Yobu 41:12-34
Yobu 41:12-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Sitanyamaa kusema habari za via vyake, Wala nguvu zake kuu, wala umbo lake zuri. Ni nani awezaye kumbambua magamba yake? Ni nani atakayepenya dirii yake maradufu? Ni nani awezaye kuifungua milango ya uso wake? Meno yake yatisha kandokando yake. Magamba yake yenye nguvu ndiyo fahari yake, Yamefungamana pamoja kama yaliyofungwa kwa mhuri. Jinsi yalivyoshikamana Hata upepo hauwezi kupita kati. Yamefungamana pamoja; Yameshikamana, hata hayawezi kutengwa. Kwa kuchemua kwake mwanga humemetuka, Na macho yake yanafanana na koze za alfajiri. Mienge iwakayo hutoka kinywani mwake, Na cheche za moto huruka nje. Moshi hutoka katika mianzi ya pua yake, Kama nyungu ikitokota, na manyasi yawakayo. Pumzi zake huwasha makaa, Na miali ya moto hutoka kinywani mwake. Katika shingo yake hukaa nguvu, Na utisho hucheza mbele yake. Minofu ya nyama yake hushikamana; Yanakazana juu yake; hayawezi kuondolewa. Moyo wake una uimara kama jiwe; Naam, uimara kama jiwe la chini la kusagia. Anapojiinua, mashujaa huogopa; Kwa sababu ya woga wao huvunjwa moyo. Mtu akimpiga kwa upanga, haumwingii; Wala fumo, wala mshale, wala mkuki wenye ncha. Yeye huona chuma kuwa kama nyasi, Na shaba kama mti uliooza. Mshale hauwezi kumkimbiza; Na mawe ya teo kwake hugeuka kuwa kama makapi. Marungu huhesabiwa kama mabua; Naye hucheka mshindo wa mkuki ukitupwa. Pande zake za chini ni kama vigae vikali; Hutandika malazi kama kuweka chombo cha kupuria nafaka juu ya matope. Yeye hufanya kilindi kichemke kama chungu; Hufanya bahari kuwa kama chungu cha mafuta. Hufanya mapito yake kung'aa nyuma yake Hata mtu angedhani kilindi kina mvi. Juu ya nchi hapana aliyefanana naye, kiumbe asiye na woga. Yeye hutazama kila kitu kilicho juu; Ni mfalme juu ya wote wenye kiburi.
Yobu 41:12-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Sitanyamaa kusema habari za via vyake, Wala nguvu zake kuu, wala umbo lake zuri. Ni nani awezaye kumbambua magamba yake? Ni nani atakayepenya dirii yake maradufu? Ni nani awezaye kuifungua milango ya uso wake? Meno yake yatisha kandokando yake. Magamba yake yenye nguvu ndiyo fahari yake, Yamefungamana pamoja kama kwa kufungwa kwa muhuri. Jinsi yalivyoshikamana Hata upepo hauwezi kupita kati. Yamefungamana pamoja; Yameshikamana, hata hayawezekani kutengwa. Kwa kuchemua kwake mwanga humemetuka, Na macho yake yanafanana na makope ya alfajiri. Mienge iwakayo hutoka kinywani mwake, Na macheche ya moto huruka nje. Moshi hutoka katika mianzi ya pua yake, Kama nyungu ikitokota, na manyasi yawakayo. Pumzi zake huwasha makaa, Na miali ya moto hutoka kinywani mwake. Katika shingo yake hukaa nguvu, Na utisho hucheza mbele yake. Manofu ya nyama yake hushikamana; Yanakazana juu yake; hayawezi kuondolewa. Moyo wake una imara kama jiwe; Naam, imara kama jiwe la chini la kusagia. Anapojiinua, mashujaa huogopa; Kwa sababu ya woga wao huvunjwa moyo. Mtu akimpiga kwa upanga, haumwingii; Wala fumo, wala mshale, wala mkuki wenye ncha. Yeye huona chuma kuwa kama nyasi, Na shaba kama mti uliooza. Mshale hauwezi kumkimbiza; Na mawe ya teo kwake hugeuka kuwa kama makapi. Marungu huhesabiwa kama mabua; Naye hucheka mshindo wa mkuki ukitupwa. Pande zake za chini ni kama vigae vikali; Hutandika malazi kama kuweka chombo cha kupuria nafaka juu ya matope. Yeye huchemsha kilindi mfano wa nyungu; Hufanya bahari kuwa kama mafuta. Hufanya mapito yake kung’aa nyuma yake Hata mtu angedhani kilindi kina mvi. Juu ya nchi hapana aliyefanana naye, Aliyeumbwa pasipo oga. Yeye hutazama kila kitu kilicho juu; Ni mfalme juu ya wote wenye kiburi.
Yobu 41:12-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Sitashindwa kunena juu ya maungo yake, nguvu zake na umbo lake zuri. Ni nani awezaye kumvua gamba lake la nje? Ni nani awezaye kumsogelea na lijamu? Nani athubutuye kuufungua mlango wa kinywa chake, kilichozungukwa na meno yake ya kutisha pande zote? Mgongo wake una safu za ngao zilizoshikamanishwa imara pamoja; kila moja iko karibu sana na mwenzake, wala hakuna hewa iwezayo kupita kati yake. Zimeunganishwa imara kila moja na nyingine; zimengʼangʼaniana pamoja wala haziwezi kutenganishwa. Akipiga chafya mwanga humetameta; macho yake ni kama mionzi ya mapambazuko. Mienge iwakayo humiminika kutoka kinywani mwake; cheche za moto huruka nje. Moshi hufuka kutoka puani mwake, kama kutoka kwenye chungu kinachotokota kwa moto wa matete. Pumzi yake huwasha makaa ya mawe, nayo miali ya moto huruka kutoka kinywani mwake. Nguvu hukaa katika shingo yake; utisho hutangulia mbele yake. Mikunjo ya nyama yake imeshikamana imara pamoja; iko imara na haiwezi kuondolewa. Kifua chake ni kigumu kama mwamba, kigumu kama jiwe la chini la kusagia. Ainukapo, mashujaa wanaogopa; hurudi nyuma mbele yake anapokwenda kwa kishindo. Upanga unaomfikia haumdhuru, wala mkuki au mshale wala fumo. Chuma hukiona kama unyasi, na shaba kama mti uliooza. Mishale haimfanyi yeye akimbie; mawe ya kombeo kwake ni kama makapi. Rungu kwake huwa kama kipande cha jani kavu; hucheka sauti za kugongana kwa mkuki. Sehemu zake za chini kwenye tumbo zina menomeno na mapengo kama vigae vya chungu, zikiacha mburuzo kwenye matope kama chombo chenye meno cha kupuria. Huvisukasuka vilindi kama sufuria kubwa ichemkayo, na kukoroga bahari kama chungu cha marhamu. Anapopita nyuma yake huacha mkondo unaometameta; mtu angedhani vilindi vilikuwa na mvi. Hakuna chochote duniani kinacholingana naye: yeye ni kiumbe kisicho na woga. Yeye huwatazama chini wale wote wenye kujivuna; yeye ni mfalme juu ya wote wenye kiburi.”