Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Maombolezo 1:12-22

Maombolezo 1:12-22 Biblia Habari Njema (BHN)

“Enyi wapita njia, hivi hamjali kitu? Tazameni! Hakuna aliyepatwa na uchungu kama mimi, uchungu alioniletea Mwenyezi-Mungu, siku ya hasira yake kali. “Aliteremsha moto kutoka juu, ukanichoma hata mifupani mwangu. Alinitegea wavu akaninasa, kisha akanirudisha nyuma, akaniacha nimeduwaa na kuzirai mchana kutwa. “Aliyahesabu makosa yangu yote akayakusanya mahali pamoja; aliyafunga shingoni mwangu kama nira, nikafyonzwa nguvu zangu kwa uzito wake. Mwenyezi-Mungu aliniweka mikononi mwao watu ambao siwezi kuwapinga. “Mwenyezi-Mungu aliwakataa askari walionilinda, alitangaza wakati maalumu wa kuniadhibu kuwaponda vijana wangu wa kiume. Aliwaponda kama katika shinikizo watu wangu wa Yuda. “Kwa sababu ya hayo ninalia, machozi yanitiririka, sina mtu yeyote wa kunifariji; hakuna yeyote wa kunitia moyo. Watoto wangu wameachwa wakiwa, maana adui yangu amenishinda. “Nainyosha mikono yangu lakini hakuna wa kunifariji. Mwenyezi-Mungu ametoa amri dhidi yangu mimi Yakobo, jirani zangu wawe maadui zangu. Naam, mimi Yerusalemu nimekuwa kinyaa kwao. “Lakini Mwenyezi-Mungu amefanya sawa kwa maana nimeliasi neno lake. Nisikilizeni enyi watu wote, yatazameni mateso yangu. Wasichana wangu na wavulana wangu, wamechukuliwa mateka. “Niliwaita wapenzi wangu, lakini wao wakanihadaa. Makuhani na wazee wangu wamefia mjini wakijitafutia chakula, ili wajirudishie nguvu zao. “Ona, ee Mwenyezi-Mungu nilivyo taabuni. Roho yangu imechafuka, moyo wangu unasononeka kwani nimekuasi vibaya. Huko nje kumejaa mauaji, ndani nako ni kama kifo tu. “Sikiliza ninavyopiga kite; hakuna wa kunifariji. Maadui zangu wote wamesikia juu ya taabu yangu: Wanafurahi kwamba umeniletea maafa. Uifanye ile siku uliyoahidi ifike, uwafanye nao wateseke kama mimi. “Uwapatilize kwa ajili ya uovu wao wote. Uwatende kama ulivyonitenda mimi kwa sababu ya makosa yangu yote. Nasononeka sana kwa maumivu na moyo wangu unazimia.”

Maombolezo 1:12-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Je! Si kitu kwenu, enyi nyote mpitao njia, Angalieni, mtazame Kama kuna majonzi yoyote mfano wa majonzi yangu, Niliyotendwa mimi, Ambayo BWANA amenihuzunisha kwa hayo Siku ya hasira yake iwakayo. Toka juu amepeleka moto mifupani mwangu, Nao umeishinda; Ametandika wavu aninase miguu, Amenirudisha nyuma; Amenifanya kuwa mtu wa pekee, Na mgonjwa mchana kutwa. Kongwa la makosa yangu limefungwa na mkono wake; Hayo yameshikamana; Yamepanda juu shingoni mwangu; Amezikomesha nguvu zangu; Bwana amenitia mikononi mwao, Ambao siwezi kupingamana nao. Bwana amewafanya mashujaa wangu wote Kuwa si kitu kati yangu; Ameita mkutano mkuu kinyume changu Ili kuwaponda vijana wangu; Bwana amemkanyaga kama shinikizoni Huyo bikira binti Yuda. Mimi ninayalilia mambo hayo; Jicho langu, jicho langu linachuruzika machozi; Kwa kuwa mfariji yuko mbali nami, Ambaye ilimpasa kunihuisha nafsi; Watoto wangu wameachwa peke yao, Kwa sababu huyo adui ameshinda. Sayuni huinyosha mikono yake; Hakuna hata mmoja wa kumfariji; BWANA ametoa amri juu ya Yakobo, Kwamba wamzungukao wawe watesi wake; Yerusalemu amekuwa kati yao Kama kitu kichafu. BWANA ndiye mwenye haki; Maana nimeiasi amri yake; Sikieni, nawasihi, enyi watu wote, Mkayatazame majonzi yangu; Wasichana wangu na wavulana wangu Wamechukuliwa mateka. Niliwaita hao walionipenda Lakini walinidanganya; Makuhani wangu na wazee wangu Walifariki mjini; Hapo walipokuwa wakitafuta chakula ili kuzihuisha nafsi zao. Angalia, Ee BWANA; maana mimi ni katika dhiki; Mtima wangu umetaabika; Moyo wangu umegeuka ndani yangu; Maana nimeasi vibaya sana; Huko nje upanga huua watu; Nyumbani mna kama mauti. Wamesikia kwamba napiga kite; Hakuna hata mmoja wa kunifariji; Adui zangu wote wamesikia habari ya mashaka yaliyonipata; Hufurahi kwa kuwa umeyafanya hayo; Utaileta siku ile uliyoitangaza, Nao watakuwa kama mimi. Huo uovu wao wote Na uje mbele zako wewe; Ukawatende wao kama ulivyonitenda mimi Kwa dhambi zangu zote; Kwa maana mauguzi yangu ni mengi sana, Na moyo wangu umezimia.

