaka na kutoa nuru, nanyi kwa muda mlichagua kuifurahia nuru yake. “Lakini ninao ushuhuda mkuu zaidi kuliko wa Yohana. Kazi zile nizifanyazo, zinashuhudia juu yangu, zile ambazo Baba amenituma nizikamilishe, naam, ishara hizi ninazofanya, zinashuhudia kuwa Baba ndiye alinituma. Naye Baba mwenyewe ameshuhudia juu yangu. Hamjapata kamwe kuisikia sauti yake wala kuona umbo lake, wala hamna neno lake ndani yenu, kwa sababu hamkumwamini yeye aliyetumwa naye. Ninyi mnachunguza Maandiko mkidhani ya kuwa ndani yake mna uzima wa milele, maandiko haya ndiyo yanayonishuhudia Mimi. Lakini mnakataa kuja kwangu ili mpate uzima. “Mimi sitafuti kutukuzwa na wanadamu. Lakini ninajua kwamba hamna upendo wa Mungu mioyoni mwenu. Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, nanyi hamnipokei, lakini mtu mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea. Ninyi mwawezaje kuamini ikiwa mnapeana utukufu ninyi kwa ninyi, lakini hamna bidii kupata utukufu utokao kwa Mungu? “Lakini msidhani kuwa mimi nitawashtaki mbele za Baba, mshtaki wenu ni Mose, ambaye mmemwekea tumaini lenu. Kama mngelimwamini Mose, mngeliniamini na mimi kwa maana aliandika habari zangu. Lakini ikiwa hamwamini aliyoandika Mose, mtaaminije ninayoyasema?”