Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Maombolezo 2:1-12

Maombolezo 2:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Jinsi Bwana alivyomfunika binti Sayuni Kwa wingu katika hasira yake! Ameutupa toka mbinguni hata nchi Huo uzuri wa Israeli; Wala hakukikumbuka kiti cha miguu yake Katika siku ya hasira yake. Bwana ameyameza makao yote ya Yakobo, Wala hakuona huruma; Ameziangusha ngome za binti Yuda Katika ghadhabu yake; Amezibomoa hata nchi Ameunajisi ufalme na wakuu wake. Ameikata pembe yote ya Israeli Katika hasira yake kali; Ameurudisha nyuma mkono wake wa kulia Mbele ya hao adui, Naye amemteketeza Yakobo kama moto uwakao, Ulao pande zote. Ameupinda upinde wake kama adui, Amesimama na mkono wake wa kulia kama mtesi; Naye amewaua hao wote Waliopendeza macho; Katika hema ya binti Sayuni Amemimina ghadhabu yake kama moto. Bwana amekuwa mfano wa adui, Amemmeza Israeli; Ameyameza majumba yake yote, Ameziharibu ngome zake; Tena amemzidishia binti Yuda Matanga na maombolezo. Naye ameondoa maskani yake kwa nguvu, Kana kwamba ni ya bustani tu; Ameziharibu sikukuu zake; BWANA amezisahaulisha katika Sayuni Sikukuu na sabato; Naye amewadharau mfalme na kuhani Katika uchungu wa hasira yake. Bwana ameitupilia mbali madhabahu yake, Amepachukia patakatifu pake; Amezitia katika mikono ya hao adui Kuta za majumba yake; Wamepiga kelele ndani ya nyumba ya BWANA Kama katika sikukuu. BWANA amekusudia kuuharibu Ukuta wa binti Sayuni; Ameinyosha hiyo kamba, Hakuuzuia mkono wake usiangamize; Bali amefanya boma na ukuta kuomboleza; Zote pamoja hudhoofika. Malango yake yamezama katika nchi; Ameyaharibu makomeo yake na kuyavunja; Mfalme wake na wakuu wake wanakaa Kati ya mataifa wasio na sheria; Naam, manabii wake hawapati maono Yatokayo kwa BWANA. Wazee wa binti Sayuni huketi chini, Hunyamaza kimya; Wametupa mavumbi juu ya vichwa vyao, Wamejivika viunoni nguo za magunia; Wanawali wa Yerusalemu huinama vichwa vyao Kuielekea nchi. Macho yangu yamechoka kwa machozi, Mtima wangu umetaabika; Ini langu linamiminwa juu ya nchi Kwa uharibifu wa binti ya watu wangu; Kwa sababu watoto wachanga na wanyonyao, Huzimia katika mitaa ya mji. Wao huwauliza mama zao, Ziko wapi nafaka na divai? Hapo wazimiapo kama waliojeruhiwa Katika mitaa ya mji, Hapo walipomiminika nafsi zao Vifuani mwa mama zao.

