Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 7:37-52

Yohane 7:37-52 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake. Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa. Basi wengine katika mkutano walipoyasikia maneno hayo, walisema, Hakika huyu ndiye nabii yule. Wengine walisema, Huyu ndiye Kristo. Wengine wakasema, Je! Kristo atoka Galilaya? Andiko halikusema ya kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu, mji ule alioukaa Daudi? Basi kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake. Baadhi yao wakataka kumkamata, lakini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika. Basi wale watumishi wakawaendea wakuu wa makuhani na Mafarisayo. Nao wakawaambia, Mbona hamkumleta? Wale watumishi wakajibu. Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena. Basi Mafarisayo wakawajibu, Je! Ninyi nanyi mmedanganyika? Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo? Lakini makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa. Akawaambia Nikodemo, (naye ni yule aliyemwendea zamani, maana ni mmoja wao), Je! Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo? Wakajibu, wakamwambia, Je! Wewe nawe umetoka Galilaya! Tafuta, ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokea nabii.

Shirikisha
Soma Yohane 7

Yohane 7:37-52 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalumu. Yesu alisimama, akasema kwa sauti kubwa, “Aliye na kiu na aje kwangu anywe. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: ‘Anayeniamini mimi, mito ya maji ya uhai itatiririka kutoka moyoni mwake!’” (Alisema hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea. Wakati huo Roho alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado). Baadhi ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, “Kweli mtu huyu ndiye yule nabii!” Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!” Lakini wengine walisema, “Je, yawezekana Kristo akatoka Galilaya? Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: ‘Kristo atatoka katika ukoo wa Daudi, na atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!’” Basi, kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu. Baadhi ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata. Kisha wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza, “Kwa nini hamkumleta?” Walinzi wakawajibu, “Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo mtu huyu!” Mafarisayo wakawauliza, “Je, nanyi pia mmedanganyika? Je, mmekwisha kumwona hata mmoja wa viongozi wa watu, au mmoja wa Mafarisayo aliyemwamini? Lakini umati huu haujui sheria ya Mose; umelaaniwa!” Mmoja wao alikuwa Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu. Basi, yeye akawaambia, “Je, sheria yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza na kujua anafanya nini?” Nao wakamjibu, “Je, wewe pia umetoka Galilaya? Haya, kayachunguze Maandiko Matakatifu nawe utaona kwamba Galilaya hakutoki kamwe nabii!”

Shirikisha
Soma Yohane 7

Yohane 7:37-52 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Yesu akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe. Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yasemavyo, vijito vya maji ya uzima vitatiririka ndani mwake.” Yesu aliposema haya alimaanisha Roho Mtakatifu ambaye wote waliomwamini wangempokea, kwani mpaka wakati huo, Roho alikuwa hajatolewa, kwa kuwa Yesu alikuwa bado hajatukuzwa. Waliposikia maneno hayo, baadhi ya watu miongoni mwa ule umati wakasema, “Hakika huyu ndiye yule Nabii.” Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!” Lakini wengine wakauliza, “Je, Kristo kwao ni Galilaya? Je, Maandiko hayasemi kwamba Kristo atakuja kutoka jamaa ya Daudi na kutoka Bethlehemu, mji alioishi Daudi?” Kwa hiyo watu wakagawanyika kwa ajili ya Yesu. Baadhi yao walitaka kumkamata, lakini hakuna aliyethubutu kumgusa. Hatimaye wale walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliokuwa wamewatuma ili kumkamata Yesu, wakaulizwa, “Mbona hamkumkamata?” Wale walinzi wakajibu, “Kamwe hajanena mtu yeyote kama yeye anenavyo.” Mafarisayo wakajibu, “Je, nanyi pia mmedanganyika? Je, kuna kiongozi yeyote au mmoja wa Mafarisayo ambaye amemwamini? Lakini huu umati wa watu wasiojua Sheria ya Mose, wamelaaniwa.” Ndipo Nikodemo, yule aliyekuwa amemwendea Yesu siku moja usiku, ambaye alikuwa mmoja wao akauliza, “Je, sheria zetu zinaturuhusu kumhukumu mtu kabla ya kumsikiliza na kufahamu alilotenda?” Wakamjibu, “Je, wewe pia unatoka Galilaya? Chunguza nawe utaona kwamba hakuna nabii atokae Galilaya!” [

Shirikisha
Soma Yohane 7