Maombolezo 1:1-11
Maombolezo 1:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Ajabu mji uliokuwa umejaa watu, sasa wenyewe umebaki tupu! Ulikuwa maarufu kati ya mataifa; sasa umekuwa kama mama mjane. Miongoni mwa miji ulikuwa kama binti mfalme; sasa umekuwa mtumwa wa wengine. Walia usiku kucha; machozi yautiririka. Hakuna hata mmoja wa wapenzi wake wa kuufariji. Rafiki zake wote wameuhadaa; wote wamekuwa adui zake. Watu wa Yuda wamekwenda uhamishoni pamoja na mateso na utumwa mkali. Sasa wanakaa miongoni mwa watu wa mataifa, wala hawapati mahali pa kupumzika. Waliowafuatia wamewakamata wakiwa taabuni. Barabara za kwenda Siyoni zinasikitisha; hakuna wapitao kwenda kwenye sikukuu. Malango ya mji wa Siyoni ni tupu; makuhani wake wanapiga kite, wasichana wake wana huzuni, na mji wenyewe uko taabuni. Adui zake ndio wanaoutawala na wanafanikiwa, kwani Mwenyezi-Mungu ameutesa kwa sababu ya makosa mengi. Watoto wake wametekwa na kupelekwa mbali. Fahari yote ya watu wa Siyoni imewatoweka; wakuu wake wamekuwa kama kulungu wasio na malisho. Bila nguvu waliwakimbia watesi wao. Ukiwa sasa magofu matupu, Yerusalemu wakumbuka fahari yake. Ulipoangukia mikononi mwa maadui zake, hakuna aliyekuwako kuusaidia. Washindi wake walichekelea kuanguka kwake. Yerusalemu ulitenda dhambi mbaya, ukawa mchafu kwa dhambi zake. Wote waliousifia wanaudharau, maana wameuona uchi wake. Wenyewe wapiga kite na kujificha kwa aibu. Uchafu wake ulionekana waziwazi, lakini wenyewe haukujali mwisho wake. Anguko lake lilikuwa kubwa mno; hakuna awezaye kuufariji. Wasema: “Tazama ee Mwenyezi-Mungu mateso yangu, maana adui yangu ameshinda.” Maadui wamenyosha mikono yao, wanyakue vitu vyake vyote vya thamani. Naam umeona watu wa mataifa wakiingia hekaluni, watu ambao Mwenyezi-Mungu aliwakataza kujumuika na jumuiya ya watu wake. Watu wa Yerusalemu wote wanahangaika kutafuta chakula; hazina zao wanazitoa kupata chakula, wajirudishie nguvu zao. Nao mji unalia, “Hebu niangalie, ee Mwenyezi-Mungu, ona jinsi nilivyogeuka kuwa duni.
Maombolezo 1:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Jinsi mji huu ukaavyo ukiwa, Huo uliokuwa umejaa watu! Jinsi alivyokuwa kama mjane, Yeye aliyekuwa mkuu kati ya mataifa! Binti mfalme kati ya majimbo, Jinsi alivyoshikwa shokoa! Hulia sana wakati wa usiku, Na machozi yake yapo mashavuni; Miongoni mwa wote waliompenda Hakuna hata mmoja amfarijiye; Rafiki zake wote wamemtenda hila, Wamekuwa adui zake. Yuda amehamishwa kwa sababu ya kuonewa, Na kwa sababu ya utumwa mkuu; Anakaa kati ya mataifa, Haoni raha yoyote; Wote waliomfuata wamempata Katika dhiki yake. Njia za Sayuni zaomboleza, Kwa kuwa hakuna ajaye kwa sikukuu; Malango yake yote yamekuwa ukiwa, Makuhani wake hupiga kite; Wanawali wake wanahuzunika; Na yeye mwenyewe huona uchungu. Watesi wake wamekuwa kichwa, Adui zake hufanikiwa; Kwa kuwa BWANA amemtesa Kwa sababu ya wingi wa makosa yake; Watoto wake wadogo wamechukuliwa mateka Mbele yake huyo mtesi. Naye huyo binti Sayuni Enzi yake yote imemwacha; Wakuu wake wamekuwa kama ayala Wasioona malisho; Nao wamekwenda zao hawana nguvu Mbele yake anayewafuatia. Siku za mateso na misiba yake, Yerusalemu huyakumbuka matamanio yake yote Yaliyokuwa tangu siku za kale; Hapo watu wake walipoanguka mikononi mwa mtesi, Wala hakuna hata mmoja wa kumsaidia; Hao watesi wake walimwona, Wakafanya sabato zake kuwa mzaha. Yerusalemu amefanya dhambi sana; Kwa hiyo amekuwa kama kitu kichafu; Wote waliomheshimu wanamdharau, Kwa sababu wameuona uchi wake; Naam, yeye anaugua, Na kujigeuza aende nyuma. Uchafu wake ulikuwa katika marinda yake; Hakukumbuka mwisho wake; Kwa hiyo ameshuka kwa ajabu; Yeye hana mtu wa kumfariji; Tazama, BWANA, mateso yangu; Maana huyo adui amejitukuza. Huyo mtesi amenyosha mkono wake Juu ya matamanio yake yote; Maana ameona ya kuwa mataifa wameingia Ndani ya patakatifu pake; Ambao kwa habari zao wewe uliamuru Wasiingie katika kusanyiko lako. Watu wake wote hupiga kite, Wanatafuta chakula; Wameyatoa matamanio yao wapate chakula Cha kuihuisha nafsi; Ee BWANA, tazama, uangalie; Kwa maana mimi nimekuwa mnyonge.
