Yoshua 22:1-5
Yoshua 22:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakati huo Yoshua akawaita Wareubeni, na Wagadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, naye akawaambia, Ninyi mmeyaandama hayo yote mliyoamriwa na Musa, mtumishi wa BWANA, nanyi mmeisikia sauti yangu katika yote niliyowaamuru mimi; hamkuwaacha hao ndugu zenu siku hizi nyingi hata hivi leo, lakini mmeyashika mausia ya amri ya BWANA, Mungu wenu. Na sasa yeye BWANA, Mungu wenu, amewapa ndugu zenu kustarehe, kama alivyowaambia; basi sasa rudini ninyi mwende mahemani kwenu, hata nchi ya milki yenu, ambayo huyo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwapa ng’ambo ya pili ya Yordani. Lakini mjibidiishe sana kuzifanya amri na sheria, ambazo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwaamuru, kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kwenenda katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na kushikamana na yeye, na kumtumikia kwa moyo wenu wote na nafsi yenu yote.
Yoshua 22:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Yoshua akawaita watu wa kabila la Reubeni, la Gadi na watu wa nusu ya kabila la Manase akawaambia, “Nyinyi mmefuata yale yote Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliyowaamuru na mmetii maagizo niliyowaamuru. Wala hamkuwaacha ndugu zenu muda huo wote mrefu mpaka leo, bali mmefuata kwa makini amri ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Sasa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amewapa ndugu zenu amani, kama vile alivyoahidi, basi, rudini kwenu katika nchi ambayo mlipewa na Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, iwe mali yenu, yaani ngambo ya mto Yordani. Muwe waangalifu kutii amri na sheria ambazo Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliwaamuru: Kumpenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mfuate anachotaka na kushika amri zake; mkae pamoja naye na kumtumikia kwa moyo wote na roho yote.”
Yoshua 22:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakati huo Yoshua akawaita Wareubeni, na Wagadi, na hiyo nusu ya kabila la Manase, naye akawaambia, Ninyi mmeyafuata hayo yote mliyoamriwa na Musa, mtumishi wa BWANA, nanyi mmeisikia sauti yangu katika yote niliyowaamuru mimi; hamkuwaacha hao ndugu zenu siku hizi nyingi hata hivi leo, lakini mmeyashika maagizo ya amri ya BWANA, Mungu wenu. Na sasa yeye BWANA, Mungu wenu, amewapa ndugu zenu kustarehe, kama alivyowaambia; basi sasa rudini ninyi mwende mahemani kwenu, hata nchi ya milki yenu, ambayo huyo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwapa ng'ambo ya pili ya Yordani. Lakini mjibidiishe sana kuzifanya amri na sheria, ambazo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwaamuru, kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kwenenda katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na kushikamana na yeye, na kumtumikia kwa moyo wenu wote na nafsi yenu yote.
Yoshua 22:1-5 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Yoshua akawaita Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, naye akawaambia, “Mmeshafanya yale yote Mose mtumishi wa BWANA aliyowaamuru, nanyi mmenitii kwa kila jambo nililowaamuru. Kwa muda mrefu sasa, hadi siku hii ya leo, hamkuwaacha ndugu zenu, bali ninyi mmetimiza ile kazi BWANA Mungu wenu aliyowapa. Sasa kwa kuwa BWANA Mungu wenu amewapa ndugu zenu pumziko kama alivyoahidi, rudini nyumbani mwenu katika nchi ile ambayo Mose mtumishi wa BWANA aliwapa ngʼambo ya Yordani. Lakini mwe waangalifu sana kushika amri na sheria zile Mose mtumishi wa BWANA alizowapa: yaani kumpenda BWANA Mungu wenu na kuenenda katika njia zake zote, kutii amri zake, kushikamana naye kwa uthabiti na kumtumikia kwa moyo wenu wote na roho yenu yote.”