Yohane 7:10-24
Yohane 7:10-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata ndugu zake walipokwisha kukwea kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye alipokwea, si kwa wazi bali kana kwamba kwa siri. Basi Wayahudi wakamtafuta kwenye sikukuu, wakasema, Yuko wapi yule? Kukawa na manung’uniko mengi katika makutano juu yake. Wengine wakasema, Ni mtu mwema. Na wengine wakasema, Sivyo; bali anawadanganya makutano. Walakini hakuna mtu aliyemtaja waziwazi, kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi. Hata ikawa katikati ya sikukuu Yesu alikwea kuingia hekaluni, akafundisha. Wayahudi wakastaajabu wakisema, Amepataje huyu kujua elimu, ambaye hakusoma? Basi Yesu akawajibu, akasema, Mafunzo yangu si yangu mimi, ila ni yake yeye aliyenipeleka. Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu, au kwamba mimi nanena kwa nafsi yangu tu. Yeye anenaye kwa nafsi yake tu hutafuta utukufu wake mwenyewe; bali yeye anayetafuta utukufu wake aliyempeleka, huyo ni wa kweli, wala ndani yake hamna udhalimu. Je! Musa hakuwapa torati? Wala hakuna mmoja wenu aitendaye torati. Mbona mnatafuta kuniua? Mkutano wakajibu, Ama! Una pepo! Ni nani anayetafuta kukuua? Yesu akajibu, akawaambia, Mimi nalitenda kazi moja, nanyi nyote mnaistaajabia. Musa aliwapa tohara; lakini si kwamba yatoka kwa Musa, bali kwa mababa; nanyi siku ya sabato humtahiri mtu. Basi ikiwa mtu hupashwa tohara siku ya sabato, ili torati ya Musa isije ikavunjika, mbona mnanikasirikia mimi kwa sababu nalimfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya sabato? Basi msihukumu hukumu ya macho tu, bali ifanyeni hukumu iliyo ya haki.
Yohane 7:10-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini hakuenda kwa hadhara bali kwa siri. Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; wakauliza, “Yuko wapi?” Kulikuwa na minongono mingi katika umati wa watu. Baadhi yao walisema, “Ni mtu mwema.” Wengine walisema, “La! Anawapotosha watu.” Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema habari zake hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi. Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda hekaluni, akaanza kufundisha. Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema, “Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?” Hapo Yesu akawajibu, “Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma. Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe. Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote. Je, Mose hakuwapeni sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika sheria. Kwa nini mnataka kuniua?” Hapo watu wakamjibu, “Una pepo wewe! Nani anataka kukuua?” Yesu akawajibu, “Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia. Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba desturi hiyo ilitoka kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa nyinyi humtahiri mtu hata siku ya Sabato. Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi sheria isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya Sabato? Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki.”
Yohane 7:10-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata ndugu zake walipokwisha kupanda kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye alipopanda, si kwa wazi bali kana kwamba kwa siri. Basi Wayahudi wakamtafuta kwenye sikukuu, wakasema, Yuko wapi yule? Kukawa na manung'uniko mengi katika makutano juu yake. Wengine wakasema, Ni mtu mwema. Na wengine wakasema, Sivyo; bali anawadanganya makutano. Lakini hakuna mtu aliyemsema waziwazi, kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi. Hata ikawa katikati ya sikukuu Yesu alipanda kuingia hekaluni, akafundisha. Wayahudi wakastaajabu wakisema, Amepataje huyu kujua elimu, ambaye hakusoma? Basi Yesu akawajibu, akasema, Mafunzo yangu si yangu mimi, ila ni yake yeye aliyenituma. Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu, au kwamba mimi nanena kwa nafsi yangu tu. Yeye anenaye kwa nafsi yake tu hutafuta utukufu wake mwenyewe; bali yeye anayetafuta utukufu wake aliyemtuma, huyo ni wa kweli, wala ndani yake hamna udhalimu. Je! Musa hakuwapa torati? Wala hakuna mmoja wenu aitendaye torati. Mbona mnatafuta kuniua? Mkutano wakajibu, Ama! Una pepo! Ni nani anayetafuta kukuua? Yesu akajibu, akawaambia, Mimi nilitenda kazi moja, nanyi nyote mnaistaajabia. Musa aliwapa tohara; lakini si kwamba yatoka kwa Musa, bali kwa mababa; nanyi mwatahiri mtu siku ya sabato. Basi ikiwa mtu hupashwa tohara siku ya sabato, ili Torati ya Musa isije ikavunjika, mbona mnanikasirikia mimi kwa sababu nilimfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya sabato? Basi msihukumu kwa kuangalia kwa nje tu, bali ifanyeni hukumu iliyo ya haki.
Yohane 7:10-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini ndugu zake walipokwisha kuondoka kwenda kwenye Sikukuu, yeye pia alikwenda lakini kwa siri. Wayahudi walikuwa wakimtafuta huko kwenye Sikukuu na kuulizana, “Yuko wapi huyu mtu?” Kulikuwa na minongʼono iliyoenea kumhusu Yesu katika umati wa watu, wakati wengine wakisema, “Ni mtu mwema.” Wengine walikuwa wakisema, “La, yeye anawadanganya watu.” Lakini hakuna mtu yeyote aliyemsema waziwazi kumhusu kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi. Ilipokaribia katikati ya Sikukuu, Yesu alipanda kwenda Hekaluni na kuanza kufundisha. Wayahudi wakastaajabia mafundisho yake wakasema, “Mtu huyu amepataje kujua mambo haya bila kufundishwa?” Ndipo Yesu akawajibu, “Mafundisho yangu si yangu mwenyewe, bali yanatoka kwake yeye aliyenituma. Mtu yeyote akipenda kufanya mapenzi ya Mungu, atajua kama mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu au ninasema kwa ajili yangu mwenyewe. Wale wanenao kwa ajili yao wenyewe hufanya hivyo kwa kutaka utukufu wao wenyewe. Lakini yeye atafutaye utukufu wa yule aliyemtuma ni wa kweli, wala hakuna uongo ndani yake. Je, Mose hakuwapa ninyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja wenu anayeishika hiyo sheria. Kwa nini mnataka kuniua?” Ule umati wa watu ukamjibu, “Wewe una pepo mchafu! Ni nani anayetaka kukuua?” Yesu akawajibu, “Nimefanya muujiza mmoja na nyote mkastaajabu. Lakini kwa kuwa Mose aliwaamuru tohara (ingawa kwa kweli haikutoka kwa Mose bali kwa baba zenu wakuu), mnamtahiri mtoto hata siku ya Sabato. Ikiwa mtoto aweza kutahiriwa siku ya Sabato kusudi sheria ya Mose isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia kwa kumponya mtu mwili wake wote siku ya Sabato? Acheni kuhukumu mambo kwa jinsi mnavyoona tu, bali hukumuni kwa haki.”