Yobu 34:16-30
Yobu 34:16-30 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kama una akili sikiliza; sikiliza ninachokuambia. Je, anayetawala ulimwengu kwa sheria zake anachukia haki? Je, utathubutu kumhukumu mwadilifu na mwenye nguvu? Amwambiaye mfalme, ‘Wewe ni takataka!’ Na watu mashuhuri, ‘Nyinyi ni waovu!’ Yeye hawapendelei wakuu, wala kuwajali matajiri kuliko maskini, maana wote hao ni kazi ya mikono yake. Kufumba na kufumbua hao wamekufa; hutikiswa usiku na kuaga dunia; nao wenye nguvu hufutiliwa mbali bila kutumia nguvu za mtu. “Macho ya Mungu huchunguza mienendo ya watu; yeye huziona hatua zao zote. Hakuna weusi wala giza nene ambamo watenda maovu waweza kujificha. Mungu hahitaji kumjulisha mtu wakati wa kumleta mbele ya mahakama yake. Huwaangamiza wenye nguvu bila uchunguzi, na kuwaweka wengine mahali pao. Kwa kuwa anayajua matendo yao yote, huwaporomosha usiku wakaangamia. Huwachapa hadharani kwa ajili ya uovu wao, kwa sababu wameacha kumfuata yeye, wakazipuuza njia zake zote. Hata wakasababisha kilio cha maskini kimfikie Mungu, Mungu akasikiliza kilio chao hao walioteswa. Kama Mungu akinyamaza, nani awezaye kumlaumu? Kama akificha uso wake, nani awezaye kumwona, liwe ni taifa au mtu mmojammoja? Hufanya hivyo, mtu mbaya asitawale, au wale wahatarishao maisha ya watu.
Yobu 34:16-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikiwa una ufahamu, sikia neno hili; Isikilize sauti ya maneno yangu. Je! Atatawala mtu aichukiaye haki hata mmoja? Nawe, je! Utamhukumia mkosa aliye na haki na mwenye nguvu? Je! Inafaa kumwambia mfalme, Wewe u mwovu? Au kuwaambia wakuu, Ninyi ni wabaya? Sembuse huyo asiyependelea nyuso za wakuu, Wala hawajali matajiri kuliko maskini? Kwani wote ni kazi ya mikono yake, Hufa ghafula, hata usiku wa manane; Watu hutikisika na kwenda zao, Nao mashujaa huondolewa pasipo mkono wa mtu. Kwani macho yake ya juu ya njia za mtu, Naye huiona miendo yake yote. Hapana weusi, wala hilo giza tupu, Wawezapo kujificha watendao udhalimu. Kwani yeye hana haja ya kumfikiria mtu zaidi, ili aende mbele za Mungu ahukumiwe. Yeye huwavunja-vunja mashujaa pasina kuwachunguza, Na kuwaweka wengine mahali pao. Kwa sababu hiyo yeye huyatafiti matendo yao; Naye huwapindia usiku, wakaangamia. Yeye huwapiga kama watu wabaya Waziwazi mbele ya macho ya wengine; Kwa sababu walikengeuka, wasimwandame yeye, Wasikubali kuzishika njia zake hata moja; Hata wakafanya kilio cha maskini kumfikilia, Naye akasikia kilio cha hao wateswao. Akitoa utulivu yeye, ni nani awezaye kuhukumia makosa? Akificha uso wake, ni nani awezaye kumtazama? Kama hufanyiwa taifa, au mtu mmoja, ni sawasawa; Kwamba huyo mpotovu asitawale, Pasiwe na wa kuwatega watu.
Yobu 34:16-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikiwa una ufahamu, sikia neno hili; Isikilize sauti ya maneno yangu. Je! Atatawala mtu aichukiaye haki hata mmoja? Nawe, je! Utamhukumia mkosa aliye na haki na mwenye nguvu? Je! Inafaa kumwambia mfalme, Wewe u mwovu? Au kuwaambia wakuu, Ninyi ni wabaya? Sembuse yeye huwajali nyuso za wakuu, Wala hawajali matajiri kuliko maskini? Kwani wote ni kazi ya mikono yake, Hufa ghafla, hata usiku wa manane; Watu hutikisika na kwenda zao, Nao mashujaa huondolewa pasipo mkono wa mtu. Kwani macho yake yako juu ya njia za mtu, Naye huziona hatua zake zote. Hapana hofu ya giza kuu, mahali wawezapo kujificha watendao udhalimu. Kwani yeye hana haja ya kumfikiria mtu zaidi, ili aende mbele za Mungu ahukumiwe. Yeye huwavunjavunja mashujaa pasipo kuwachunguza, Na kuwaweka wengine mahali pao. Kwa sababu hiyo yeye huyatafiti matendo yao; Naye huwapindua usiku, wakaangamia. Yeye huwapiga kwa sababu ya uovu wao, Waziwazi mbele ya macho ya wengine; Kwa sababu walikengeuka, wasimfuate yeye, Wasikubali kuzishika njia zake hata moja; Hata wakafanya kilio cha maskini kumfikia, Naye akasikia kilio cha hao wateswao. Akitoa utulivu yeye, ni nani awezaye kuhukumia makosa? Akificha uso wake, ni nani awezaye kumtazama? Kama hufanyiwa taifa, au mtu mmoja, ni sawasawa; Ili huyo mpotovu asitawale, Wala pasiwe na wa kuwatega watu.
Yobu 34:16-30 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Kama ninyi mnaufahamu, sikieni hili; sikilizeni hili nisemalo. Je, yeye aichukiaye haki aweza kutawala? Je, utamhukumu mwenye haki, Aliye na Nguvu Zote? Je, si ni yeye awaambiaye wafalme, ‘Ninyi hamfai kitu,’ nao watu mashuhuri, ‘Ninyi ni waovu,’ yeye asiyependelea wakuu, wala haonyeshi upendeleo kwa matajiri kuliko maskini, kwa kuwa wote ni kazi ya mikono yake? Wanakufa ghafula, usiku wa manane; watu wanatikiswa nao hupita; wenye nguvu huondolewa bila mkono wa mwanadamu. “Macho yake yanazitazama njia za wanadamu; anaona kila hatua yao. Hakuna mahali penye giza nene, wala uvuli mkubwa, ambapo watenda mabaya wanaweza kujificha. Mungu hana haja ya kumchunguza mtu sana, ili apate kuja mbele zake kwa hukumu. Bila kuuliza huwapondaponda wenye nguvu nyingi na kuwaweka wengine mahali pao. Kwa sababu huyaangalia matendo yao yote, huwaondoa usiku, nao wakaangamia. Anawaadhibu kwa ajili ya uovu wao mahali ambapo kila mmoja ataweza kuwaona, kwa sababu wameacha kumfuata Mungu, nao hawakuiheshimu njia yake hata moja. Wamesababisha kilio cha maskini kifike mbele zake, hivyo akasikia kilio cha wahitaji. Lakini kama akinyamaza kimya, ni nani awezaye kumhukumu? Kama akiuficha uso wake, ni nani awezaye kumwona? Ikiwa ni taifa au mtu mmoja, kwake ni sawa, ili kumzuia mtu mwovu kutawala, au wale ambao huwategea watu mitego.