Yohane 6:1-14
Yohane 6:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya hayo, Yesu alivuka ziwa Galilaya (au ziwa Tiberia). Umati mkubwa wa watu ulimfuata kwa sababu watu hao walikuwa wameona ishara alizokuwa akifanya kwa kuwaponya wagonjwa. Yesu alipanda mlimani, akaketi pamoja na wanafunzi wake. Sikukuu ya Wayahudi iitwayo Pasaka ilikuwa imekaribia. Basi, Yesu alipotazama na kuona umati wa watu ukija kwake, alimwambia Filipo, “Tununue wapi mikate ili watu hawa wapate kula?” (Alisema hivyo kwa kumjaribu Filipo, kwani alijua mwenyewe atakalofanya.) Filipo akamjibu, “Mikate ya fedha dinari 200 haiwatoshi watu hawa hata kama kila mmoja atapata kipande kidogo tu!” Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, “Yupo hapa mtoto mmoja aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; lakini hivi vyatosha nini kwa watu wengi kama hawa?” Yesu akasema, “Waketisheni watu.” Palikuwa na nyasi tele mahali hapo. Basi, watu wakaketi, jumla yapata wanaume 5,000. Yesu akaitwaa ile mikate, akamshukuru Mungu, akawagawia watu waliokuwa wameketi; akafanya vivyo hivyo na wale samaki, kila mtu akapata kadiri alivyotaka. Watu waliposhiba Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki visipotee.” Basi, wakakusanya vipande vya mikate ya shayiri walivyobakiza wale watu waliokula, wakajaza vikapu kumi na viwili. Watu walipoiona ishara hiyo aliyoifanya Yesu, wakasema, “Hakika huyu ndiye nabii anayekuja ulimwenguni.”
Yohane 6:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya hayo Yesu alikwenda zake ng'ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye Yesu akapanda mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu. Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, ana mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi wanaume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee chochote. Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni.
Yohane 6:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baada ya hayo Yesu alikwenda zake ng’ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye Yesu akakwea mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu. Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote. Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni.
Yohane 6:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya haya, Yesu alikwenda ngʼambo ya Bahari ya Galilaya, ambayo pia huitwa Bahari ya Tiberia. Umati mkubwa wa watu uliendelea kumfuata, kwa sababu waliona ishara nyingi za miujiza alizofanya kwa wagonjwa. Kisha Yesu akapanda mlimani akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia. Yesu alipotazama na kuuona ule umati mkubwa wa watu ukimjia, akamwambia Filipo, “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?” Aliuliza swali hili kumpima, kwa maana alishajua la kufanya. Filipo akamjibu, “Hata fedha kiasi cha dinari mia mbili, hazitoshi kununua mikate ya kuwapa watu hawa ili kila mtu apate kidogo.” Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, ndugu yake Simoni Petro, akamwambia, “Hapa kuna mvulana mmoja mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Lakini hivi vitatosha nini kwa umati huu wote?” Yesu akasema, “Waketisheni watu chini.” Palikuwa na majani mengi katika eneo lile, nao watu wakaketi. Palikuwa na wanaume wapatao 5,000. Ndipo Yesu akachukua ile mikate, akamshukuru Mungu na kuwagawia wale watu waliokuwa wameketi. Akafanya vivyo hivyo na wale samaki. Kila mtu akapata kadiri alivyotaka. Watu wote walipokwisha kula na kushiba, akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki vya ile mikate, kisipotee chochote.” Hivyo wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vya ile mikate mitano ya shayiri na samaki wale wawili wadogo vilivyobakishwa na waliokula. Baada ya watu kuona muujiza ule Yesu aliofanya, walianza kusema, “Hakika huyu ndiye Nabii ajaye ulimwenguni!”