Maombolezo 2:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Tazama jinsi Bwana alivyomfunika Binti Sayuni kwa wingu la hasira yake! Ameitupa chini fahari ya Israeli kutoka mbinguni mpaka duniani, hakukumbuka kiti chake cha kuwekea miguu katika siku ya hasira yake. Bila huruma Bwana ameyameza makao yote ya Yakobo; katika ghadhabu yake amebomoa ngome za Binti Yuda. Ameuangusha ufalme wake na wakuu wake chini kwa aibu. Katika hasira kali amevunja kila pembe ya Israeli. Ameuondoa mkono wake wa kuume alipokaribia adui. Amemteketeza Yakobo kama moto uwakao ule uteketezao kila kitu kinachouzunguka. Ameupinda upinde wake kama adui, mkono wake wa kuume uko tayari. Kama vile adui amewachinja wote waliokuwa wanapendeza jicho, amemwaga ghadhabu yake kama moto juu ya hema la Binti Sayuni. Bwana ni kama adui; amemmeza Israeli. Amemeza majumba yake yote ya kifalme na kuangamiza ngome zake. Ameongeza huzuni na maombolezo kwa ajili ya Binti Yuda. Ameharibu maskani yake kama bustani, ameharibu mahali pake pa mkutano. BWANA amemfanya Sayuni kusahau sikukuu zake zilizoamriwa na Sabato zake; katika hasira yake kali amewadharau mfalme na kuhani. Bwana amekataa madhabahu yake na kuacha mahali patakatifu pake. Amemkabidhi adui kuta za majumba yake ya kifalme; wamepiga kelele katika nyumba ya BWANA kama katika siku ya sikukuu iliyoamriwa. BWANA alikusudia kuangusha ukuta uliomzunguka Binti Sayuni. Ameinyoosha kamba ya kupimia na hakuuzuia mkono wake usiangamize. Alifanya maboma na kuta ziomboleze, vyote vikaharibika pamoja. Malango yake yamezama ardhini, makomeo yake ameyavunja na kuyaharibu. Mfalme wake na wakuu wake wamepelekwa uhamishoni miongoni mwa mataifa, sheria haipo tena, na manabii wake hawapati tena maono kutoka kwa BWANA. Wazee wa Binti Sayuni wanaketi chini kimya, wamenyunyiza mavumbi kwenye vichwa vyao na kuvaa nguo za gunia. Wanawali wa Yerusalemu wamesujudu hadi ardhini. Macho yangu yamedhoofika kwa kulia, nina maumivu makali ndani, moyo wangu umemiminwa ardhini kwa sababu watu wangu wameangamizwa, kwa sababu watoto na wanyonyao wanazimia kwenye barabara za mji. Wanawaambia mama zao, “Wapi mkate na divai?” wazimiapo kama watu waliojeruhiwa katika barabara za mji, maisha yao yadhoofikavyo mikononi mwa mama zao.

Maombolezo 2:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu, kwa hasira yake, amewaweka watu wa Siyoni gizani. Fahari ya Israeli ameibwaga chini. Siku ya hasira yake alilitupilia mbali hata hekalu lake. Mwenyezi-Mungu ameharibu bila huruma makazi yote ya wazawa wa Yakobo. Kwa ghadhabu yake amezibomoa ngome za watu wa Yuda. Ufalme wao na watawala wake ameuporomosha chini kwa aibu. Nguvu yote ya Israeli ameivunja kwa hasira. Hakunyosha mkono kuwasaidia walipokutana na adui; amewawakia watu wa Yakobo kama moto, akateketeza kila kitu. Amevuta upinde wake kama adui, na kuuweka mkono wake wa kulia tayari, amewaua wote tuliowaonea fahari katika maskani yetu watu wa Siyoni. Ametumiminia hasira yake kama moto. Mwenyezi-Mungu amekuwa kama adui, ameangamiza watu wa Israeli; majumba yake yote ameyaharibu, ngome zake amezibomoa. Amewazidishia watu wa Yuda matanga na maombolezo. Hekalu lake amelibomoa kama kitalu bustanini, maskani yake ameiharibu. Amefutilia mbali sikukuu na Sabato huko Siyoni, kwa hasira yake kuu amewakataa mfalme na makuhani. Mwenyezi-Mungu ameipuuza madhabahu yake na hekalu lake amelikataa. Kuta za majumba mjini amewaachia maadui wazibomoe, wakapiga kelele humo nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu kama kelele za wakati wa sikukuu. Mwenyezi-Mungu alipania kuubomoa ukuta wa mji wa Siyoni; aliupima na kuhakikisha kila kitu kimeharibiwa; minara na kuta za nje ya mji akazifanya ukiwa, zote kwa pamoja zikaangamia. Malango yake yameanguka chini, makomeo yake ameyaharibu na kuyavunjavunja. Mfalme na wakuu wake wako uhamishoni kati ya mataifa. Mwongozo wa sheria umetoweka kabisa, manabii wake hawapati tena maono kutoka kwake Mwenyezi-Mungu. Wazee wa Siyoni wameketi chini kimya, wamejitia mavumbi vichwani na kuvaa mavazi ya gunia. Wasichana wa Yerusalemu wameinamisha vichwa. Macho yangu yamevimba kwa kulia, roho yangu imechafuka. Moyo wangu una huzuni nyingi kwa sababu ya kuangamizwa kwa watu wangu kwa sababu watoto wachanga wanazirai katika barabara za mji. Wanawalilia mama zao: “Wapi chakula, wapi kinywaji?” Huku wanazirai kama majeruhi katika barabara za mjini, na kukata roho mikononi mwa mama zao.