Maombolezo 1:12-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Je! Si kitu kwenu, enyi nyote mpitao njia, Angalieni, mtazame Kama kuna majonzi yo yote mfano wa majonzi yangu, Niliyotendwa mimi, Ambayo BWANA amenihuzunisha kwa hayo Siku ya hasira yake iwakayo. Toka juu amepeleka moto mifupani mwangu, Nao umeishinda; Ametandika wavu aninase miguu, Amenirudisha nyuma; Amenifanya kuwa mtu wa pekee, Na mgonjwa mchana kutwa. Kongwa la makosa yangu limefungwa na mkono wake; Hayo yameshikamana; Yamepanda juu shingoni mwangu; Amezikomesha nguvu zangu; Bwana amenitia mikononi mwao, Ambao siwezi kupingamana nao. Bwana amewafanya mashujaa wangu wote Kuwa si kitu kati yangu; Ameita mkutano mkuu kinyume changu Ili kuwaponda vijana wangu; Bwana amemkanyaga kama shinikizoni Huyo bikira binti Yuda. Mimi ninayalilia mambo hayo; Jicho langu, jicho langu linachuruzika maji; Kwa kuwa mfariji yu mbali nami, Ambaye ilimpasa kunihuisha nafsi; Watoto wangu wameachwa peke yao, Kwa sababu huyo adui ameshinda. Sayuni huinyosha mikono yake; Hakuna hata mmoja wa kumfariji; BWANA ametoa amri juu ya Yakobo, Kwamba wamzungukao wawe watesi wake; Yerusalemu amekuwa kati yao Kama kitu kichafu. BWANA ndiye mwenye haki; Maana nimeiasi amri yake; Sikieni, nawasihi, enyi watu wote, Mkayatazame majonzi yangu; Wasichana wangu na wavulana wangu Wamechukuliwa mateka. Naliwaita hao walionipenda Lakini walinidanganya; Makuhani wangu na wazee wangu Walifariki mjini; Hapo walipokuwa wakitafuta chakula ili kuzihuisha nafsi zao. Angalia, Ee BWANA; maana mimi ni katika dhiki; Mtima wangu umetaabika; Moyo wangu umegeuka ndani yangu; Maana nimeasi vibaya sana; Huko nje upanga hufisha watu; Nyumbani mna kama mauti. Wamesikia kwamba napiga kite; Hakuna hata mmoja wa kunifariji; Adui zangu wote wamesikia habari ya mashaka yaliyonipata; Hufurahi kwa kuwa umeyafanya hayo; Utaileta siku ile uliyoitangaza, Nao watakuwa kama mimi. Huo uovu wao wote Na uje mbele zako wewe; Ukawatende wao kama ulivyonitenda mimi Kwa dhambi zangu zote; Kwa maana mauguzi yangu ni mengi sana, Na moyo wangu umezimia.

Maombolezo 1:12-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

“Je, si kitu kwenu, ninyi nyote mpitao kando? Angalieni kote mwone. Je, kuna maumivu kama maumivu yangu yale yaliyotiwa juu yangu, yale BWANA aliyoyaleta juu yangu katika siku ya hasira yake kali? “Kutoka juu alipeleka moto, akaushusha katika mifupa yangu. Aliitandia wavu miguu yangu na akanirudisha nyuma. Akanifanya mkiwa, na mdhaifu mchana kutwa. “Dhambi zangu zimefungwa kwenye nira, kwa mikono yake zilifumwa pamoja. Zimefika shingoni mwangu na Bwana ameziondoa nguvu zangu. Amenitia mikononi mwa wale ambao siwezi kushindana nao. “Bwana amewakataa wapiganaji wa vita wote walio kati yangu, ameagiza jeshi dhidi yangu kuwaponda vijana wangu wa kiume. Katika shinikizo lake la divai Bwana amemkanyaga Bikira Binti Yuda. “Hii ndiyo sababu ninalia na macho yangu yanafurika machozi. Hakuna yeyote aliye karibu kunifariji, hakuna yeyote wa kuhuisha roho yangu. Watoto wangu ni wakiwa kwa sababu adui ameshinda.” Sayuni ananyoosha mikono yake, lakini hakuna yeyote wa kumfariji. BWANA ametoa amri kwa ajili ya Yakobo kwamba majirani zake wawe adui zake; Yerusalemu umekuwa kitu najisi miongoni mwao. “BWANA ni mwenye haki, hata hivyo niliasi dhidi ya amri yake. Sikilizeni, enyi mataifa yote, tazameni maumivu yangu. Wavulana wangu na wasichana wangu wamekwenda uhamishoni. “Niliita washirika wangu lakini walinisaliti. Makuhani wangu na wazee wangu waliangamia mjini walipokuwa wakitafuta chakula ili waweze kuishi. “Angalia, Ee BWANA, jinsi nilivyo katika dhiki! Nina maumivu makali ndani yangu, nami ninahangaika moyoni mwangu, kwa kuwa nimekuwa mwasi sana. Huko nje, upanga unaua watu, ndani, kipo kifo tu. “Watu wamesikia ninavyolia kwa uchungu, lakini hakuna yeyote wa kunifariji. Adui zangu wote wamesikia juu ya dhiki yangu, wanafurahia lile ulilolitenda. Naomba uilete siku uliyoitangaza ili wawe kama mimi. “Uovu wao wote na uje mbele zako; uwashughulikie wao kama vile ulivyonishughulikia mimi kwa sababu ya dhambi zangu zote. Kulia kwangu kwa uchungu ni kwingi na moyo wangu umedhoofika.”