Yohane 8:52-59
Yohane 8:52-59 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Wayahudi wakasema, “Sasa tunajua kweli kwamba wewe una pepo! Abrahamu alikufa, na manabii pia walikufa, nawe wasema ati, ‘Anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele!’ Je, unajifanya mkuu kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa? Hata na manabii walikufa. Wewe unajifanya kuwa nani?” Yesu akawajibu, “Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu. Baba yangu ambaye nyinyi mwasema ni Baba yenu, ndiye anayenitukuza. Nyinyi hamjapata kumjua, lakini mimi namjua. Na, nikisema simjui, nitakuwa mwongo kama nyinyi. Mimi namjua na ninashika neno lake. Abrahamu, baba yenu, alishangilia aione siku yangu; naye aliiona, akafurahi.” Basi, Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujatimiza miaka hamsini bado, nawe umemwona Abrahamu?” Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, kabla Abrahamu hajazaliwa, mimi niko.” Hapo wakaokota mawe ili wamtupie, lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni.
Yohane 8:52-59 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Wayahudi wakamwambia, Sasa tumeng'amua ya kuwa una pepo. Abrahamu amekufa, na manabii wamekufa; nawe wasema, Mtu akilishika neno langu, hataonja mauti milele. Wewe u mkuu kuliko baba yetu Abrahamu, ambaye amekufa? Nao manabii wamekufa. Wajifanya u nani? Yesu akajibu, Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu; anitukuzaye ni Baba yangu, ambaye ninyi mwanena kuwa ni Mungu wenu. Wala ninyi hamkumjua; lakini mimi namjua. Nikisema ya kwamba simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi; lakini namjua, na neno lake nilishika. Abrahamu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi. Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Abrahamu? Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Kabla ya Abrahamu kuwako, mimi niko. Basi wakaokota mawe ili wamtupie; lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni.
Yohane 8:52-59 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Wayahudi wakamwambia, Sasa tumeng’amua ya kuwa una pepo. Ibrahimu amekufa, na manabii wamekufa; nawe wasema, Mtu akilishika neno langu, hataonja mauti milele. Wewe u mkuu kuliko baba yetu Ibrahimu, ambaye amekufa? Nao manabii wamekufa. Wajifanya u nani? Yesu akajibu, Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu; anitukuzaye ni Baba yangu, ambaye ninyi mwanena kuwa ni Mungu wenu. Wala ninyi hamkumjua; lakini mimi namjua. Nikisema ya kwamba simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi; lakini namjua, na neno lake nalishika. Ibrahimu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi. Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu? Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko. Basi wakaokota mawe ili wamtupie; lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni.
Yohane 8:52-59 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Ndipo Wayahudi wakapaza sauti, wakamwambia, “Sasa tumejua kwamba una pepo mchafu! Ibrahimu alikufa, na manabii vilevile, nawe unasema kuwa mtu akitii neno lako hatakufa milele. Je, wewe ni mkuu kuliko baba yetu Ibrahimu ambaye alikufa, na manabii ambao pia walikufa? Unafikiri wewe ni nani?” Isa akawajibu, “Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu hauna maana. Baba yangu, huyo ambaye ninyi mnadai kuwa ni Mungu wenu, ndiye anitukuzaye mimi. Ingawa hamkumjua, mimi ninamjua. Kama ningesema simjui, ningekuwa mwongo kama ninyi, lakini mimi ninamjua na ninalitii neno lake. Baba yenu Ibrahimu alishangilia kwamba angeiona siku yangu, naye akaiona na akafurahi.” Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujatimiza hata miaka hamsini, nawe wasema umemwona Ibrahimu?” Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, kabla Ibrahimu hajakuwa, Mimi niko.” Ndipo wakaokota mawe ili kumpiga, lakini Isa akajificha, naye akatoka Hekaluni.