Yobu 35:1-16
Yobu 35:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Elihu akaendelea kusema: “Je, Yobu, unaona jambo hili ni sawa na kufikiri kinyume cha Mungu ukiuliza: ‘Nimepata faida gani kama sikutenda dhambi? Nimefaidika kuliko kama ningalitenda dhambi?’ Mimi nitakujibu wewe, na rafiki zako pia. Hebu zitazame mbingu! Tazama mawingu yaliyo juu kuliko wewe! Ukitenda dhambi, je, Mungu ndiye unayemdhuru? Na kama ukizidisha makosa yako, wadhani unamwumiza? Kama wewe ni mwema, je, unampatia faida, au yeye anapokea kitu kutoka kwako? Uovu wako utamdhuru binadamu kama wewe, wema wako utamfaa binadamu mwenzako. “Kwa sababu ya udhalimu mwingi watu hulia, huomba msaada kwa sababu ya mapigo ya wenye nguvu. Lakini hakuna asemaye, ‘Yuko wapi Mungu, Muumba wangu, mwenye kunifanya niwe mchangamfu usiku, anayetuelimisha kuliko wanyama, na kutufanya wenye hekima kuliko ndege!’ Watu hao huomba msaada lakini Mungu hawajibu, kwa sababu ya majivuno ya watu waovu. Kweli Mungu hasikilizi kilio cha bure; Mungu Mwenye Nguvu hajali kilio hicho. Atakujibu vipi wakati wewe unasema kwamba humwoni na kwamba kesi yako iko mbele yake na wewe unamngojea! Sasa, kwa vile Mungu anazuia hasira yake, wala hajali sana makosa ya watu, Yobu unafungua mdomo kusema maneno matupu, unazidisha maneno bila akili.”
Yobu 35:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena Elihu akajibu na kusema, Je! Wewe wadhani kwamba haya ni haki yako, Au je! Wasema, Haki yangu ni zaidi kuliko ya Mungu, Maana wasema, Kutakuwa na faida gani kwako wewe? Tena, Nitapata faida gani, kuliko nikifanya dhambi? Mimi nitakujibu, Na hawa wenzio pamoja nawe. Ziangalie mbingu ukaone; Na mawingu yaangalie, yaliyo juu kuliko wewe. Ikiwa umefanya dhambi, umefanya nini juu yake? Yakiwa makosa yako yameongezeka, wamfanyia nini yeye? Ikiwa u mwenye haki, wampa kitu gani? Au yeye hupokea nini mkononi mwako? Uovu wako waweza kumwumiza mtu kama wewe; Na haki yako yaweza kumfaa mwanadamu. Kwa sababu ya wingi wa jeuri wao hulia; Walilia msaada kwa sababu ya mkono wa wakuu. Wala hapana asemaye, Yuko wapi Mungu Muumba wangu, Awapaye nyimbo wakati wa usiku; Atufundishaye zaidi ya hayawani wa nchi, Na kutufanya wenye hekima kuliko ndege za angani? Hulia huko, lakini hapana ajibuye, Kwa sababu ya kiburi cha watu waovu. Hakika Mungu hatasikia ubatili, Wala Mwenyezi hatauangalia. Sembuse usemapo wewe ya kuwa humwangalii, Hiyo daawa i mbele yake, nawe wamngojea! Lakini sasa, kwa sababu yeye hakukujilia katika hasira zake, Wala hauangalii sana unyeti; Ndiposa Ayubu hufunua kinywa chake kwa ubatili; Huongeza maneno pasipo maarifa.
Yobu 35:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena Elihu akajibu na kusema, Je! Wewe wadhani kwamba haya ni haki yako, Au je! Wasema, Ni haki yangu mbele za Mungu, Maana wasema, Kutakuwa na faida gani kwako wewe? Tena, Nitapata faida gani, kuliko nikifanya dhambi? Mimi nitakujibu, Na hawa wenzio pamoja nawe. Ziangalie mbingu ukaone; Na mawingu yaangalie, yaliyo juu kuliko wewe. Ikiwa umefanya dhambi, umefanya nini juu yake? Ikiwa makosa yako yameongezeka, wamfanyia nini yeye? Ikiwa u mwenye haki, wampa kitu gani? Au yeye hupokea nini mkononi mwako? Uovu wako waweza kumwumiza mtu kama wewe; Na haki yako yaweza kumfaa mwanadamu. Kwa sababu ya wingi wa dhuluma wao hulia; Walilia msaada kwa sababu ya mkono wa wakuu. Wala hapana asemaye, Yuko wapi Mungu Muumba wangu, Awapaye nyimbo wakati wa usiku; Atufundishaye zaidi ya wanyama wa nchi, Na kutufanya wenye hekima kuliko ndege wa angani? Hulia huko, lakini hapana ajibuye, Kwa sababu ya kiburi cha watu waovu. Hakika Mungu hatasikia ubatili, Wala Mwenyezi hatauangalia. Sembuse usemapo wewe ya kuwa humwangalii, Hiyo kesi i mbele yake, nawe wamngojea! Lakini sasa, kwa sababu yeye hakukujia katika hasira zake, Wala hauzingatii sana makosa; Ndiposa Ayubu hufunua kinywa chake kwa ubatili; Huongeza maneno pasipo maarifa.
Yobu 35:1-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Elihu akasema: “Je, unadhani hili ni haki? Wewe unasema, ‘Nina haki mbele za Mungu.’ Bado unamuuliza, ‘Ni faida gani nimepata, na imenifaidi nini kwa kutokutenda dhambi?’ “Ningependa nikujibu wewe pamoja na marafiki zako walio pamoja nawe. Tazama juu mbinguni ukaone; yaangalie mawingu yaliyo juu sana juu yako. Je, ukitenda dhambi, inamdhuruje Mungu? Kama dhambi zako zikiwa nyingi, hilo linamfanyia nini Mungu? Kama wewe ni mwadilifu, unampa nini, au yeye anapokea nini mkononi kwako? Uovu wako unamdhuru tu mtu mwingine kama wewe, nayo haki yako inawafaa wanadamu tu. “Wanadamu hulia kwa kulemewa na mateso; huomba msaada kutoka mkono wenye nguvu. Lakini hakuna asemaye, ‘Yuko wapi Mungu Muumba wangu, yeye anifanyaye niimbe usiku, yeye atufundishaye sisi zaidi kuliko wanyama wa dunia, na kutufanya wenye hekima kuliko ndege wa angani?’ Yeye hajibu wakati watu waliapo kwa sababu ya kiburi cha watu waovu. Naam, Mungu hasikilizi maombi yao ya ubatili; Mwenyezi hayazingatii. Si zaidi sana kwamba hatakusikiliza wewe usemapo humwoni, tena ya kwamba shauri lako liko mbele zake na wewe lazima umngojee, pia zaidi, kwamba hasira yake kamwe haiadhibu wala haangalii uovu hata kidogo? Hivyo Ayubu hufumbua kinywa chake kwa maneno yasiyo na maana; anaongea maneno mengi bila maarifa.”