Yobu 37:14-24
Yobu 37:14-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Sikiliza neno hili, Ee Ayubu; Simama kimya, uzifikiri kazi za Mungu za ajabu. Je! Wajua wewe jinsi Mungu anavyoziagiza, Na kuumulikisha umeme wa wingu lake? Je! Wajua jinsi mawingu yalivyowekwa sawasawa, Hizo kazi za ajabu za huyo mkamilifu wa maarifa? Jinsi nguo zako zilivyo na moto, Hapo nchi ituliapo kwa sababu ya upepo wa kusini? Je! Waweza kuzitandaza mbingu pamoja naye, Ambazo zina nguvu kama kioo cha kuyeyushwa? Utufundishe ni maneno gani tutakayomwambia; Kwa maana hamwezi kuyatengeza kwa sababu ya giza. Je! Aambiwe kwamba nataka kunena? Au mtu angetamani kumezwa? Na sasa watu hawawezi kuutazama mwanga ung’aao mbinguni; Lakini upepo ukipita huzitakasa. Kaskazini hutokea umemetufu wa dhahabu; Mungu huvikwa ukuu utishao. yeye Mwenyezi hamwezi kumwona; Yeye ni mkuu mwenye uweza; Tena mwenye hukumu, na mwingi wa haki, hataonea. Kwa hiyo watu humwogopa; Yeye hawaangalii walio na hekima mioyoni.
Yobu 37:14-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Ayubu, sikiliza hili; nyamaza na uyafikiri maajabu ya Mungu. Je, unajua jinsi Mungu anavyoyaongoza mawingu, na kufanya umeme wake wa radi utoe mwanga? Je, wajua jinsi mawingu yanavyokaa yakiwa yametulia, hayo maajabu yake yeye aliye mkamilifu katika maarifa? Wewe unayeshindwa na joto katika nguo zako wakati nchi imenyamazishwa kimya bila upepo wa kusini, je, waweza kuungana naye katika kuzitandaza anga, zilizo ngumu kama kioo cha shaba ya kuyeyushwa? “Tuambieni yatupasayo kumwambia; hatuwezi kutayarisha shauri letu kwa sababu ya ujinga wetu. Je, aambiwe kwamba nataka kuongea? Je, yuko mtu ambaye angeomba kumezwa? Basi hakuna awezaye kulitazama jua, jinsi linavyongʼaa angani, upepo ukishafagia mawingu. Kutoka kaskazini yeye huja na fahari kuu; Mungu huja katika utukufu wa kutisha. Yeye Mwenyezi hatuwezi kumfikia, naye ametukuzwa katika uweza; katika hukumu zake na haki yake kuu, hataonea. Kwa hiyo, wanadamu mheshimuni, kwa kuwa yeye hamstahi yeyote anayejidhania kuwa ana hekima.”
Yobu 37:14-24 Biblia Habari Njema (BHN)
“Unapaswa kusikiliza Yobu; nyamaza, usikilize maajabu ya Mungu. Je, wajua jinsi Mungu anavyovipa amri yake, na kufanya umeme wa mawingu yake ungae? Je, wajua jinsi mawingu yanavyoelea angani? Ndizo kazi za ajabu za yule aliye mkamilifu wa maarifa! Wewe wajiona umevaa nguo za joto sana, wakati upepo wa kusi unaivamia nchi. Je, waweza, kuzitandaza mbingu kama yeye zikawa ngumu kama kioo cha shaba? Tufundishe tutakachomwambia Mungu; maana hoja zetu si wazi, tumo gizani. Je, nani anathubutu kumwambia: Nataka kuongea? Nani aseme apate balaa? “Ghafla mtu hawezi tena kuona waziwazi: Jua limefichika nyuma ya mawingu, na upepo umefagia anga! Mngao mzuri hutokea kaskazini; Mungu amezungukwa na utukufu wa kutisha. Mungu Mwenye Nguvu asiyeweza kufikiwa na mtu, uwezo na uadilifu wake ni mkuu, amejaa wema wala hapotoshi haki kamwe. Kwa hiyo, watu wote humwogopa; yeye hamjali mtu yeyote mwenye kiburi.”
Yobu 37:14-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Sikiliza neno hili, Ee Ayubu; Simama kimya, uzifikiri kazi za Mungu za ajabu. Je! Wajua wewe jinsi Mungu anavyoziagiza, Na kuufanya umeme wa wingu lake uangaze? Je! Wajua jinsi mawingu yalivyowekwa sawasawa, Hizo kazi za ajabu za huyo mkamilifu wa maarifa? Jinsi nguo zako zilivyo na moto, Hapo nchi ituliapo kwa sababu ya upepo wa kusini? Je! Waweza kuzitandaza mbingu pamoja naye, Ambazo zina nguvu kama kioo cha kuyeyushwa? Utufundishe ni maneno gani tutakayomwambia; Kwa kuwa hatuwezi kutoa hoja zetu maana tumo gizani. Je! Aambiwe kwamba nataka kunena? Au kuna mtu ambaye angetamani kumezwa? Na sasa watu hawawezi kuutazama mwanga ung'aao mbinguni; Lakini upepo ukipita huzitakasa. Kaskazini hutokea mng'ao wa dhahabu; Mungu huvikwa ukuu utishao. Yeye Mwenyezi hamwezi kumwona; Yeye ni mkuu mwenye uweza; Tena mwenye hukumu, na mwingi wa haki, hataonea. Kwa hiyo watu humwogopa; Yeye hawaangalii walio na hekima mioyoni.