Maombolezo 2:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Jinsi Bwana alivyomfunika binti Sayuni Kwa wingu katika hasira yake! Ameutupa toka mbinguni hata nchi Huo uzuri wa Israeli; Wala hakukikumbuka kiti cha miguu yake Katika siku ya hasira yake. Bwana ameyameza makao yote ya Yakobo, Wala hakuona huruma; Ameziangusha ngome za binti Yuda Katika ghadhabu yake; Amezibomoa hata nchi Ameunajisi ufalme na wakuu wake. Ameikata pembe yote ya Israeli Katika hasira yake kali; Ameurudisha nyuma mkono wake wa kuume Mbele ya hao adui, Naye amemteketeza Yakobo kama moto uwakao, Ulao pande zote. Ameupinda upinde wake kama adui, Amesimama na mkono wake wa kuume kama mtesi; Naye amewaua hao wote Waliopendeza macho; Katika hema ya binti Sayuni Amemimina kani yake kama moto. Bwana amekuwa mfano wa adui, Amemmeza Israeli; Ameyameza majumba yake yote, Ameziharibu ngome zake; Tena amemzidishia binti Yuda Matanga na maombolezo. Naye ameondoa maskani yake kwa nguvu, Kana kwamba ni ya bustani tu; Ameziharibu sikukuu zake; BWANA amezisahauzisha katika Sayuni Sikukuu za makini na sabato; Naye amewadharau mfalme na kuhani Katika uchungu wa hasira yake. Bwana ameitupilia mbali madhabahu yake, Amepachukia patakatifu pake; Amezitia katika mikono ya hao adui Kuta za majumba yake; Wamepiga kelele ndani ya nyumba ya BWANA Kama katika siku ya kusanyiko la makini. BWANA amekusudia kuuharibu Ukuta wa binti Sayuni; Ameinyosha hiyo kamba, Hakuuzuia mkono wake usiangamize; Bali amefanya boma na ukuta kuomboleza; Zote pamoja hudhoofika. Malango yake yamezama katika nchi; Ameyaharibu makomeo yake na kuyavunja; Mfalme wake na wakuu wake wanakaa Kati ya mataifa wasio na sheria; Naam, manabii wake hawapati maono Yatokayo kwa BWANA. Wazee wa binti Sayuni huketi chini, Hunyamaza kimya; Wametupa mavumbi juu ya vichwa vyao, Wamejivika viunoni nguo za magunia; Wanawali wa Yerusalemu huinama vichwa vyao Kuielekea nchi. Macho yangu yamechoka kwa machozi, Mtima wangu umetaabika; Ini langu linamiminwa juu ya nchi Kwa uharibifu wa binti ya watu wangu; Kwa sababu watoto wachanga na wanyonyao, Huzimia katika mitaa ya mji. Wao huwauliza mama zao, Zi wapi nafaka na divai? Hapo wazimiapo kama waliojeruhiwa Katika mitaa ya mji, Hapo walipomiminika nafsi zao Vifuani mwa mama zao.