Maombolezo 1:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Tazama jinsi mji ulivyoachwa ukiwa, mji ambao zamani ulikuwa umejaa watu! Jinsi ambavyo umekuwa kama mama mjane, ambaye wakati fulani alikuwa maarufu miongoni mwa mataifa! Yule ambaye alikuwa malkia miongoni mwa majimbo sasa amekuwa mtumwa. Kwa uchungu, hulia sana usiku, machozi yapo kwenye mashavu yake. Miongoni mwa wapenzi wake wote hakuna yeyote wa kumfariji. Rafiki zake wote wamemsaliti, wamekuwa adui zake. Baada ya mateso na kufanyishwa kazi kikatili, Yuda amekwenda uhamishoni. Anakaa miongoni mwa mataifa, hapati mahali pa kupumzika. Wote ambao wanamsaka wamemkamata katikati ya dhiki yake. Barabara zielekeazo Sayuni zaomboleza, kwa kuwa hakuna yeyote anayekuja kwenye sikukuu zake zilizoamriwa. Malango yake yote yamekuwa ukiwa, makuhani wake wanalia kwa uchungu, wanawali wake wanahuzunika, naye yuko katika uchungu wa maumivu makuu. Adui zake wamekuwa mabwana zake, watesi wake wana raha. BWANA amemletea huzuni kwa sababu ya dhambi zake nyingi. Watoto wake wamekwenda uhamishoni, mateka mbele ya adui. Fahari yote imeondoka kutoka kwa Binti Sayuni. Wakuu wake wako kama ayala ambaye hapati malisho, katika udhaifu wamekimbia mbele ya anayewasaka. Katika siku za mateso yake na kutangatanga, Yerusalemu hukumbuka hazina zote ambazo zilikuwa zake siku za kale. Wakati watu wake walipoanguka katika mikono ya adui, hapakuwepo na yeyote wa kumsaidia. Watesi wake walimtazama na kumcheka katika maangamizi yake. Yerusalemu ametenda dhambi sana kwa hiyo amekuwa najisi. Wote waliomheshimu wanamdharau, kwa maana wameuona uchi wake. Yeye mwenyewe anapiga kite na kugeukia mbali. Uchafu wake umegandamana na nguo zake; hakuwaza juu ya maisha yake ya baadaye. Anguko lake lilikuwa la kushangaza, hapakuwepo na yeyote wa kumfariji. “Tazama, Ee BWANA, teso langu, kwa maana adui ameshinda.” Adui ametia mikono juu ya hazina zake zote, aliona mataifa ya kipagani wakiingia mahali patakatifu pake, wale uliowakataza kuingia kwenye kusanyiko lako. Watu wake wote wanalia kwa uchungu watafutapo chakula; wanabadilisha hazina zao kwa chakula ili waweze kuendelea kuishi. “Tazama, Ee BWANA, ufikiri, kwa maana nimedharauliwa.”
Maombolezo 1:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Jinsi mji huu ukaavyo ukiwa, Huo uliokuwa umejaa watu! Jinsi alivyokuwa kama mjane, Yeye aliyekuwa mkuu kati ya mataifa! Binti mfalme kati ya majimbo, Jinsi alivyoshikwa shokoa! Hulia sana wakati wa usiku, Na machozi yake yapo mashavuni; Miongoni mwa wote waliompenda Hakuna hata mmoja amfarijiye; Rafiki zake wote wamemtenda hila, Wamekuwa adui zake. Yuda amehamishwa kwa sababu ya kuonewa, Na kwa sababu ya utumwa mkuu; Anakaa kati ya makafiri, Haoni raha iwayo yote; Wote waliomfuata wamempata Katika dhiki yake. Njia za Sayuni zaomboleza, Kwa kuwa hakuna ajaye kwa sikukuu; Malango yake yote yamekuwa ukiwa, Makuhani wake hupiga kite; Wanawali wake wanahuzunika; Na yeye mwenyewe huona uchungu. Watesi wake wamekuwa kichwa, Adui zake hufanikiwa; Kwa kuwa BWANA amemtesa Kwa sababu ya wingi wa makosa yake; Watoto wake wadogo wamechukuliwa mateka Mbele yake huyo mtesi. Naye huyo binti Sayuni Enzi yake yote imemwacha; Wakuu wake wamekuwa kama ayala Wasioona malisho; Nao wamekwenda zao hawana nguvu Mbele yake anayewafuatia. Siku za mateso na misiba yake, Yerusalemu huyakumbuka matamaniko yake yote Yaliyokuwa tangu siku za kale; Hapo watu wake walipoanguka mikononi mwa mtesi, Wala hakuna hata mmoja wa kumsaidia; Hao watesi wake walimwona, Wakafanya sabato zake kuwa mzaha. Yerusalemu amefanya dhambi sana; Kwa hiyo amekuwa kama kitu kichafu; Wote waliomheshimu wanamdharau, Kwa sababu wameuona uchi wake; Naam, yeye anaugua, Na kujigeuza aende nyuma. Uchafu wake ulikuwa katika marinda yake; Hakukumbuka mwisho wake; Kwa hiyo ameshuka kwa ajabu; Yeye hana mtu wa kumfariji; Tazama, BWANA, teso langu; Maana huyo adui amejitukuza. Huyo mtesi amenyosha mkono wake Juu ya matamaniko yake yote; Maana ameona ya kuwa makafiri wameingia Ndani ya patakatifu pake; Ambao kwa habari zao wewe uliamuru Wasiingie katika kusanyiko lako. Watu wake wote hupiga kite, Wanatafuta chakula; Wameyatoa matamaniko yao wapate chakula Cha kuihuisha nafsi; Ee BWANA, tazama, uangalie; Kwa maana mimi nimekuwa mnyonge.