Yohane 8:1-11
Yohane 8:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini Yesu akaenda kwenye mlima wa Mizeituni. Kesho yake asubuhi na mapema alikwenda tena hekaluni. Watu wote wakamwendea, naye akaketi akawa anawafundisha. Basi, waalimu wa sheria na Mafarisayo wakamletea mwanamke mmoja aliyefumaniwa katika uzinzi. Wakamsimamisha katikati yao. Kisha wakamwuliza Yesu, “Mwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi. Katika sheria yetu Mose alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe. Basi, wewe wasemaje?” Walisema hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akainama chini, akaandika ardhini kwa kidole. Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, “Mtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe.” Kisha akainama tena, akawa anaandika ardhini. Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmojammoja, wakitangulia wazee. Yesu akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale. Yesu alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, “Wako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?” Huyo mwanamke akamjibu, “Bwana, hakuna hata mmoja!” Naye Yesu akamwambia, “Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena.”]
Yohane 8:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Walikwenda kila mtu nyumbani kwake; naye Yesu akaenda mpaka katika mlima wa Mizeituni. Asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha. Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake kama hawa; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika ardhi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika ardhi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati. Yesu akainuka asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; wala usitende dhambi tena.]
Yohane 8:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
[Walikwenda kila mtu nyumbani kwake; naye Yesu akaenda mpaka mlima wa Mizeituni. Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha. Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati. Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.]
Yohane 8:1-11 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Lakini Isa akaenda katika Mlima wa Mizeituni. Alfajiri na mapema Isa akaja tena Hekaluni; watu wote wakakusanyika, naye akaketi, akaanza kuwafundisha. Walimu wa Torati na Mafarisayo wakamleta mwanamke mmoja aliyefumaniwa akizini. Wakamsimamisha katikati ya umati wa watu wote. Wakamwambia Isa, “Mwalimu, huyu mwanamke amekutwa akizini. Katika sheria, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake wa namna hii, hadi wafe. Sasa wewe wasemaje?” Walimuuliza swali hili kama mtego ili wapate sababu ya kumshtaki. Lakini Isa akainama akaanza kuandika ardhini kwa kidole chake. Walipoendelea kumuulizauliza akainuka, akawaambia, “Kama kuna mtu yeyote miongoni mwenu ambaye hana dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe.” Akainama tena na kuandika ardhini. Waliposikia haya, wakaanza kuondoka mmoja mmoja, wakianzia wazee, hadi Isa akabaki peke yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele yake. Isa akainuka na kumwambia, “Mwanamke, wako wapi wale waliokuwa wanakuhukumu kuwa mwenye hatia?” Yule mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja, Bwana.” Isa akamwambia, “Hata mimi sikuhukumu. Nenda zako. Kuanzia sasa usitende dhambi tena.”]