Yobu 33:23-33
Yobu 33:23-33 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini malaika akiwapo karibu naye, mmoja kati ya maelfu ya watetezi wa Mungu, ili kumwonesha lililo jema la kufanya, akamwonea huruma na kumwambia Mungu; ‘Mwokoe asiingie Shimoni, ninayo fidia kwa ajili yake.’ Hapo mwili wake utaweza kuwa tena kama kijana, ataweza kurudia tena nguvu zake za ujana. Kisha atamwomba Mungu na kukubaliwa, atakuja mbele yake kwa furaha, na Mungu atamrudishia fahari yake. Atashangilia mbele ya watu na kusema: ‘Nilitenda dhambi na kupotosha haki, nami sikuadhibiwa kutokana na hayo. Mungu aliniokoa nisiangamie Shimoni; nimebaki hai na ninaona mwanga.’ “Tazama Mungu humfanyia binadamu haya yote, tena mara mbili, mara tatu. Humwokoa binadamu asiangamie Shimoni, aweze kuona mwanga wa maisha. Sikia Yobu, nisikilize kwa makini; kaa kimya, nami nitasema. Kama una la kusema, nijibu; sema, maana nataka kukuona huna hatia. La sivyo, nyamaza unisikilize, kaa kimya nami nikufunze hekima.”
Yobu 33:23-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwamba akiwapo malaika pamoja naye, Mkalimani, mmoja katika elfu, Ili kumwonyesha binadamu hayo yampasayo; Ndipo amwoneapo rehema, na kusema, Mwokoe asishuke shimoni; Mimi nimeuona ukombozi. Nyama ya mwili wake itakuwa laini kuliko ya mtoto; Huzirudia siku za ujana wake; Yeye humwomba Mungu, naye akamtakabalia; Hata auone uso wake kwa furaha; Naye humrejezea mtu haki yake. Yeye huimba mbele ya watu, na kusema, Mimi nimefanya dhambi, na kuyapotosha hayo yaliyoelekea, Wala sikulipizwa jambo hilo; Yeye ameikomboa nafsi yangu isiende shimoni, Na uhai wangu utautazama mwanga. Tazama, hayo yote ni Mungu anayeyafanya, Mara mbili, naam, hata mara tatu, kwa mtu, Ili kurudisha roho yake itoke shimoni, Ili atiwe mwanga kwa mwanga wa walio hai. Angalia sana, Ee Ayubu, unisikilize; Nyamaza, mimi nitasema. Kama una neno la kusema, nijibu; Nena, kwani nataka kukuhesabia kuwa na haki. Kama sivyo, unisikilize mimi; Nyamaza, nami nitakufunza hekima.
Yobu 33:23-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini akiwapo malaika pamoja naye, Mpatanishi, mmoja katika elfu, Ili kumwonesha binadamu hayo yampasayo; Ndipo amwoneapo rehema, na kusema, Mwokoe asishuke shimoni; Mimi nimeuona ukombozi. Nyama ya mwili wake itakuwa laini kuliko ya mtoto; Huzirudia siku za ujana wake; Yeye humwomba Mungu, naye akamtakabalia; Hata auone uso wake kwa furaha; Naye humrejeshea mtu haki yake. Yeye huimba mbele ya watu, na kusema, Mimi nimefanya dhambi, na kuyapotosha hayo yaliyoelekea, Wala sikulipizwa jambo hilo; Yeye ameikomboa nafsi yangu isiende shimoni, Na uhai wangu utautazama mwanga. Tazama, hayo yote ni Mungu anayeyafanya, Mara mbili, naam, hata mara tatu, kwa mtu, Ili kurudisha roho yake itoke shimoni, Ili atiwe mwanga kwa mwanga wa walio hai. Angalia sana, Ee Ayubu, unisikilize; Nyamaza, mimi nitasema. Kama una neno la kusema, nijibu; Nena, kwani nataka kukuhesabia kuwa na haki. Kama sivyo, unisikilize mimi; Nyamaza, nami nitakufunza hekima.
Yobu 33:23-33 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Kama bado kuna malaika upande wake kama mtetezi, mmoja miongoni mwa elfu, wa kumwambia mwanadamu lililo jema kwake, kumwonea huruma na kusema, ‘Mwokoe asije akatumbukia shimoni; nimepata ukombozi kwa ajili yake’: ndipo nyama ya mwili wake hufanywa mpya kama ya mtoto; hurudishwa upya kama siku za ujana wake. Humwomba Mungu, akapata kibali kwake, huuona uso wa Mungu na kushangilia kwa furaha; Mungu humrudisha katika hali yake ya uadilifu. Ndipo huja mbele za watu na kusema, ‘Nilitenda dhambi na kupotosha kilichokuwa haki, lakini sikuadhibiwa kama nilivyostahili. Alinikomboa nafsi yangu nisitumbukie shimoni, nami nitaishi ili kuufurahia mwanga.’ “Mungu hufanya haya yote kwa mwanadamu; mara mbili hata mara tatu, ili aigeuze nafsi yake toka shimoni, ili nuru ya uzima imwangazie. “Ayubu, zingatia, nisikilize mimi; nyamaza, nami nitanena. Kama unalo lolote la kusema, unijibu; sema, kwa maana ninataka uonekane huna hatia. Lakini kama huna la kusema, basi nisikilize mimi; nyamaza, nami nitakufundisha hekima.”