Yohane 6:60-71
Yohane 6:60-71 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, wengi wa wafuasi wake waliposikia hayo, wakasema, “Haya ni mambo magumu! Nani awezaye kuyasikiliza?” Yesu alijua bila kuambiwa na mtu kwamba wanafunzi wake walikuwa wananungunika juu ya jambo hilo, akawauliza, “Je, jambo hili linawafanya muwe na mashaka? Itakuwaje basi, mtakapomwona Mwana wa Mtu akipanda kwenda kule alikokuwa kwanza? Roho ndiyo iletayo uhai; mwili hauwezi kitu. Maneno niliyowaambia ni roho na uhai. Hata hivyo, wako baadhi yenu wasioamini.” (Yesu alisema hivyo kwani alijua tangu mwanzo ni kina nani wasioamini, na pia ni nani atakayemsaliti). Kisha akasema, “Ndiyo maana niliwaambieni kwamba hakuna awezaye kuja kwangu asipowezeshwa na Baba yangu.” Kutokana na hayo, wengi wa wafuasi wake walirudi nyuma, wasiandamane naye tena. Basi, Yesu akawauliza wale kumi na wawili, “Je, nanyi pia mwataka kwenda zenu?” Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tutakwenda kwa nani? Wewe unayo maneno ya uhai wa milele. Sisi tunaamini, na tunajua kwamba wewe ndiwe yule Mtakatifu wa Mungu” Yesu akawaambia, “Je, sikuwachagua nyinyi kumi na wawili? Hata hivyo, mmoja wenu ni Ibilisi!” Yesu alisema hayo juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti; maana huyu alikuwa ndiye atakayemsaliti, ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili.
Yohane 6:60-71 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia, walisema, Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia? Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung'unikia neno hilo, akawaambia, Je! Neno hili linawakwaza? Itakuwaje basi, mumwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima. Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti. Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Kumi na Wawili, Je! Ninyi nanyi mnataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumeamini, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu. Yesu akawajibu, Je! Mimi sikuwachagua ninyi Kumi na Wawili, na mmoja wenu ni shetani? Alimnena Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti; maana huyo ndiye atakayemsaliti; naye ni mmojawapo wa wale Kumi na Wawili.
Yohane 6:60-71 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia, walisema, Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia? Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung’unikia neno hilo, akawaambia, Je! Neno hili linawakwaza? Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima. Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti. Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu. Yesu akawajibu, Je! Mimi sikuwachagua ninyi Thenashara, na mmoja wenu ni shetani? Alimnena Yuda, mwana wa Simoni Iskariote; maana huyo ndiye atakayemsaliti; naye ni mmojawapo wa wale Thenashara.
Yohane 6:60-71 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wengi wa wafuasi wake waliposikia jambo hili wakasema, “Mafundisho haya ni magumu. Ni nani awezaye kuyapokea?” Yesu alipojua kwamba wafuasi wake wananungʼunika kuhusu mafundisho yake, akawaambia, “Je, jambo hili limewaudhi? Ingekuwaje basi kama mngemwona Mwana wa Adamu akipaa kwenda zake huko alipokuwa kwanza? Roho ndiye atiaye uzima, mwili haufai kitu. Maneno haya niliyowaambia ni Roho tena ni uzima. Lakini baadhi yenu hamwamini.” Kwa maana Yesu alifahamu tangu mwanzo wale ambao hawangemwamini miongoni mwao na yule ambaye angemsaliti. Akaendelea kusema, “Hii ndiyo sababu niliwaambia kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.” Tangu wakati huo wafuasi wake wengi wakarejea nyuma wakaacha kumfuata. Hivyo Yesu akawauliza wale wanafunzi wake kumi na wawili, “Je, ninyi pia mnataka kuondoka?” Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tuondoke twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Tunaamini na kujua kuwa wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu.” Ndipo Yesu akajibu, “Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Lakini mmoja wenu ni ibilisi.” (Hapa alikuwa anasema juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili, ndiye ambaye baadaye angemsaliti Yesu.)