Yoeli 2:12-17
Yoeli 2:12-17 Biblia Habari Njema (BHN)
“Lakini hata sasa,” nasema mimi Mwenyezi-Mungu, “Nirudieni kwa moyo wote, kwa kufunga, kulia na kuomboleza. Msirarue mavazi yenu kuonesha huzuni bali nirudieni kwa moyo wa toba.” Mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; yeye amejaa neema na huruma; hakasiriki upesi, ni mwingi wa fadhili; daima yu tayari kuacha kuadhibu. Huenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atabadili nia na kuwapeni baraka ya mazao, mkamtolea sadaka za nafaka na kinywaji. Pigeni tarumbeta huko Siyoni! Toeni amri watu wafunge; itisheni mkutano wa kidini. Wakusanyeni watu wote, wawekeni watu wakfu. Waleteni wazee, wakusanyeni watoto, hata watoto wanyonyao. Bwana arusi na bibi arusi na watoke vyumbani mwao. Kati ya madhabahu na lango la hekalu, makuhani, wahudumu wa Mwenyezi-Mungu, walie na kuomba wakisema: “Wahurumie watu wako, ee Mwenyezi-Mungu. Usiyaache mataifa mengine yatudharau na kutudhihaki yakisema, ‘Yuko wapi basi Mungu wao?’”
Yoeli 2:12-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini hata sasa, asema BWANA, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuomboleza; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie BWANA, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi kuadhibu. Ni nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa BWANA, Mungu wenu? Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, Na hao wanyonyao maziwa; Bwana arusi na atoke chumbani mwake, Na bibi arusi katika hema yake. Hao makuhani, wahudumu wa BWANA, na walie Kati ya patakatifu na madhabahu, Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee BWANA, Wala usiutoe urithi wako upate aibu, Hata mataifa watawale juu yao; Kwa nini waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?
Yoeli 2:12-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini hata sasa, asema BWANA, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie BWANA, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. N’nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa BWANA, Mungu wenu? Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, Na hao wanyonyao maziwa; Bwana arusi na atoke chumbani mwake, Na bibi arusi katika hema yake. Hao makuhani, wahudumu wa BWANA, na walie Kati ya patakatifu na madhabahu, Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee BWANA, Wala usiutoe urithi wako upate aibu, Hata mataifa watawale juu yao; Kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?
Yoeli 2:12-17 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Hata sasa,” asema Mwenyezi Mungu, “nirudieni kwa mioyo yenu yote, kwa kufunga, kwa kulia na kuomboleza.” Rarueni mioyo yenu na siyo mavazi yenu. Mrudieni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa maana yeye ndiye mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo, huona huruma, hujizuia kuleta maafa. Ni nani ajuaye? Yeye aweza kugeuka na kuwa na huruma na kuacha baraka nyuma yake: sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Pigeni tarumbeta katika Sayuni, tangazeni saumu takatifu, liiteni kusanyiko takatifu. Wakusanyeni watu, wekeni wakfu kusanyiko; waleteni pamoja wazee, wakusanyeni watoto, wale wanyonyao maziwa. Bwana arusi na atoke chumbani mwake na bibi arusi naye atoke katika chumba chake. Makuhani, ambao wanahudumu mbele za Mwenyezi Mungu, na walie katikati ya ukumbi wa Hekalu na madhabahu. Waseme, “Wahurumie watu wako, Ee Mwenyezi Mungu. Usifanye urithi wako kitu cha kudharauliwa, neno la dhihaka kati ya mataifa. Kwa nini wasemezane miongoni mwao, ‘Yuko wapi Mungu wao?’ ”